Sunday, November 18, 2012

Mtaa wa UGOMBOLWA, KATA YA SEGEREYA, WILAYA YA ILALA, DAR ES SALAAM, TANZANIA, WAFUNGA MACHINJIO YA NGURUWE,

Ugombolwa wafunga machinjio ya nguruwe
 
na Betty Kangonga
 
Tz Daima 18 Nov 2012
 
UONGOZI wa Serikali ya Mtaa wa Ugombolwa, Kata ya Segerea, Wilaya ya Ilala, imeyafunga machinjio ya nguruwe kutokana na wamiliki hao kukiuka taratibu za kisheria.
Akizungumza jana mara baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika machinjio hayo yaliyopo katika eneo la makazi, Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Mathew Mayonga aliyeambatana na uongozi wa mtaa huo, alisema amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha na ukiukwaji wa taratibu.
Alisema kuwa amelazimika kuyafunga machinjio hayo na kuwasilisha zuio la mahakama kutokana na uongozi wa mtaa huo kutokuwa na taarifa juu ya uwepo wa machinjia hayo katika eneo hilo.
“Yaani naomba kuanzia sasa msimamishe zoezi la uchinjaji na muuze nyama zilizokwisha andaliwa…na kama mtakiuka utaratibu huo nina hakika nitapata maelezo na hapo ninajua nini hatua ya kuchukua,” alisema.
Mayonga, alisema kuwa wamiliki hao hawana nyaraka zozote zinazowahitaji kufanya shughuli hiyo hivyo hata uandaaji wa nyama hiyo unaweza kuwa na dosari.
Alisema baada ya kukagua mazingira yanayolizunguka eneo hilo alibaini utitirishwaji hovyo wa maji machafu ambao umekuwa kero kubwa kwa majirani wanaoishi eneo hilo.
“Mnawezaje kufanya kazi wakati hakuna nyaraka zinazowataka kufanya hivyo kwa kweli naomba msimamishe haraka hadi mtakapopata barua rasmi la kutakiwa kufanya shughuli hiyo,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa mtaa huo, Mariam Machicha, alisema kuwa hiyo ni mara ya pili kufika katika eneo hilo na mara ya kwanza walilazimika kulifungia eneo hilo lakini wakashangaa kwa kufunguliwa tena.
“Hii ni mara ya pili nafika hapa…mara ya kwanza tulilifunga lakini cha ajabu likafunguliwa kinyemela,” alisema
Akijitetea Katibu wa Umoja wa wadau wa nguruwe Manispaa ya Ilala, Daudi Charles, alisema kuwa ofisa mifugo wa wilaya hiyo aliwataka kuendelea na biashara hiyo huku akiendelea kuwatafutia vibali.
 

No comments:

Post a Comment