Wednesday, June 18, 2014

WACHA BIBLIA ISEME na ALI MUHSIN [TANZANIA]


Imetundikwa hapa leo 19/6/2014.
Wacha Biblia Iseme
Yaliyomo


Wacha Biblia Iseme
Imetungwa na Sheikh Ali Muhsin

Bismillahi Arrahmani Arrahim
Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehema Mwenye Kurehemu

SHUKRANI

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniongoza Njia iliyonyooka.
Pia nampa ahsante Bw. Kingsley Green, Mwalimu wa biology wa asli ya Kiaustralia aliyekuwa akisomesha Mazengo Secondary School, Dodoma, Tanzania, ambaye kwa kuwa ni mhubiri alikuwa akija kutuzuru gerezani tulipokuwa tumewekwa kizuizini baada ya kupinduliwa serikali yetu ya Zanzibar.  Kwake yeye nilijifunza kuisoma Biblia kwa nidhamu.

Hali kadhaalika nawapa ahsante wahubiri wengi wa Kikristo waliokuwa wakituhubiria nilipokuwako Chuo Kikuu Makerere, na nilipokuwako kizuizini. Kwa wanafunzi wenzangu na wafungwa wenzangu ambao nikijadiliana nao kirafiki katika mambo ya dini nina  deni kubwa la shukrani.

Ni waajibu wangu kushukuru Shirika la Kimataifa la Msamaha (Amnesty International) kwa kuniletea vitabu nilipokuwa kizuizini, ambavyo vitabu hivyo vimenisaidia sana kunizidishia  maarifa juu ya mawazo ya Kikristo ya hivi sasa.

Sina fadhila ya kumlipa Baba yangu mzazi, Sheikh Muhsin bin Ali Barwani (ambaye kwake ndio nimesoma sana ilimu za dini ya Kiislamu), na kaka yangu Sheikh Muhammad Muhsin, na mashekhe na walimu kadhaa wa kadhaa wengineo niliosoma kwao.  Miongoni mwa hao ni Sheikh Abubakar Baakathir, Sheikh Muhammad bin Omar Al Khatib, Sheikh Suleiman Al Alawy, Sheikh Burhan Mkelle, Sheikh Abdulrahman Muhammad Al Kindy, Sheikh Said bin Abdulla Lindi, na Sheikh Abdulla Saleh Al Farsy. Pia nawashukuru kwa kuniongoza kwa nasaha na mifano Habib Omar bin Sumeit, Sayyid Ahmed bin Husein, Sheikh Abdulla Muhammad Al-Hadhramy, Sheikh Muhammad Abubakar, Sheikh Muhammad Salim Barwani (Jinja), Sayyid Hamid Mansab na Sheikh Abdulla bin Suleiman Al Harthy. Sina la kuwalipa ila kuwaombea Mwenyezi Mungu awarehemu, na kama itapatikana faida yo yote kwa walionifundisha basi thawabu zake zirejee kwao mashekhe na walimu wangu niliowataja na nisiowataja.

Mwishoni siwezi ila kumshukuru mwenzangu wa maisha, mzazi mwenzangu, Azza bint Muhammad bin Seif, ambaye kwa subira yake na ushujaa wake na imani yake iliyo kubwa, ndio nikaweza kubeba taabu za kizuizi zaidi ya miaka kumi, huku yeye peke yake akijitazama mwenyewe na watoto wetu, naye yupo uhamishoni kama ni mkimbizi katika nchi ya ugeni Misri.  Ingelikuwa si yeye na wema wa wahisani wetu wa Kimisri, na khasa  katika wao Dr. Abdoh Sallam, Bw. Fathi Sabri, Dr. Mustafa Momen, Dr. Farid Abul Ezz, Bw. Hilmy Shaarawy, Bw. Bahgat Disouqy na Dr. Muhammad Abdul-Aziz Is'haq, mimi nisingekuwa na tamakuni ya moyo hata nikaweza kusoma nilikosoma, kuchungua nilikochungua, na kuandika nilikoandika nami nimo katika utumwa wa kifungoni.

Taarikh 2 Ramadhani mwaka 1409 A.H. iliyo wafikiana na 7 Aprili 1989, mwenzangu wa miaka 45, Mama Azza, aliniacha mkono, Mwenyezi Mungu akamkhitari. Shida na taabu zilizo mpata kwa yaliyo tokea kwetu, na kifungo changu, na maisha ya ukimbizi kwa robo karne, yalimuathiri afya yake sana na mwisho ndio akanitoka katika umri wa miaka 63.

Fadhila ya uchapishaji kitabu hichi kwa Kiswahili na kabla yake kwa Kiingereza inarejea kwa Muislamu mtenda wema, Dr. Moawiyah Shunnar wa Dubai, Mwenyezi Mungu amjaze kila kheri.


DIBAJI

Kuzozana sio makusudio ya kuandika Risala hii.  Makusudio ya hakika ni kutaka kuwapa mwangaza Wakristo na Waislamu ambao katika sehemu nyingi za ulimwengu inawapasa waishi kama ni wananchi wamoja na jirani.  Inatumainiwa pindi wakinawirika, na kila mmoja akaifahamu vyema misingi ya imani ya mwenziwe, wote watakuja thamini ule msingi mmoja unaowaunga wote kwenye Imani ya asli, nayo ndiyo Dini ya Ulimwengu mzima inayofunza kila mwanaadamu ajisalimu kwa ukamilifu wake kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mmoja wa kweli, kwani hapo ndipo unapotegemea mwendo mwema wa binaadamu.

Kwa bahati mbaya Yesu Kristo (Isa Masihi) hakutuachia mafunzo yake kwa maandishi ya kutegemewa kama alivyofanya Nabii Muhammad. Katika Qur'ani utakuta mafunzo ya Kiislamu yaliyo safi kabisa, yasiyo na chembe ya ila au wasiwasi.  Hatukutii katika Injili mfano wa hayo. Hizo ziitwazo Injili zaweza kulinganishwa na Hadithi za Mtume, bali khasa ni kama Sira Nabawiya, yaani Hadithi za Maisha ya Mtume, ni kama vitabu vya Maulidi.
Inakubaliwa na Wakristo wenyewe kuwa katika maneno na vitendo vya Yesu, kama inavyoelezwa katika Biblia, yamo mengi ambayo si ya kweli, na si ya kutegemewa, kama yalivyokuwepo katika Hadithi za Mtume kabla ya kuchujwa na kun'golewa hadithi na khabari zilizo dhaifu na kuthibitishwa zenye nguvu, Sahihi.  Haikataliki kuwa kwa sababu za kimadhehebu na sababu nyenginezo za mfarakano hadithi nyingi ziliwahi kubuniwa na kusingiziwa kuwa ni za Mtume, hali Mtume hakukhusika nazo kabisa.
Wachunguzi wa haki lazima wakiri kuwa katika kuzichambua na kuzikusanya Hadithi za Mtume Muhammad kulikuwepo mwendo bora zaidi wa kitaalamu kuliko uliokuwapo zilipoteuliwa hizi Injili ziliomo katika Biblia.  Hao wanazuoni wakubwa - Maimamu - waliotumia maisha yao yote katika kukusanya Hadithi, yaani semi na vitendo vya Mtume Muhammad, walifanya kila juhudi waliyokuwa nayo (yaani Ijtihad) wakitumia vipimo vya ilimu (scientific methodology) kuhakikisha ukweli na umadhubuti wa kila kauli na kila kitendo cha Mtume.  Kila Hadithi waisikiayo waliichungua na kuipekua kwa nani imepokelewa, na huyo naye kaipokea kwa nani, na tena kwa nani, mpaka kwa aliyeipata kwa mwenyewe Mtume.  Kila kiungo katika mnyororo wa wapokeaji uwe madhubuti sawa sawa kwa kila njia. Maisha ya kila mmoja ya wapokeaji yalilazimu kusomwa na yadurusiwe, na yachunguzwe kwa uangalifu kamili, mpaka uthibiti bila ya shaka yo yote uaminifu wake wa kupokea na kusimulia khabari kwa kweli bila ya kuzidisha wala kupunguza.  Hiyo peke yake ni ilimu iliyotungiwa vitabu kwa vitabu.  Tena huchunguzwa lugha - jee, ni ndio lugha namna hiyo na mbinu zake kama ilivyokuwa ikitumika Makka na Madina katika zama za Mtume?  Ni kweli ndiyo namna ya lugha alivyokuwa mwenyewe Mtume akijuulikana kutumia?  Pia huchunguzwa kuwa hayo maneno anayoambiwa Mtume kayasema, au vitendo kavitenda, havigongani kwa namna yo yote na mafunzo yaliomo katika Qur'ani? Kwani Qur'ani ndicho kipimo madhubuti kabisa.  Hayagongani na hakika ya mambo yanavyojuulikana kikweli bila ya khitilafu? Kwa njia hizi na nyenginezo ndio hao Maimamu waliokusanya Hadithi za Mtume wakizichuja, na zenye shaka wakizitenga kando, na kuziita Dhaifu, au Ziliobuniwa. Ziliopasi ndio wakaziita Sahihi na nzuri.

Lakini juu ya jitahada kuu waliyoifanya hao wanazuoni wa Hadithi bado juhudi yao ni juhudi ya kibinaadamu, na huenda ikakosea. Kwa bahati njema ipo Qur'ani, amabayo ukweli wake haujapata kutolewa kombo na rafiki wala adui.  Kila mtu ameangusha shingo yake mbele ya ukweli wa Qur'ani kuwa hapana mfano wake kitabu cho chote duniani ambacho kimebakia karne nenda karne rudi bila ya mabadiliko yo yote au machafuzi yo yote.  Hapana neno moja lililoongezwa, wala neno moja lililopunguzwa.  Hii Qur'ani iliopo sasa kwa lugha ya Kiarabu (sio tafsiri za maana yake katika lugha mbali mbali) ndio ile ile Qur'ani ambayo Mtume Muhammad aliyowakariria wafwasi wake miaka 1400 iliyopita, na wao wakaihifadhi kwa moyo na kuiandika, na khalafu yake miaka michache tu baada ya kufa kwa Mtume ikakusanywa pamoja kuwa ni Msahafu kama huu tuuonavyo sisi hii leo.  Huu basi ndio msingi usiolegalega, uliojengewa juu yake mafunzo ya Imani ya Kiislamu. Hichi ndicho kipimo cha kupimia usahihi wa Hadithi au Khabari yo yote ya Mtume, na ndio mwamba ambao juu yake limejengwa jengo la Uislamu.

Katika sahifa zifwatazo itaonekana kuwa nimependelea mno kunukulu maneno kutokana na vitabu mbali mbali.  Huu ndio mtindo wangu ninapoandika juu ya jambo muhimu, na khasa jambo lilio muhimu kupita kiasi kama hili la dini.  Sipendelei kuwa miongoni mwa wale "ambao wanaojadili mambo yaliyomkhusu Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu wala kitabu chenye kutoa mwangaza", kama isemavyo Qur'ani.

Nilipokuwa nikiidurusu Biblia katika upweke wa kizuizini katika magereza ya Tanzania nalijaribu kuyatafuta mafunzo ya kweli ya Yesu na Manabii wa Wana wa Israili waliomtangulia. Miaka kumi na miezi mitano ya kizuizi ikawa ni miaka kumi na miezi mitano ya mafunzo ya kweli kweli ya Biblia.  Kwa juhudi na taabu nikawa nabandua, bandu bandu, kidogo kidogo, magamba yaliyoifunika hiyo niliyokuwa nina yakini nayo - Lulu in'gaayo iliyozikwa chini ya magamba.
Nikaigundua.
Basi sasa nawaomba ndugu zangu wa Kiislamu ambao kuujua kwao Ukristo ni juu juu tu, na rafiki zangu wa Kikristo ambao takriban hawajui lo lote la kweli katika Uislamu (na kwa hakika hata Ukristo wa kweli) waje nami, na katika sahifa hizi zifwatazo tuutafute Ukweli.  Tutauona, kwani Ukweli ni Nyumba iliyojengwa juu ya Mwamba, na mvua itaanguka, na pepo zitavuma, lakini Nyumba haitaanguka.  Huko katika Yerusalemu Takatifu walipopaa wote wawili, Muhammad na Yesu, kwa uvuto wa kiroho mpaka wakafikilia Utukufu wake Mola Mlezi, kuna ishara ya dhaahiri inayotoa mwanga wa kuenea kote kote, ishara ya Ukweli unaomuamrisha Mwislamu na Mkristo kumsujudia Mwenyezi Mungu yule yule ambaye anaabudiwa kwa hamu na unyenyekevu sawasawa katika Msikiti ulio juu ya Mwamba na katika Kanisa la Kaburi Takatifu.  Ukweli huu unatuamrisha tuache mila za binaadamu na tufuate amri za Mwenyezi Mungu.  Ukweli huu unatuamrisha tuache mtindo wa kuigawa Dini katika vikundi vikundi  vya madhehebu na tuushikilie Umoja wa Mungu (Tawhid) unaotuunga sote pamoja.  Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani:
 Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka. Na tulimfanya Mwana wa Maryamu na mama yake kuwa Ishara na tukawapa makimbilio kwenda mahali polipoinuka penye utulivu na chemchem za maji.
Enyi Mitume!   Kuleni vyakula vizuri na fanyeni mema, hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
Na kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.
Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali.  Kila kundi likafurahia kwa waliyo nayo.
 Basi waache katika ghafla yao kwa muda.

Tusitangetange ovyo katika vichochoro vya makosa na hali Njia safi Iliyonyooka iko wazi machoni mwetu. Tujifunze ukweli kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu. Tufahamiane na tukubaliane kuwa kila mmoja wetu kwa dhati ya nafsi yake atafanya juhudi  kuutafuta Ukweli, kwani Ukweli ndio utaotupa uzima. 

Ali Muhsin Al Barwani



1- MAFUNZO YA KANISA

Maana ya neno "Kanisa" ni mkusanyiko wa Wakristo, au khasa ni mapadri ambao wamejipa kazi ya kutengeneza imani na ibada na vile vile kutoa huduma maalumu za kidini kwa kufuata yale yanayoaminiwa kuwa ni mafunzo ya Yesu Kristo.  "Kanisa" yaweza kuwa vile vile na maana ya madhehebu fulani ambayo Mkristo anaikubali na kuifuata, kama vile Kanisa la Kikatoliki, la Kianglikana, la Kiluteri n.k. Mbali na kuwa neno "Kanisa" pia lina maana ya kawaida ya kuwa ni jengo la ibada la Wakristo, kama ulivyokuwa Msikiti kwa Waislamu, na Hekalu kwa wengineo.

Takriban makanisa yote, au madhehebu zote za Kikristo, zinashikilia itikadi hizi zifwatazo bila ya wasiwasi wo wote au kutaka kusaili cho chote. 
Imani kama hizo huitwa "Dogma", yaani imani za kuaminiwa bila ya kusailiwa kuwa zaingia akilini  au la:

1.    Yupo Mungu Mmoja.
2.    Katika Mungu zipo Nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Nafsi hizi tatu zinaitwa Utatu Mtakatifu.  Zote Nafsi tatu ni sawa, zote ni za milele, yaani hazina mwanzo wala hazina mwisho.  Hizo si miungu mitatu, bali ni Mungu Mmoja.
3.    Baba ni Mungu na ndiye Nafsi ya kwanza katika Utatu Mtakatifu.
4.    Mwana ni Mungu na ndiye Nafsi ya pili katika Utatu. Yeye ni Yesu Kristo ambaye ni Mungu aliyekuja kwa sura ya mtu. Hakuumbwa, lakini alizaliwa na Bikra Maria yapata karibu miaka elfu mbili iliyopita katika nchi ya Palastina, akasalibiwa, akafa na akafufuka kutoka wafu siku ya tatu. Kifo chake na mateso yake msalabani yalikusudiwa kuwa ni kafara ili dhambi za wanaadamu zisamehewe.  Hii ndiyo yaitwa Kafara ya Yesu, na kwa hivyo yeye anaitwa Mwokozi.
5.   Roho Mtakatifu ni nafis ya tatu ya Utatu Mtakatifu.  Baada ya kufa kwa Yesu Kristo, Roho Mtakatifu aliwateremkia "Mitume" (wale wamishinari wa mwanzo) wa Yesu Kristo, na huyo Roho anaendelea kuliongoza Kanisa.
6.   Kila mtoto wa kibinaadamu anayo dhambi, hiyo inayoitwa Dhambi Ya Asili iliyorithiwa kutokana na uasi wa Adam alipovunja amri ya Mungu kumkataza asile tunda, naye akala yeye na mkewe Hawa.
7.   Ubatizo, ibada ya kummichia mtu maji, au kwa mujibu wa baadhi ya madhehebu, kumzamisha mtu katika maji, kuwa ni ishara ya kukubaliwa katika Kanisa, na imani ya Kafara ya Yesu Kristo ni njia pekee ya kuokoka.

Kwa kirasmi itikadi hizo zimo katika hiyo iitwayo Imani ya Mitume. Kinyume na dhana ya wengi kuwa imani hiyo ilianzishwa na hao waitwao Mitume wa Yesu (yaani wafwasi wake aliowatuma), yajuulikana kuwa ilitungwa baadae sana.  Baadhi ya wataalamu wa Kikristo wanasema ilitungwa mwaka 150 baada ya Kristo, wengine katika karne yane.  Kwa sura hii ilivyo sasa ilianza kutumiwa katika  karne ya nane.  Katika Kanisa Katoliki Imani ya Mitume husomwa katika ibada za Misa, katika kubatiza, na penginepo. Katika makanisa ya Kiprotestani husomwa katika ibada za Jumaapili.
Aghlabu ya madhehebu za Kikristo zinaikubali imani hii kama hivi ifwatavyo:
Imani ya Mitume
1.    Namuamini Mungu Baba Mwenye nguvu zote, Muumba Mbingu na ardhi,
2.    Na Yesu Kristo, Mwanawe wa pekee, Bwana wetu,
3.    Aliyechukuliwa mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria,
4.    Akateseka chini ya Pontias Pilato, akasalibiwa, akafa, na akazikwa;
5.    Alishuka Jahannamu; siku ya tatu Alifufuka tena kutoka wafu.
6.    Akapaa Mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, Baba Mwenye nguvu zote;
7.    Kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu;
8.    Naamini: Roho Mtakatifu,
9.    Kanisa Takatifu Katoliki, ushiriki wa watakatifu,
10.  Kusamehewa dhambi,
11. Kufufuka mwili, na
12.  Maisha ya milele.

 Angalia katika 9 hapo juu, neno "Katoliki" lina maana la wote, yaani Wakristo, sio kwa maana la Kanisa la Roma tu, ambalo ndilo linalotumia jina hilo kwa ukamilifu wake: Kanisa Katoliki la Roma.
Sasa na tuyachungue mafunzo ya Kanisa kwa mujibu wa mwangaza wa maandishi ya Biblia ambayo Kanisa la Kikristo kwa jumla linakubali kuwa ni Neno la Mungu lenye mamlaka yote.



2- BIBLIA

Hili neno Biblia ni neno la Kigiriki, na maana yake ni "vitabu". Basi Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vingi ambavyo ndio vinafanya msingi wa imani ya Kikristo.  Inakubaliwa kuwa vitabu hivi vimeandikwa na watu wengi mbali mbali, wajuulikanao na wasiojuulikana.  Lakini hao waandishi wanaaminiwa kuwa walipata ufunuo kutokana na Mwenyezi Mungu, na wameandika walivyoandika chini ya uangalizi na uwongozi wa Mwenyezi Mungu;  kwa hivyo Biblia inaambiwa kuwa ni Neno la Mungu.  Biblia ya Wakatoliki, lakini, kidogo inakhitalifiana na ya Waprotestani.  Ya Wakatoliki ina vitabu 73, na ya Waprotestani ina vitabu 66.

Kwa jumla Biblia imegawika sehemu mbili kubwa, Agano la Kale na Agano Jipya.  Agano la Kale ni vitabu vyote vilivyoandikwa kabla ya kutokea Yesu Kristo.  Vitabu hivi vinaeleza tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, na Adamu na Hawa, historia (taarikh) ya wanaadamu na khasa ya Wana wa Israili, sharia alizopewa Musa na Mwenyezi Mungu, vita vya Mayahudi na jirani zao, mafunzo ya manabii kadhaa wa kadhaa katika Bani Israili yaliyotokana na Mwenyezi Mungu. Isipokuwa kwa baadhi ya vitabu ambavyo hawavikubali hili liitwalo Agano la Kale, kwa jumla, ndio liliokuwa Biblia na mpaka hivi sasa ndio Biblia ya Mayahudi. Mayahudi hawaikubali kabisa sehemu ya pili iitwayo Agano Jipya inayokubaliwa na Wakristo.
  Agano Jipya ni ile sehemu ya Biblia iliyoandikwa baada ya Yesu Kristo.  Sehemu hiyo inakusanya Injili nne. Hizi ziitwazo Injili ziliomo katika Biblia ni vitabu vinavyosimulia maisha ya Yesu Kristo na mafunzo yake. Katika Agano Jipya kipo kitabu  kinachoitwa Matendo ya Mitume, kinachoeleza khabari za wanafunzi wake Yesu aliowatuma kwenda tangaza dini. Pia kipo kitabu kinacho itwa "Ufunuo" chenye kueleza mambo ya ajabu ajabu ambayo yasimuliwa kuwa Yohana alifunuliwa akayaona. Hali kadhaalika zimo barua kadhaa wa kadhaa, nyingi zao ni za Paulo, walizopelekewa watu fulani fulani kuwafunza mambo ya dini. Hizi barua za Paulo, Myahudi aliyetanasari, zinategemewa sana na Wakristo, na ndio msingi wa imani na itikadi zao, hata wengi wapo wanaosema kuwa huu Ukristo tuuonao sasa kwa hakika uliasisiwa na Paulo.

Vitabu viliomo katika Agano la Kale kama vilivyo hivi sasa labda viliandikwa baada ya kurejea Mayahudi kutoka utumwani Babilionia, yaani baada ya mwaka 536 kabla ya Kristo.  Na vitabu vya Agano Jipya vilikusanywa na kukubaliwa na wakuu wa Kanisa katika karne ya nne baada ya Kristo (kiasi 367 A.D.) Injili nne ziliomo katika Agano Jipya, yaani ya Mathayo, ya Marko, ya Luka na ya Yohana, ndizo zilizoteuliwa na kukubaliwa na wakuu wa Kanisa kutokana na Injili nyingi sana ambazo zimekataliwa. Neno "Injili" ni neno la Kigiriki, na maana yake ni "Khabari Njema", kwa kuwa Yesu alikuwa akisema kuwa analeta Khabari Njema, yaani Bishara. Vitabu ambavyo vingeweza kuwa ni sehemu ya Biblia, na kwa hakika vikawa vinakubaliwa kwanza na pengine mpaka sasa na baadhi ya madhehebu za Kikristo, vinaitwa "Apokrifa", yaani "vilivyofichwa".

Sisi tunaposema Biblia tunakusudia vitabu vinavyotambuliwa na madhehebu kuu za Kikristo kuwa ndivyo Neno la Mungu tu.



3- DHAMBI YA ASILI

Katika Agano la Kale kitabu cha kwanza, kinachoitwa Mwanzo, imo hadithi ya kuumbwa mtu na kuanguka kwake.  Hivyo ndivyo inavyosimuliwa alivyoanguka Adam kutokana na kukosa neema:
Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.  Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Mwanzo 2.15-17
Juu ya hivyo lakini Adam kwa kushawishiwa na mkewe, Hawa, aliasi amri ya Mungu na akala matunda ya mti wa ujuzi aliyokatazwa. Mungu akawalaani wote wawili:
Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako;  kwa utungu utazaa watoto;  na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.  Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale;  ardhi imelaaniwa kwa ajili yako;  kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;  michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;  kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata  utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa;  kwa maana u mavumbi wewe, na mavumbini utarudi.
Mwanzo 3.16-19
 Kwa ajili ya dhambi yao hiyo, Kanisa linasema, Adamu na Hawa wakakosa neema ya kutakaswa, haki ya kuwapo Mbinguni na vile vipawa vyao mahsusi;  ndio ikawa waweza kufa, kuteseka, na kuwa na matamanio makubwa kutenda maovu na wakafukuzwa kutoka bustani ya Paradisio (Firdausi).  Kwa sababu ya dhambi ya Adamu wanaadamu wote wakizaliwa wanakosa neema ya utakaso na wanarithi adhabu yake.  Hii ndiyo inayoitwa dhambi ya asili.

Thiologia, yaani ilimu ya Ungu, ya Mtakatifu Paulo iliikuza hiyo imani ya Dhambi ya Asili kuthibitisha imani nyengine, yaani imani ya kuokoka kwa kifo cha Yesu msalabani. Katika barua yake aliyowapelekea Warumi Paulo aliandika hivi:
Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti;  na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;  maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria;  walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja.  Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa;  kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Warumi 5.12-15
Pia vile vile Paulo aliwaandikia Wakorintho:
Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhaalika na katika Kristo wote watahuishwa.
1 Wakorintho 15.22
Paulo anakusudia kusema kuwa wanaadamu wote, wameingia makosani kwa vile Adam alivyovunja amri ya Mwenyezi Mungu, ndio maana ya kufa kwao; mpaka kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo ndiko kumeleta uhai kwa wenye kumuamini kuwa yeye ni Mwana wa Mungu aliyekuja duniani kwa ajili ya kuwaokoa walimwengu kwa kuteswa na kutundikwa msalabani na kufa na kuingia Jahannam na kisha kufufuka na kupaa mbinguni.  Haya ni mafunzo ambayo Paulo amejaribu kufunza katika barua zake.  Lakini imani aliyofunza Paulo ya Dhambi ya Asili ya kurithiwa inapingwa na vifungu vingine kutokana na Biblia.  Katika Kumbukumbu la Torati, kwa mfano (na hicho ni katika vitabu vitano vinavyohisabiwa kuwa ndiyo Torati inayoaminiwa na Mayahudi na Wakristo) Musa anasema:
Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuwawe kwa ajili ya baba zao;  kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
Kumbukumbu 24.16
Hali kadhaalika tunasoma neno la Mungu katika kitabu cha Yeremia:
Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe;  kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
Yeremia 31.29-30
 Tena Neno la Mungu linaendelea kusema katika kitabu cha Ezekieli kwa uwazi zaidi:
Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake?  Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi.  Roho itendayo dhambi, ndiyo itayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe; haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
Ezekieli 18.19-20
Hayo tuliyoyanukulu kutokana na vitabu vya Yeremia na Ezekieli ni maneno ya Bwana Mungu, na yale yaliyotoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati ni maneno ya Musa, ambaye alileta sharia itokayo kwa Bwana Mungu na ambayo Yesu alisema kuwa yeye hakuja kuitengua hata nukta moja bali amekuja kuitimiza tu. Ni wazi kabisa kuwa nadhariya ya Paulo ya dhambi ya asili ya kurithiwa inagongana na neno la Mungu kama lilivyo katika Biblia. Na haya yametajwa na Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:
Au hakuambiwa yaliyomo katika vitabu vya Musa, na vya Ibrahimu aliyetimiza ahadi, ya kwamba habebi mwenye kubeba mzigo wa mwengine?  Na ya kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya? Na kwamba amali yake itaonekana?
 (Qur'ani) An Najm 53.36-40
Katika Injili pia upo ushahidi ya kuwa Yesu mwenyewe anapinga hiyo nadhariya ya imani ya Dhambi ya Asili, yaani wanaadamu wamerithi dhambi aliyotenda Adam:
Hata (yesu) alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?  Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.
Yohana 9.1-3
Neno "Rabi" kama lilivyo hapo juu kuitwa Yesu maana yake kwa lugha ya Kiyahudi ni Maalim au Shekhe, sio kama wanavyotumia Waislamu kuwa ni Mola Mlezi. Hata katika Kiarabu pengine hutumiwa kwa maana ya "bwana", kama kusema: Rabbi lbait, yaani Bwana wa nyumba.
Kinyume na mafunzo ya Kanisa linalojiita kwa jina lake, ya kwamba watoto wote waliozaliwa wamezaliwa katika dhambi, mwenyewe Yesu Kristo anathibitisha kuwa watoto hawana dhambi. Tunaona hayo zaidi katika maneno haya yaliyotajwa katika Injili ya Mathayo:
Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
     Mathayo 18.2-3
Maana ya maneno hayo ya Yesu ni kuwa vitoto havina dhambi ya kurithi wala yo yote. Kwa hivyo nini linalolazimisha kuwa mtoto hataokoka ila abatizwe? Au kuwa kila mtu anahesabiwa kuwa ana dhambi mpaka aamini kuwa Mwenyezi Mungu kamgeuza mwanawe wa pekee auliwe kama dhabihu kondoo imwagike damu yake, ndio Mwenyezi Mungu awe radhi na amsamehe huyo mwenye dhambi?  Huyu ni Mungu mwenye rehema na mapenzi kwa viumbe vyake, au ni Mungu aliye katili kwa waja wake na hata kwa mwanawe?  Kwanza awasingizie wanaadamu wote kuwa wana dhambi kwa jambo wasilolitenda, kisha kuwasamehe kwake ni kwa kumwuua mwanawe mwenyewe! Makosa mawili hayafanyi moja lisibu.
Basi tunaona kuwa nadhariya ya imani ya kuwa dhambi hurithiwa iliyoanzishwa na Mt Paulo kama ilivyo katika barua yake ya mwanzo kwa Wakorintho tulionukulu hapo juu, inapingwa na ushahidi wenye nguvu zaidi kutokana na Biblia, yaani kwa maneno ya Musa yaliyomo katika Kumbukumbu la Torati, na maneno ya Bwana Mungu yaliyomo katika Yeremia na Ezekieli, na maneno ya Yesu kama yaliyomo katika Injili ya Mathayo na Injili ya Yohana.  Lakini wazee wa Kanisa wamekhiari kuukataa ushahidi wazi wa kukata wa Nabii Musa, wa Bwana Mungu, na wa Yesu, uliomo katika Torati na Manabii na Injili, na kufuata badala yake ubishi wa barua za Mt Paulo.
Lakini huyo Mtakatifu Paulo ni nani?


4- MTAKATIFU  PAULO

Mt Paulo alikuwa Myahudi aliyezaliwa katika mji wa Tarsus katika nchi ijuulikanayo hivi sasa kuwa ni Uturuki.  Alipozaliwa nchi hiyo ilikuwa ni sehemu ya mamlaka ya Dola ya Kirumi.  Kwa hivyo ijapokuwa kwa kabila na dini alikuwa ni Myahudi, kwa uraia alikuwa ni Mrumi.  Paulo hakuwa katika wanafunzi aliowateuwa Yesu katika uhai wake.  Kwa hakika hapana dalili kuonyesha kuwa hata hao wawili waliwahi kukutana.  Linalojuulikana ni kuwa ni mtu aliyepita mipaka katika chuki zake kuwachukia Wakristo, na mwenyewe alijitwika jukumu la kuwasaka Wakristo kila kipembe walipojificha ili wapelekwe kuteswa na kuuwawa.  Yeye alishiriki wakati alipokuwa anarujumiwa kwa mawe Mtakatifu Stefano, shahidi wa mwanzo wa Kikristo.
Alipokuwa yuko njiani anakwenda Dameski (Dimishqi) miaka kadhaa wa kadhaa baada ya Yesu kwisha ondoka duniani, yasemekana kuwa Paulo alijiwa na Yesu ambaye alimwambia maneno fulani. Tangu hapo akaingiwa na hamu kubwa ya kutaka kuwaita watu waingie katika dini ya Kikristo.  Juu ya hivyo huo Ukristo wa Mt Paulo aliodai kuwa umefunuliwa kwake na Yesu mwenyewe, ni namna mbali kabisa na Ukristo waliokuwa wamefunzwa wanafunzi wake Yesu, alioweteuwa mwenyewe na akawafunza katika uhai wake. Kwa hivyo pakatokea mzozano  mkubwa baina ya Paulo na wanafunzi wa Yesu wa asili, ambao walikuwa wanashikilia kufuata sharia ya Musa, kama alivyokuwa akiifuata mwenyewe Yesu.

Kwa kuwa alielewa vyema ilimu na ustaarabu wa Kirumi na Kiyunani (Kigiriki), na kuwa alikuwa ni mtu mwenye akili, Paulo aliweza upesi kuwa ni kiongozi katika wale wanafunzi wa Yesu, ijapokuwa yeye hakika hakupata kumwona Yesu ila katika hiyo ndoto iliyomjia alipoanguka njiani kwa kupigwa jua kali. Kwa uhodari wake aliweza kuathiri sana mawazo na fikra za dini ya Kikristo kama inavyojuulikana hii leo.  Jinsi mawazo yake yalivyotawala na kuenea hata baadhi wanamwona kuwa ni yeye ndiye muanzishaji wa Ukristo. Mafunzo ya imani ya Paulo hayakutegemea sana juu ya maneno na vitendo vya Yesu kama yalivyotegemea juu ya falsafa za Kigiriki, itikadi za Kiyahudi, na itikadi za kipagani (kishirikina) zilizokuwa zimeenea katika eneo lile la dunia wakati ule. Kwa hivyo utaona kuna mkorogo na migongano katika imani ya Mungu mmoja kama alivyokuwa akiamini Yesu pamoja na Mayahudi wote, na imani ya miungu kadhaa kama walivyokuwa wakiamini mapagani wa Kirumi, Kigiriki, Kimisri na Kiajemi katika zama zile.  Utaona mgongano baina ya imani ya wanafunzi wake Yesu kuwa Yesu hakuuliwa msalabani, na imani ya Mayahudi kuwa wamemwua kwa kumtundika msalabani na kwa hivyo kafa kifo cha laana, kama isemavyo Taurati kuwa anayekufa kwa kutundikwa huyo ni mlaanifu. Kwa uhodari mkubwa Paulo alikusanya ya huku akachanganya na ya huku akaunda hii ijuulikanayo kuwa ni Thiolojia (ilimu ya Ungu) ya Kikristo. Yeye alikuwa ni mhubiri mwenye hima na hamasa kubwa, na alikuwa tayari, kama anavyojisifu mwenyewe, afanye lo lote ili makusudio yake yatimie, yaani apate wafwasi wengi kama inavyowezekana.

Barua zake alizokuwa akiwapelekea Wakristo mbali mbali zimo katika Biblia na zinahisabika kuwa ni sehemu ya Agano Jipya. Muhimu katika mafunzo yake ni kuwa mtu anapata haki kwa imani si kwa vitendo, na imani ya kwamba kila mwanaadamu kazaliwa na dhambi ya asili ambayo haifutiki ila aamini kuwa Bwana Mungu kamleta mwanawe wa pekee kuja duniani ili ateseke na auliwe msalabani kuwa kama ni kafara ya hiyo dhambi ya tokea Adam. Hayo yanatosha. Kufuata sharia sio muhimu.  Ni yeye Paulo ndiye aliyeondoa na kubatilisha sharia ya tangu Ibrahim ya kuingia tohara, na kuwa nyama wasiochinjwa, na nguruwe ni haramu.  Sharia zote ambazo Yesu na wanafunzi wake wote walikuwa wakizifuata Paulo alifunza kuwa hazina maana. Haya yalikuwa na maana kabla Yesu hajajitoa mhanga msalabani.  Baada ya hapo litakikanalo ni Imani tu ya uwokozi wa watu kwa kifo cha Yesu msalabani.

Jengine lililoleta ugomvi baina yake Paulo na wanafunzi wa asili wa Yesu ni kuwa mafunzo ya Yesu kwenda kufunzwa kabila nyengine zisiokuwa Wana wa Israili, ndio hao waitwao "Mataifa" katika Biblia. Wanafunzi wa Yesu kwa kufuata amri zake mwenyewe alizohimiza mara kadhaa wa kadhaa walipinga shauri ya Paulo kutaka kuwahubiria dini watu wasiokuwa Bani Israili. Paulo kwa ukaidi wake, na werevu wake mwingi aliwashinda nguvu wanafunzi wa Yesu waliopewa jukumu kuitangaza dini katika taifa la Israili tu.
Paulo aliuliwa kwa kukatwa kichwa karibu na Roma baina ya mwaka 61 B.K. na 68 B.K.


5- MWANA WA MUNGU WA PEKEE

Katika Injili nne ziliomo katika Biblia Yesu Kristo ametajwa mara kadhaa wa kadhaa kwa jina la "Mwana wa Mungu". Ifuatayo ni baadhi ya mifano yake:
Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
Marko 15.39
Huyo akida anayetajwa hapo juu ni mpagani wa Kirumi mwenye kuamini wanaadamu wanakuwa miungu, hata mfalme wao wakimwita kuwa ni mungu na mwana wa mungu.
Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli;  kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
Luka 1.35
Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu?  Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.
Luka 22.70
Amemtegemea Mungu;  na amwokoe sasa, kama anamtaka;  kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.
Mathayo 27.43
Na pepo wachafu, kila walipmwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.  Akawakataza sana, wasimdhihirishe.
Marko 3.11-12
Naye alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kupitia njia ile.  Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu?  Je! umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?
Mathayo 8.28-29
Katika Injili za Mathayo, Marko na Luka, Yesu ameitwa mara 22 kwa jina la "Mwana wa Mungu", lakini hata mara moja yeye mwenyewe hakujiita kwa jina hilo.  Katika Mathayo 27.43 tuliyonukulu hapo juu yanatajwa maneno ya wakuu wa makuhani wa Kiyahudi pamoja na waandishi na wazee waliokuwa wakimdhihaki, si maneno yake yeye Yesu. Hao walikuwa wakimzulia kuwa anadai uwana wa Mungu, na anadai kuwa ni Mfalme wa Israeli. Aghlabu waliokuwa wakimwita Mwana wa Mungu walikuwa ama wendawazimu, wenye pepo wachafu, au askari wa Kirumi ambao tokea hapo wao ni washirikina, mapagani. Ama mwenyewe Yesu alikuwa daima akipendelea kujiita mwana wa Adamu kwa Kiebrani, lugha yake, Bin Adam, yaani ni binaadamu, mtu tu. Katika Injili jina hili la Yesu kuitwa mwana wa Adamu limetajwa yapata mara 80.  Makhasimu zake wa Kiyahudi walimzulia kuwa alidai kuwa ni Mfalme wa Mayahudi ili kumchongea kwa watawala wa Kirumi, na kuwa alidai kuwa ni Mwana wa Mungu ili apate kuchusha kwa Mayahudi.

Francis Young, Mwalimu wa mafunzo ya Agano Jipya katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza, akiandika katika kitabu kinachoitwa The Myth of God Incarnate (Uwongo wa Mungu kuwa Mtu) anasema:
"Isipokuwa katika Injili ya Yohana, ambako maneno ya maelezo yamewekwa kwenye mdomo wa Yesu, injili zote nyengine zinaeleza kuwa wenye kutumia maneno kama 'Mtakatifu wa Mungu', au 'Mwana wa Daudi', au 'Mwana wa Mungu' si Yesu bali wengineo. Jina pekee alilokuwa mwenyewe Yesu daima akilitumia ni 'Mwana wa Adamu'...
" Yafaa pia tukumbuke kuwa katika zama za Yesu ilikuwa ni jambo lililoenea kuwabandikiza ungu viumbe vya hadithini na hata wanaadamu wa kweli kweli walio hai.  Mwandishi wa kipagani Laertu alieandika kitabu kiitwacho Lives  of the Philosophers   (Maisha   ya  Mafailasufi),   ameandika kuwa mafailasufi kadhaa wa kadhaa walikuwa wana wa Mungu.  Plato amesimuliwa kuwa wazee wake ni miungu;  hali kadhaalika Paithagoras akiaminiwa kuwa ni mwana mungu aliyekuwa mwanaadamu na mzazi wake ni mungu aitwae Hermes.  Empedokles pia alidaiwa kuwa ni mungu wa milele aliyekuwa akiponyesha wagonjwa, na wafwasi wake wakimuabudu na kumsalia.  Plutarch, mwandishi mwengine wa zama hizo, alikuwa anaamini kuwa bila ya shaka yo yote Alexander (Iskandar) Mkubwa ni mwana wa mungu, na Romulus, huyo anayedhaniwa kuwa ndiye baba wa Warumi, alikuwa ni Mwana wa Mars (Marrikh), mungu wa vita.  Yeye akiaminiwa kuwa alipaa mbinguni katika kiwingu.  Yapo maandishi ya mwaka 48 K.K. (Kabla ya Yesu) yaliyomweleza Juliasi Kaisari, Mtawala maarfu wa Warumi, kuwa ni 'mungu wa kweli, mwana wa Ares na Aphrodites, mwokozi wa wote wa maisha ya wanaadamu.'  Maandishi mengine yanamtaja Agosti Kaisari, aliyerithi utawala wa Juliasi, kuwa 'Mfalme wa wafalme, Kaisari, Mwana wa Mungu, mungu Agosti, mwaangalizi wa ardhi na bahari'.

Majina haya, basi, ya "mungu", "mwana wa mungu" na "Bwana" kwa kuwa yalikuwa yameenea na maarufu katika nchi za bahari ya Kati (Mediterranean) katika zama za Yesu haiwezi kukosa kuathiri mawazo ya watu ambao bado haijawavaa imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja kama ilivyokuwa ikifunza dini ya Kiyahudi.  Majina kama hayo yalikuwa yakitumiliwa ovyo na kila mtu takriban.

Na hizo hadithi za watu kama hao, ikiwa ni watu wa hadithini tu si wa kweli kweli, au watu walioishi kweli kweli duniani, zimefanana mno na hizo ambazo khalafu yake zikaaminiwa na Wakristo kuwa zimemkhusu Yesu Kristo peke yake.

Francis Young katika insha yake inayoitwa Mizizi Miwili au Matatanisho (Two roots or a Tangled Mass) ameandika:
"Tena, hatuwezi kutupilia mbali mawazo kuwa mambo kama hayo yalitokea kwa mintarafu ya Yesu.  Kwa mfano, kuna kufanana kukubwa baina ya hadithi ya Romulus, kama alivyoeleza Livy, na baadhi ya hadithi zinavyoelezwa kuwa ni za Yesu katika Injili:  kuzaliwa na bikra, kutiwa mimba na mungu, maisha ya kiajabu, kutoonekana mabaki yake baada ya kufa, kutokea tena baada ya kufa na kuwatuma wafuasi wake, kumwomba kwa sala.  Itakuwa ni muhali kuleta ushahidi kuwa haya yote yaliigwa tu; lakini watu walioishi wakati mmoja sana huonekana kuwa wanazua hadithi zilizoelekeana."

Tukirejea  kuyanukulu yaliyomo  katika Biblia tunamwona Yesu mahkamani alikataa kukiri mashtaka aliyoshtakiwa kuwa yeye alidai kuwa ni Mwana wa Mungu, kama wendawazimu na mapagani walivyokuwa wakimuenezea:
Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno?  Hawa wanakushuhudia nini?  Lakini, Yesu akanyamaza.  Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu   lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.
Mathayo 26.62-64
Injili tatu za Mathayo, Marko na Luka (ambazo zimefanana) hazimtaji kabisa Yesu kuwa ni Mwana "Pekee" wa Mungu.  Ni Injili ya  Yohana tu ndiyo iliyokazania  kumpa ungu Yesu na kumwita Mwana Pekee wa Mungu. Injili ya Yohana inasema:
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;  nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohana 1.14
 Lugha ya Yohana ni ya namna ya peke yake.  Injili tatu za mwanzo, Mathayo, Marko na Luka zinamweleza Yesu ni binaadamu. Lakini Yohana amepindukia mipaka hapa kwa kumweleza Yesu kuwa ni "Neno" kwa maana aliyoipata kutokana na waandishi wa Kigiriki, sio kutokana na maandishi ya Kiyahudi.  Kauli hii haikutajwa katika Injili hizo tatu za mwanzo wala katika vitabu vyote vya Agano la Kale. Katika karne ya sita kabla ya Yesu kulizuka katika maifalasufi wa Kigiriki nadhariya ya kuwa uumbaji wa ulimwengu haukuzuka ovyo lakini kwa mpango wa kiakili, na ulimwengu wote unaendeshwa kwa kufuata sharia maalumu. Sharia hii au akili hii au mpango huu waliuwita "Logos", maana yake ni "Neno". Tunaona tamko hilo linatumika katika "Bio-logy" "Geo-logy" "Psycho-logy", kwa maana ya "ilimu". Katika zile zile zama za Yesu alikuwako mwanachuoni wa Kiyahudi katika mji wa Iskandaria katika Misri ambaye alikuwa ni mwanachuoni katika ilimu za Kiyahudi na vile vile ni mtaalamu katika falsafa za Kigiriki.  Alijaribu kutaka kueleza mafunzo ya Kiyahudi kwa kutumia hoja za falsafa za Kigiriki. Yeye alitumia hii kauli ya Logos au "Neno" kwa kueleza ile hekima na busara ya Mwenyezi Mungu katika kuumba. Myahudi huyu akiitwa Filo. Yohana aliitumia lugha ya huyo Filo na kuingiza ndani yake mawazo ya kipagani akachanganya falsafa ya Kigiriki kwa kumuambatishia Yesu, na kumfanya yeye Yesu ndiye "Logos" au "Neno" na hilo "Neno" lilikuwapo tangu mwanzo, na hilo "Neno"lilikuwa pamoja na Mungu, bali ndilo khasa likawa ni Mungu.  Haya yote hayakusemwa kabisa na Injili zote zilizotangulia, wala Yesu mwenyewe hakuyadai, wala wanafunzi wake hawakupata kumdaia. Tena Yohana alizidi kusema:
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Yohana 3.16
Tunaona kwa mara ya kwanza Yesu kuitwa Mwana wa Mungu wa pekee. Lakini hata kulitumia neno "Mwana wa Mungu" kuna maana gani khasa?  Tukiipitia Biblia na kufungua sahifa zake tutaona kuwa jina hilo limetumiliwa kwa watu wengi licha Yesu.  Katika Agano la Kale ambalo lote limeandikwa hata kabla ya Yesu hajazaliwa tunakuta mifano kama hii:
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri;  wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
Mwanzo 6.1-2
Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani?
Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni,
Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,
Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?
Ayubu 38.6-7
Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa;  tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.
Hosea 1.10
Ni dhaahiri tunaona ilikuwa ni jambo la kawaida hata kwa waandishi wa Kiyahudi wanaoamini Mwenyezi Mungu mmoja kutumia maneno kama "wana wa Mungu" kwa kukusudia "vipenzi vya Mungu", au "waja wa Mungu", yaani watu wema.
Mwanachuoni wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri, aliyeandika kitabu chake, Maisha ya Yesu (The Life of Jesus), anaamini kuwa neno hilo "Mwana wa Mungu" limegeuka maana kwa kupitiwa na miaka ya makosa ya kufasiri.  Ameandika:
"Kwa hakika, Agano la Kale limetumia neno ebed Yahweh, ambalo maana yake ni 'mtumishi wa Mungu', 'mtumwa wa Mungu', 'khaadimu wa Mungu'.  Matini ya Kigiriki ya Septuagint imeipa tafsiri ambayo yaweza kuwa na maana mbili, (Pais Theou), hali ya kuwa pais, kama neno puer laweza kuwa maana ya 'mvulana mdogo' au 'mtumwa'.  Baada yake ilikuwa ni wepesi kuliondoa neno pais lenye maana ya 'mvulana' likatiwa neno (hyos)ambalo maana yake ni 'Mwana'."

Lugha ya Kiyahudi ya Kiebrani na lugha ya Kiarabu zina asli moja. Mfano wa hayo ni kama mathalan kutumia neno la Kiarabu Abd kama katika "Abdu-Llahi" kwa maana ya "Mtumwa wa Mwenyezi Mungu",na likaja baadae kugeuzwa na kubuniwa neno
"Ghulam" ambalo lina maana ya "Mtumishi" na vile vile "Kijana". Na khatimaye likatumiwa neno "Ibn" ambalo maana yake ni "Mwana" tu.
Hii ndio shida inayompata mtu ye yote anapotaka kujua hakika ya mafunzo ya Kikristo.  Hapana kitabu cho chote duniani chenye asli ya matamshi yake Yesu wala wanafunzi wake. Wao wakisema Kiaramia, lugha ya mazungumzo zama zile huko Palastini,  kama ilivyo lugha ya Kiswahili kwetu. Na lugha yao ya dini ni Kiebrania, kama ilivyo lugha ya Kiarabu kwa Waislamu po pote pale walipo, au Kilatini kwa Wakatoliki. Injili zote ziliopo hapana hata moja iliyoandikwa na kubaki katika lugha ya Kiebrania ya asli, ambayo tungeweza kuirejea tupate ukweli wa kauli za Yesu. Ziliopo zote ni tafsiri za Kigiriki.  Injili za Kiebrania ziliamrishwa zote zichomwe moto.  Hiyo ni amri ya Wazee wa Kanisa, na ye yote aliyeonakana nayo hukumu yake ilikuwa kifo. Inakubaliwa pia kuwa Injili zote zimeandikwa miaka mingi baada ya Yesu kwisha ondoka duniani, na zimeandikwa na watu ambao hawakumwona bali ni kwa kufuata masimulizi waliyoyasikia.  Na ziliopo ni tafsiri, na tafsiri za tafsiri. Yesu hakusema maneno yake kwa Kiswahili, wala Kiingereza, wala Kilatini wala Kigiriki. Kama si kwa Kiebrania basi akifunza kwa lugha iliyofanana nayo, nayo ni Kiaramia.
Hata bila ya ubabaishi wa tafsiri ni jambo la hakika kuwa katika maandishi ya vitabu vya Biblia hili neno "mungu" likitumiwa ovyo. Tunasoma katika Agano la Kale Mwenyezi Mungu anamwambia Musa vipi yatavyokuwa makhusiano yake na nduguye Haruni:
Naye (Haruni) atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe (Musa) utakuwa mfano wa Mungu kwake.
Kutoka 4.16
Angalia tena isemavyo Zaburi:
Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
Zaburi 82.6
Utumiaji ovyo ovyo maneno hayo matakatifu kama "Mungu" au ya kufuru kama "mwana wa Mungu" yaliyotumiwa na waandishi wa Biblia yaonyesha wazi vipi imani na agano la Ibrahimu na Manabii wengine walilofungamana kwalo na Mwenyezi Mungu lilivyopotoshwa. Mayahudi ambao kumshirikisha Mwenyezi Mungu na cho chote ni mwiko walishawishiwa na watawala wao na makafiri waliokuwa wakikaa nao kutumia lugha na maneno ya kikafiri bila ya wenyewe kutambua. Sisi tunaona vipi hii leo tulivyoharibiwa hata Kiswahili chetu na watawala ambao mila na dini zao ni mbali na yetu. Tunaona vipi maneno kama "Halali na Haramu" yalivyopotoshwa hata imekuwa yanatumiwa kuwa ni kilichoruhusiwa au kukatazwa na serikali au chama kinachotawala, wala sio kama ilivyo asli kuwa alichohalalisha na kuharimisha Mwenyezi Mungu. Tunasikia inasemwa kuna pombe ya "halali", yaani inayoruhusiwa na serikali. Tunasikia kuna majumba au mashamba yaliyopokonywa (kughusubiwa) na serikali yanaambiwa ati  "yametaifishwa" kihalali. Na ilhali hapana unyan'ganyi, au wizi wa halali. Yote ni haramu.  Hata hili neno "sharia" limepotoshwa pia. Sharia ni sharia ya Kiislamu tu. Ya Serikali ni "Kanuni" si sharia. Sharia ni ya Mwenyezi Mungu. Makosa anayoyafanya mcheza mpira (faul) sasa yanaitwa: Dhambi. Badala ya Nguzo Tano za Uislamu watoto wetu wanafunzwa "Nguzo tano za ujamaa".
Ni namna hivyo basi waandishi wa Biblia wa Kiyahudi ambao walikuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu mmoja waliikoroga lugha yao kwa kuwa maneno ya kikafiri ya watawala wao wa kipagani wa Kirumi na jirani zao mapagani wa Kigiriki, wa Kimisri na wengineo waliokuwa katika pande zile za mashariki ya Bahari ya Kati (Mediterranean Sea) yaliwaathiri hata wao wakawa wanayatumia kama jambo la dasturi.
Tuliyokwisha kuyanukulu ni maneno ya kutokana na sehemu ya Biblia iitwayo Agano la Kale, yaani ile sehemu iliyoandikwa kueleza mambo ya Manabii waliokuwa kabla ya Yesu. Hebu tuangalie sasa yaliyosemwa na Agano Jipya lilioandikwa baada ya Yesu. Luka anatusimulia katika Injili yake alivyohubiri Yesu:
Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru na waovu.
Luka 6.35
Hapo twaona Yesu anawaambia wafwasi wake kuwa katika malipo ya watendao mema na kuwapenda maadui zao ni kuwa watakuwa "wana wa Aliye juu" yaani Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Mathayo Yesu anasema:
Heri wapatanishi;
 Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Mathayo 5.9
Ni wazi kwa maneno haya kuwa Yesu hakujiona yeye kuwa ni "mwana wa Mungu" kwa maana ya namna ya peke yake kama linavyofundisha Kanisa. Kwa mujibu wa Biblia wote watendao mema, wapatanishi, wanaokopesha bila ya kutaraji kulipwa n.k. ni "wana wa Mungu".  Hiyo ndiyo lugha ya Kibiblia, ndiyo lugha iliyokuwa ikitumiwa wakati huo. Nasi tutakuwa wajinga tukimsikia mtangazaji wa redio au T.V. kwenye uwanja wa futboli akisema: "Kafanya dhambi" kwa kuwa mchezaji kaugusa mpira kwa mkono, nasi  tukaamini kuwa yule mtu kweli kafanya dhambi tunayoijua sisi, yaani kamkosa Mwenyezi Mungu na hivyo anastahiki kutiwa katika jahannam! Haya yanadhihirika wazi katika hadithi hii inayosimuliwa katika Injili ya Yohana. Mayahudi walipotaka kumpiga mawe Yesu aliwauliza kwa vitendo gani vyema alivyowaonyesha ndio wanampiga?
Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe;  bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.  Yesu akawajibu, Je! haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ninyi miungu?
Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);  je! yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru;  kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu?
Yohana 10.33-36
 Kwa mujibu wa kauli hiyo iliyoelezwa na Yohana tunafahamu kuwa Yesu anawaambia Mayahudi kuwa ikiwa katika vitabu vyao watu wema wote wameitwa "wana wa Mungu" pana ajabu gani basi kuwa Mtume wa Mungu aliyetakasika akaitwa vile vile ni "mwana wa  Mungu" kwa maana hiyo ya jumla jamala. Na haya yanawekwa wazi na maneno aliyoyanukulu huyo huyo Yohana kuwa Yesu akimwambia Mariamu Magdalene:
Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.
Yohana 20.17
Hata Paulo naye amesema katika barua yake aliyowapelekea Warumi:
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
Warumi 8.14
Yohana na Paulo ndio wakubwa wa kumfanya Yesu ni Mungu, au mwana wa Mungu, lakini hata wao wametoa ushahidi wa kutosha kuwa huo "uwanamngu" wa Yesu ndio ule ule kama walio nao wote walio wema.
Mwandishi wa Kimarekani maarufu, Upton Sinclair, akiandika katika kitabu chake A Personal Jesus (Yesu Mtu) amesema:
"Na ili asidhani mtu ye yote kuwa kwa kumuita Mungu kuwa ni Baba yake, Yesu akijitangaza kuwa yeye ni Mwana wa Mungu, yafaa ibainishwe wazi ya kuwa vile vile alimwita Mungu 'Baba yenu.' Aliyasema hayo mara kumi na nane katika Agano Jipya:  'Baba yenu wa mbinguni anajua,'  na kadhaalika.  Alikusudia ya kuwa sote sisi ni wana wa Mungu, na yeye (Yesu) ni mmoja wao."


6- JE! MUNGU NA YESU NI MMOJA?

Makanisa ya Kikristo yanafunza ya kuwa Yesu Kristo si kama kuwa ni Mwana wa Mungu tu, bali hakika ni Mungu khasa.  Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni mmoja.  Watatu katika mmoja, na mmoja katika watatu.  Wote ni wa milele, wote ni sawa.  Yesu ni Mungu, na Mungu ni Yesu. Hiyo ni imani ya Kikristo, ambayo inaaminiwa na karibu Wakristo wote.  Hebu tuifunue Biblia tutazame inasema nini katika jambo hili?

Mt Paulo katika barua yake ya kwanza kuwapelekea Wakorintho aliandika:
Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
1 Wakorintho 15.15
Juu ya kuwa Paulo anaambiwa ya kuwa akiamini kuwa Masihi (yaani Kristo) na Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja hapa anasema: "Tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo." Ikiwa Mungu kamfufua Kristo, hawawezi kuwa wote wawili hao ni mtu  mmoja. Mmoja alikuwa ni mtenda, mfufuaji, na wa pili alikuwa ni mtendwa, mfufuliwa. Kama Kristo ni Mungu mwenye uwezo wa kufufua basi maelekeo ni kusema: "Kristo kajifufua", sio kafufuliwa. Mwenye kufufuliwa ni mfu asiyejiweza kitu.

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume inasimuliwa kuwa Mt Stefano alisema aliyoyaona yaliyo mbinguni. Alisema:
Tazama!  naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
      Matendo 7.56
Mwana wa Adamu ndiye Yesu, na kwa jina hilo ndio mwenyewe akipenda kujiita, sio Mwana wa Mungu. Hapo basi huko mbinguni Stefano anasema anamwona Yesu kakaa mkono wa kulia wa Mungu. Mwenye kukaa mkono wa kulia wa fulani hawezi kuwa ndiye yule yule fulani. Hayo ni maelezo ya mbinguni.  Ni wazi basi kwa ushahidi wa Biblia kuwa Yesu hakuwa Mungu mbinguni kama alivyokuwa si Mungu duniani.

Yesu alipokimbilia kwenye Mlima wa Zaituni na huku akisakwa na Mayahudi alijitenga na wanafunzi wake.  Huko faraghani aliomba hivi:
Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.  Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
  Luka 22.42-43
Hapa tunaona mambo matatu muhimu:
  1. Yesu anamwomba Mungu. Yesu anamwabudu Mungu. Wawili hao ni mbali mbali, na vyeo vyao ni mbali mbali. Yesu ni mtumwa mnyonge mwenye kuomba na kuabudu. Na Mungu ni Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wote na mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, hata na Yesu, mwenye kutakiwa msaada pekee, hata na Yesu.
  2. Mapenzi ya Mungu ni mbali na yale ya Yesu. Yesu hataki kuuliwa, ananyenyekea na kuomba kwa Bwana wake: "uniondolee kikombe hiki" cha mauti.  Yesu hana azma hata chembe ya kufa msalabani, kifo cha mhalifu, kifo cha laana kama maadui zake  Mayahudi walivyoazimia kumpatilisha nacho. Lakini anakiri kuwa ni mapenzi ya Mungu sio yake yeye yatendeke. Yeye hana hila wala nguvu za kuzuia kudra ya Mwenyezi Mungu.
  3. Yesu, Mwana wa Adamu, anakata tamaa. Imani inampunguka. Kavunjika moyo. Ikabidi "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu."
Jee, yaelekea kuwa Yesu ndiye Mungu? Yaelekea kuwa yeye na Mungu kuwa ni sawa? Kama upo wasiwasi wo wote wa kujibu hayo, mwenyewe Yesu anajibu kama anavyo hadithiwa na Yohana kuwa kasema:
Baba ni mkuu kuliko mimi.
Yohana 14.28
Na mwishoni naye yupo mslabani:
Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani?  yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?
Mathayo 27.46
Yafaa hapa tujiulize: Yesu akimlilia Mungu gani hapo msalabani ikiwa naye mwenyewe ni Mungu? Au nini alikusudia aliposema: "Mungu wangu naye ni Mungu wenu"?  Maneno hayo kama yanaonyesha cho chote basi yanaonyesha unyenyekevu wa Yesu mbele ya Mungu wake.  La kustaajabisha ni kule kukata tamaa kwake na kuvunjika moyo.  Huwaje mtu wa imani, licha ya nabii na mwana pekee wa Mungu, akate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.  Ama kuwa Mungu akate tamaa na Mungu, na kumyayatikia: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha", ni jambo ambalo halimkiniki kuwa.
Kwa uthibitisho ulio wazi Biblia inatwambia kuwa Yesu si Mungu, wala Mungu si Yesu.


7- UWEZO NI WA NANI?

Katika hoja zinazotolewa na baadhi ya watu kutaka kuthibitisha ungu wa Yesu ni miujiza inayosimuliwa kuwa aliitenda. Mifano ya miujiza hiyo ni kugeuza maji yakawa mvinyo, kuponyesha wakoma na waliopooza, kuwachomoa waliopandwa na pepo, kufufua waliokwisha kufa, na kutembea kwa miguu juu ya maji.   Lakini hizo hizo Injili zinazosimulia miujiza hiyo zinatwambia vile vile ya kwamba Yesu mwenyewe alisema kuwa akifanya yote hayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu aliyemtuma. Wala si kama Yesu alikiri kuwa miujiza tu ni ya Mwenyezi Mungu, bali lo lote alilosema au alilolitenda alisema kuwa ni kwa amri, na upendo wa Mwenyezi Mungu. Yeye hakuweza kuvunja udole bila ya uwezo wa Mola wake. Katika Injili ya Yohana Yesu anasimuliwa kusema:
Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu;  bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele;  basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohana 12.49-50
Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Yohana 5.30
 Fakhari kubwa ya Yesu ilikuwa kwamba kila alisemalo na alitendalo ni kufuata mapenzi ya Mungu na kutii maamrisho yake.

Katika hadithi ya muujiza wa kufufuliwa Lazaro tunasoma kama ilivyo katika Injili ya Yohana:
Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi.  Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. Yesu akasema, Liondoeni jiwe.  Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana ananuka sasa;  maana amekuwa maiti siku nne.  Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?  Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia.  Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote;  lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
Yohana 11.38-42
Kutokana na kisa hichi tunajifunza nini?  Mambo matatu hapa yanatudhihirikia wazi:
  1. Yesu anamwambia Martha, dada wa maiti, kuwa "ataona utukufu wa Mungu" si utukufu wa Yesu, kwani muujiza ni wa Mwenyezi Mungu, si wa Yesu, Mwana wa Adamu. Mfufuaji ni Mwenyezi Mungu, mwenye uwezo wa kila kitu. Yesu "hawezi kufanya neno mwenyewe".
  2. Yesu anamwomba Mungu na anamshukuru Mungu kwa kumwitikia na kuyasikia maombi yake.
  3. Yeye Yesu anajua kuwa Mungu siku zote anamwitikia maombi yake, lakini alifanya yale hadharani ili athibitishe kwa wale waliohudhuria kuwa kweli yeye Yesu ametumwa na Mungu, yaani yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema mwenyewe:"ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma."  Yesu pia anathibitisha kuwa ayatendayo ni mapenzi na amri ya Mungu.
Hayo ndiyo, lakini yeye mwenyewe Yesu kafufuka kutoka wafu. Huo si muujiza wa kuonyesha kuwa yeye ni Mungu? Hebu tuitazame Biblia inasema nini juu ya tukio hili. Kila tusomapo kitabu hichi kitakatifu tunaona kuwa ni Mungu ndiye aliyemfufua Yesu.
Hatuoni kuwa Yesu kajifufua mwenyewe. Vile vile tunasoma humo humo kuwa si yeye peke yake aliyesimuliwa na kuaminiwa kuwa kafufuliwa kutoka wafu.  Twasoma katika 2 Wafalme:4.32-37 vipi Nabii Elisha (Al Yasaa) alivyomfufua mtoto aliyekwisha kufa. Kisa kingine kama hicho kinasimuliwa katika 1 Wafalme 17.22.  Biblia pia inawataja watu wengine wasiokuwa Yesu waliopaa wakenda mbinguni. Katika 2 Wafalme tunasoma:
Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili (Elisha na Eliya, yaani Al Yasaa na Ilyas); naye Eliya (Ilyas) akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.
2 Wafalme 2.11
"Kisulisuli" ni upepo wa chamchera au kimbunga.  Hadithi kama hizo za watu watukufu kupaa mbinguni na kufufuka zilikuwa zimeenea sana katika zama za Yesu.  Josefas akiandika katika kitabu Antiquities (Ya Kale) anasimulia khabari ya Musa: "Kwa ghafla kiwingu kilisimama mbele yake, naye akapotea katika bonde fulani, ijapokuwa ameandika katika vitabu vitakatifu ya kuwa alikufa. Hayo yalifanywa  kwa kuogopa wasije kusema kuwa kwa sababu ya uchamngu wake uliopita kiasi, alikwenda kwa Mwenyezi Mungu." Josefas pia ametaja kuwa baadhi ya watu walifikiri kuwa "Musa ameingizwa katika ungu."
Na J. Jeremias katika Moyses amesema:

"Watatu wamepaa mbinguni nao wahai: Enoko, Musa na Eliya".
Almuradi tunaona kwa uthibitisho wa maandiko matakatifu ya Kikristo kwamba si Yesu peke yake aliyeitwa "Mwana wa Mungu, au Mungu", wala si yeye peke yake aliyefufua wafu, wala si yeye peke yake aliyefufuka na kupaa mbinguni.


8- KUZALIWA BILA YA BABA

Labda katika miujiza yote ya kumthibitishia Yesu ungu ni kule kuzaliwa kwake na bikra bila ya baba. Wengi wanaona hayo ndiyo yanayoonyesha kwa nguvu zaidi kuwa yeye ni Mungu au Mwana wa Mungu. Mtaalamu mkubwa wa Kikristo, Maurice Wiles, Professor of Divinity and Canon of Christ Church Oxford, na Mwenyekiti wa Tume ya Imani ya Kanisa la Kiingereza, ameeleza vipi ilivyokuwa ni muhimu kabisa kuamini kuzaliwa na bikra kwa mwenye kutaka kuamini kwamba Yesu ni Mungu.  Professor Wiles akiandika katika kitabu The Myth of God Incarnate (Uwongo wa Mungu kuwa Mtu) amesema:
"Mwanzoni mwa karne hii (ya ishirini) zilipokuwa shaka shaka zinatamkwa kuwa ati ni kweli hakika Yesu alichukuliwa mimba na bikra, maneno hayo ya kuonyesha shaka yalionekana mara nyingi kuwa  ni mashambulio khasa juu ya imani ya kuwa Mungu kawa mtu. Ilionekana kwamba imani ya kuzaliwa na bikra na kwamba Mungu amekuwa mtu ni kama pacha wasiobandukana, ama zitasimama pamoja au zianguke pamoja."

Biblia yasemaje juu ya jambo hili?  Kwa hakika si kitu cha kawaida mtu kuzaliwa na mwanamke bikra asiyeingiliwa. Ni kweli huo ni muujiza. Lakini ndio ndivyo kuamini kuwa chenye kuzaliwa kwa muujiza ni Mungu?  Au hata ndio ndivyo kuona tukio kama hilo ni dalili mojawapo ya kuzidisha ushahidi ya kuwa huyo mtoto ni Mungu au Mwana wa Mungu, kwa maana wanavyotaka wakuu wa makanisa wafwasi wao waamini?

Biblia inayotwambia kuwa Yesu kazaliwa bila ya mama yake kuingiliwa na mwanaadamu (Injili ya Mathayo 1.18) vile vile inatuambia ya kuwa Adamu hakuwa na baba wala mama. (Mwanzo 1.26- 27). Kama wa Yesu ni muujiza wa Adam ni muujiza mardufu. Hali kadhaalika Paulo amewaandikia Waebrania:
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;  ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;  hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu);  huyo adumu kuhani milele.
Waebrania 7.1-3
Tunaona basi Biblia inatuhakikishia kuwa Yesu hakuwa pekee mwenye kuzaliwa bila ya baba. Wapo waliomtangulia katika muujiza huu. Kama huo ndio ungu, basi wangelikuwa Adam na Melkizedeki wa mbele, ambaye anasimuliwa na Biblia kuwa alikuwa
"hana baba, hana mama, hana mwanzo wala mwisho".

Hoja nyingi zimetolewa kukanya fikra ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aligeuka binaadamu akaishi duniani kwa sura ya Yesu wa Nazareti. Hoja hizo ziko za misahafuni mpaka za kisayansi. Katika Qur'ani ameshabihishwa Yesu na Adam. Hali kadhaalika muujiza ulitokea kabla kidogo tu ya kuzaliwa Yesu, alipochukua mimba Elizabeti, mke wa Zakaria na ilhali huyo mama ni tasa tangu ujana wake na hapo kesha zeeka na kapindukia miaka ya kuzaa. Mumewe, naye, Zakaria alikuwa ni mkongwe.  Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani, Sura ya Al Imran:
Akasema Zakaria: Mola wangu! Vipi nitapata mtoto, na hali ukongwe umesha nifika, na mke wangu ni tasa?  Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
(Qur'ani) Al Imran 3.40
Ilipofika zamu ya Maryam kuchukua mimba Qur'ani inasema:
(Maryam) akasema:  Mola Mlezi wangu! Vipi nitampata mtoto na hali hajanigusa mwanaadamu  ye yote? (Mwenyezi Mungu) akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho; anapohukumu jambo, huliambia: Kuwa! Basi likawa.
(Qur'ani) Al Imran 3.47
Hizi ni hoja za misahafu, ni hoja za watu wenye imani. Wapo wengineo ambao wamepuuzilia mbali hadithi yote hiyo ya kuwa Maryam kachukua mimba bila ya kuingiliwa na mtu. Hao ni kama Mayahudi ambao wanamtukana Yesu na mama yake kwa kusema kuwa hiyo ni mimba ya haramu.  Miongoni ya wataalamu wa Kizungu wenye asli ya Ukristo wapo wanaoamini hayo. Wanasema kuwa imani ya kuzaliwa na mama bikra ilikuwako tangu zamani katika dini za kipagani (kishirikina) kabla ya kuja Yesu. Bikra Rea Silvia alimzaa Romulus wa Roma. Horus wa Misri alizaliwa na Isis, malkia bikra wa mbinguni. Hoja inayotolewa kama ilivyokuwa hizi na nyenginezo ni hadithi za kubuni tu zilioenea pande za Bahari ya Kati, basi ndio hivyo hivyo hadithi ya kuwa Maryam alikuwa bikra alipochukua mimba na kumzaa Yesu ni hadithi ya kubuni kuiga zile zilizotangulia.
Mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri anawashutumu wakuu wa Kanisa kwa kutafuta kila kipengee katika Biblia kutoa ushahidi kuwa kuzaliwa kwa Yesu na bikra kuliaguliwa mbele. Kipande kinachonukuliwa mno ni kile kiliomo katika Isaya ambacho kinasema:
Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara.  Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Isaya 7.14
Mtaalamu huyu anasema maneno haya hayakukhusu kuzaliwa kwa Yesu hata chembe. Kwanza neno la asli halikutaja "bikira" lakini ni "mwanamke kijana". Tafsiri nyingine kama Revised Standard Version zimefuata hivyo ilivyo asli. Neno la Kiebrania liliotumiwa ni almah ambalo maana yake ni mwanamke kijana au msichana. Neno bikra kwa Kiebrania ni bethulah, kama ilivyo katika Kiarabu batuul. Na haya mambo ambayo yametokea zaidi ya miaka 700 kabla ya Yesu yalikhusiana na mke wake Isaya ambaye alikuwa umri wake ni miaka 20 wakati ule na kweli akaja kumzaa mtoto mwanamume. Ama hilo neno Imanueli, maana yake ni Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, na wala sio maana yake kuwa huyo mtoto kuwa ndiye Mungu. Lugha ya Kiebrania imekaribiana na Kiarabu, na kwa Kiarabu ni Ma'anallah, nalo ni jina la kawaida, na kama kwamba kumwombea kheri huyo mwenye kuitwa. Mtaalamu Isaac Asimov ameeleza wazi juu ya utabiri huu wa Isaya katika kitabu chake, Asimov's Guide to the Bible.

Mtaalamu mwengine mwenye kupima mambo kiakili aitwaye G. Vermes amesema katika kitabu chake Jesus the Jew (Yesu Myahudi) akidai kuwa hili neno "bikira" hata lilivyotumiwa kwa Mariamu yawezekana sana kuwa maana yake ni kuwa mdogo mno kwa uzazi, kama walivyokuwa Sara, Hanna na Elizabeti kuwa ni wakongwe mno, au tasa.

Mwishoe kuna maoni ya mwana-sayansi na daktari juu ya hili suala la kushika mimba mwanamke hali naye ni bikra. Dr. T.H. Van de Velde M.D. akiandika katika kitabu chake cha kitaalamu, Ideal Marriage (Ndoa Bora) anasema:
"Mara nyingi imewahi kutokea, ijapokuwa ni nadra, kushika mimba kwa kupenya mbegu ya uzazi katika utupu wa mwanamke bila ya kuingiza kabisa dhakari, au utupu wa mwanamume. Mifano kama hiyo ni muhimu kabisa kimaisha. Ni dhaahiri kuwa inathibitisha vitu viwili. Kwanza, kuwa katika hali maalumu yawezekana mimba kutiwa ijapokuwa kizinda hakikupasuliwa. Na pili ya kwamba mbegu ya uzazi yaweza kufika ndani ya utupu wa mwanamke kwa njia isiyokuwa moja kwa moja, kwa mfano kwa mguso wa kidole..."

Hapana shaka pana utaalamu mkubwa katika mawazo na fikra hizi, za kidaktari, za kisayansi au za kiakili; lakini ni Qur'ani ndiyo inauweleza ukweli kwa maneno mepesi kabisa hata watoto wachanga wakaweza kuelewa na ikawa ya kuwatukuza Yesu na mama yake:
Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa mchanga kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa. Hii ni kweli inayotoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka.
(Qur'ani) Al Imran 3.59-60
 

9- YESU - NABII ALIYETOKA NAZARETI MTUMISHI WA MUNGU

Masih hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu.
 (Qur'ani) An Nisaa 4.172
Biblia inahakikisha ukweli huu wa Qur'ani. Mara nyingi tunaona Yesu anatafakhari kujitangaza kuwa yeye ametumwa na Mungu, na mara nyingi anaitwa "mtumishi wa Mungu". Katika Injili ya Yohana mathalan tunasoma:
Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.  Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.
   Yohana 17.3-4
Kwa unyenyekevu wa safi ya niya Yesu anamkhatibu Mola wake, "Mungu wa pekee wa kweli", siye mungu wa uwongo miongoni wa miungu ya uwongo uwongo iliyokuwa ikiabudiwa na makafiri. Ajuulikane Mwenyezi Mungu na kadhaalika ajuulikane yeye Yesu Kristo, Mtume na mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume kiliomo katika Agano Jipya la Biblia tunasoma:
Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.
Matendo 3.26
Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.
Matendo 3.13
Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya;  ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.
Matendo 4.29-30
Wagonjwa wanaponyeshwa, ishara zinaonyeshwa, na maajabu yanatendeka.  Nani afanyae yote haya?  Ni kudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu.  Jina la Yesu huenda likatumiwa, lakini ni kama chombo tu, wasila, mwombezi, kwani kama atavyokuwa yeye ni "mtumishi mtakatifu wa Mungu." Katika Matendo 3.26 na 3.13 hapo juu Paulo aliwaandikia Mayahudi ambao walimkataa mtumishi wa Mungu, Yesu Kristo, alipowajia na utumishi kutoka kwa Mungu wa babu zao Mayahudi, Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na Yakobo.
Mwenyezi Mungu ni yule yule mmoja, Mitume ni mbali mbali, lakini utumishi wao ni mmoja. Mayahudi wakawakubali wote waliotangulia wakamkataa Yesu. Mwenyewe Yesu anawasimanga Mayahudi kama inavyotueleza Injili ya Yohana:
Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua;  wala sikuja kwa nafsi yangu;  ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi.  Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.
Yohana 7.28-29
Katika Injili ya Marko Yesu anasimuliwa alimchukua mtoto akasema:
Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi:  na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.
Marko 9.37
Kama hayo aliambiwa Mtume Muhammad s.a.w. na Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:
Sema:  Ikiwa ninyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakusameheni madhambi yenu, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
 (Qur'ani) Al Imran 3.31
Yesu amesema:
Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.
Yohana 4.34
Haya khasa ndio maana ya neno Uislamu. Uislamu ni kujisalimisha nafsi yako kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kutenda apendavyo Mola wako Mlezi.  Na hicho ndicho chakula chake Yesu, kama asemavyo, yaani kama anavyohitaji kula kila siku ili aishi, kama wanavyohitaji wanaadamu wote, basi hali kadhaalika kuwa daima anajisalimu mbele ya matakwa ya Mwenyezi Mungu aliyemtuma duniani kuwa ni Mtume. Tena Yesu amesema:
 Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu.  Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe;  bali anayetafuta utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu.
Yohana 7.16-18
Tunaona basi kwa ushahidi wake mwenyewe Yesu kuwa fakhari yake ni kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu wake aliyemuumba na akamtuma kwa Wana wa Israili waliopotea kama kondoo.  Kwa uthibitisho wake mwenyewe yeye ni mtumishi wa haki aliyepewa Unabii na kufanywa Mtume.  Hataki utukufu wake yeye, bali utukufu wa Mungu wake aliyemtuma na kumpeleka awaongoe watu wafwate njia iliyo nyooka. Katika Injili ya Mathayo anazidi kufafanua nini wadhifa wake na nini cheo chake mbele ya Mwenyezi Mungu  na mbele ya wanaadamu wenziwe. Alipowateua wanafunzi wake kumi na mbili kuwapeleka kuwahubiria Mayahudi alisema:
Awapokeaye ninyi, anipokea mimi;  naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.  Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii;  naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.
Mathayo 10.40-41
Yeye mwenyewe Yesu amesema kuwa yeye ni Mtume, yeye ni Mtumishi, yeye ni Nabii.  Je, nini mawazo ya wale wafwasi wake waliomuamini na wakamwona na wakaishi naye? Injili zinatwambia:
Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.
Yohana 6.14
Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Mathayo 21.46
Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?  Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.
Mathayo 21.10-11
Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.  Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.  Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.  Macho yao yakafumbwa wasimtambue.  Akawaambia, ni Maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea?  Wakasimama wamekunja nyuso zao.  Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je!  wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?  Akawauliza, Mambo gani?  Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda mbele za Mungu na watu wote.
Luka 24.13-19
Injili kwa umoja wao zinathibitisha kuwa watu wake Yesu waliokuwa naye na kumuamini na wakaona miujiza yake tangu kuzaliwa kwake mpaka mwisho wake walimjua kuwa ni Nabii wa haki, naye ni mtu, mwanaadamu.
"Hakika huyu ni nabii", anasema Yohana.
"waliwona kuwa nabii", anasema Mathayo.
"Huyu ni yule nabii, Yesu", anasema tena Mathayo.
"Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii", anasema Luka.
Jinsi ya hadhari zake asisingiziwe kuwa anazo au anadai sifa za ungu, Yesu alikataa hata kuitwa "Mwalimu mwema". Sikiliza masimulizi ya Injili ya Marko:
Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akmwuuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?  Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema?  hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.
Marko 10.17-18
Tafsiri kubwa kabisa ya Biblia iitwayo The Interpreter's Bible inasema kuwa kauli hiyo ya Yesu, yaani: "Kwa nini kuniiita mwema?  hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu", imewatatiza wataalamu wa thiolojia (ilimu ya Ungu) ya Kikristo wa baadaye. Wameona taabu kuambatisha maneno haya yalio wazi na imani yao kuwa Yesu ni mungu, na hali hapo dhaahiri yake ni kuwa anakataa ungu. Kwa hivyo basi kujitoa kimasomaso ikaandikwa katika Injili ya Mathayo (ambayo iliandikwa baada ya Marko) kwa njia nyengine. Ilivyoandikwa katika Mathayo ni hivi:
Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia, Kwani kuniuliza habari ya wema?  Aliye mwema ni mmoja.
Mathayo 19.16-17
Kila imani ilipozidi kugeuka maandiko mapya yaliandikwa na kunasibishiwa   Yesu. Kitabu hicho The Interpreter's Bible kinaikataa tafsiri ya kusema kuwa makusudio ya Yesu yalikuwa ni kusema:  Kama unanita mwema, basi unakusudia kuwa mimi ni Mungu. Hayo siyo. Aliyokusudia Yesu kusema ni kuwa :Sifai kupewa sifa za Mungu.
Mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri, ameandika katika kitabu chake The Life of Jesus (Maisha ya Yesu):
"Yesu kwa mara moja alimpa somo zuri kabisa la unyenyekevu, ambalo juu ya mengineyo, ni ushahidi ulio wazi ya kwamba hakupata kabisa kujiona mwenyewe ni sawa na Mungu:  Kwa nini kuniita mwema?  Hakuna mwema ila mmoja, ndiye Mungu."

Mukhtasari wa yote tuliyokwisha yazungumza, ni kuwa tumepata uthibitisho wa kutosha kutokana na Biblia kuwa Yesu wa Nazareti ni mwanaadamu, Nabii wa Mungu, na Mtume wake.
Jee, Mtume huyo katumwa kwa nani?


10- MTUME KWA WAISRAILI

Tumekwisha ona kutokana na maneno ya Injili na maandiko mengine ya Agano Jipya tuliyoyanukulu kwamba Yesu ametumwa na Mwenyezi Mungu. Ametumwa awendee nani?  Hebu tuiache Biblia itueleze:
Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.  Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake;  kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akisema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.  Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana, unisaidie.  akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.  Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani za bwana zao.  Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa;  na iwe kwako kama utakavyo.  Akapona binti yake tangu saa ile.
Mathayo 15.21-28
Kwa maneno yasiotatanisha Yesu Kristo anasema kuwa yeye hakutumwa ila kwa "kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Hakuwajia Waarabu, wala Wazungu, wala Wahindi, wala Waafrika, wala Machina. Kama hayo hayakutosha kuonyesha kuwa yeye hakuwajia wasio Mayahudi anazidi kufahamisha kwa mfano wa kumkata mtu kiu: Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." Ikiwa ipo shaka yo yote katika akili ya mtu kuwa maana ya maneno hayo ni kuwa Yesu anasema kuwa hakutumwa kwa kabila nyengine zo zote ila Waisiraili tu na atazame mwenye shaka tafsiri kubwa kabisa ya Wakristo inayoeleza maana wazi maneno ya Biblia, The Interpreter's Bible, sahifa 441 jalada VII ambamo imeandikwa hivi:  "Yaonekana wazi kuwa Yesu hakika aliamini kuwa ujumbe wake kwanza na khasa ni kwa watu wake mwenyewe." Ndio maana alisema:
Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.
Mathayo 7.6
Mbwa na nguruwe ni watu wa mataifa yasiyokuwa wana wa Israili. Ukristo haufai kufundishwa watu wo wote isipokuwa Mayahudi. Hayo ndiyo mawazo ya Yesu, au ya hao walioandika Injili na wakatia maneno hayo kinywani mwa Yesu.  Kama asemavyo Isaac Asimov katika kitabu chake Guide to the Bible (Uwongozi kwa Biblia):
"Suala liliopo ni nani hao mbwa na nguruwe wnaokusudiwa katika mstari huu? Yaweza kuwa maana ya mstari huu ni kuwa haifai kufunza ukweli wa dini kwa wale wasiotubu katika kejeli zao, au wale waliozama katika madhambi, lakini hayo hayaelekei kabisa. Basi mtu amfundishe nani? Wale waliokwisha amini? Yesu mwenyewe anakanya hayo, kwani aliposhutumiwa kuwa anachanganyika na wenye dhambi ananukuliwa kusema:
Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
Mathayo 9.12
"Upande mwengine, huku kutaja mbwa na nguruwe huweza kuwa ni maneno aliyoyachagua Mathayo kulipa nguvu wazo lake kuwa isifanywe juhudi kubwa kueneza mafunzo ya Yesu miongoni mwa Mataifa mengine. Labda ni nadhari ya Mathayo kuwa ipo khatari kubwa ya hayo Mataifa kuudhika na juhudi za kutaka kuwatanasarisha na kwa hivyo wakawatesa Wakristo; itakuwa ndio 'watageuka na kuwararua'.Na hayo kwa hakika waliwahi kuyafanya. Yaweza kuwa aliona kuwa yale Mataifa yaliyoukubali Ukristo bila ya kuijua Sharia ya Musa yangeweza kuyavuruga mafunzo ya Yesu: 'na kuyakanyaga chini ya miguu yao.'"

Na juu ya kauli ya Yesu : "Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa," Asimov anasema:
"Hapa Mathayo kwa uwazi anatuletea Yesu ambaye kazi yake ni ndani ya mipaka ya uwananchi wa Kiyahudi tu."

Tukiendelea na isemavyo Biblia juu ya ujumbe wa Yesu tunapata ushahidi zaidi kutokana na Injili ya Mathayo:
Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.  Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
Mathayo 10.5-6
 Hao Thenashara ni wanafunzi wake kumi na mbili aliowateua mwenyewe Yesu kutangaza mafunzo yake.  Hapo anawapa amri zilizo wazi kuwa wasiwaendee watu wa Mataifa, yaani wasiokuwa Waisraili. Hao wanafunzi kumi na mbili ndio wanaoitwa katika Biblia "mitume" kwa kuwa walitumwa na Yesu. Na wao kama yeye mwenyewe hawakutumwa ila kwa "kondoo waliopotea wa Israel" kwani "si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."

Kwa nini Yesu alisema maneno kama haya ya kukataa na kukataza kuwafunza dini ila Waisraili tu?  Kwa nini alitumia mifano mibaya kama hivyo "mbwa" na "nguruwe" kwa kuwakusudia hao watu wengine wasio Mayahudi, yaani ndio mimi na wewe mwenzangu?  Wataalamu wa Kikristo na wasio Wakristo wamestaajabishwa na maneno hayo.  Ni maneno machache katika aliyoyasema Yesu ambayo yamewatatiza wasomaji Wakristo kuliko maneno haya.  Wapo wanaoona kuwa Yesu alitumia matusi yale kuwaita wote wasio Mayahudi kufuata mwenendo wa Kiyahudi, yaani ndio hivyo Mayahudi wawaonavyo binaadamu wote wasio kuwa wao. Na wapo wasemao kuwa Yesu akipenda kufunza kwa mifano, na hivyo anafananisha kama kwamba yeye anaamini hiyo imani mbovu ya Kiyahudi ya kudharau watu wasiokuwa kabila yao. Na wapo wengine kama Asimov ambao wanaona maneno yale ni ya Mathayo, na yeye Mathayo (au ye yote yule aliyeandika Injili hiyo) kamuambatisha nayo Yesu maneno hayo, kwa kuwa yeye mwandishi alikuwa Mkristo wa kabila la Kiyahudi na anacho kiburi cha Kiyahudi.

Ama kusema kuwa hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa Israeli inaonekana kama kilivyosema kitabu cha The Interpreter's Bible kuwa Yesu hakika kwanza aliamini kuwa alitumwa kwa Waisraili tu.  Ni jambo la kustaajabisha kuwa Mungu au Mwana wa Mungu aje duniani atumwe na kwanza asiujue utumwa wake ila aamini tu kuwa katumwa kwa watu wake wa Kiyahudi basi.  Na kama yeye ni Mungu au Mwana wa Mungu, katumwa na nani?  Kama katumwa na Mungu, basi yeye si Mungu.  Si hilo tu, bali hata akiwa ni Nabii na Mtume wa Mungu tunamtaraji aujue tangu mwanzo huo ujumbe wake aliokuja nao, asiwe kutapatapa, kupapasa,  na kuhangaika katika jambo la msingi.

Hapana haja ya kuyatafutia tafsiri hii na maana hii, hayo maneno yaliyo wazi ya Yesu Kristo.  Yesu hakika hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.  Yesu hakika kawakataza "mitume" wake wasende kuwahubiria mataifa mengine.  Yesu ni kweli kaonya kuwa kuwafundisha mafunzo yake hayo mataifa mengine ni sawa sawa na kuwapa mbwa kilicho kitakatifu, na kuwatupia lulu nguruwe. Kwa nini ikawa hivi? Ikiwa Yesu kweli katumwa na Mungu, kwa nini ujumbe wake uwekewe mipaka kwa jamaa zake tu wa Kiisraili, na yeye asikiuke mipaka ile?  Naam, zipo sababu zenye nguvu kwa hayo.

Kwa hakika hayo hayakuwa mageni, wala Yesu hakuwa Mtume wa mwanzo kutumwa hivyo na Mwenyezi Mungu.  Mitume wote waliokwisha kuja kabla yake walikuwa ni Mitume wa vikundi vyao tu, na zama zao tu, na walikuja na mafunzo yao maalumu machache. Musa alikuwa hivyo, na Yesu hali kadhaalika.  Hali yake hali ya wenziwe, ila yeye alikuwa ndiye Mtume wa mwisho katika Mitume waliotumwa kwa kabila maalumu.  Kwa nini Mwenyezi Mungu akafanya hivyo?

Kwa nini Yesu alikatazwa, mathalan, asiwahubirie yeye wala wafwasi wake, Waafrika, au Wazungu, au Wahindi, au Machina, au Waarabu?  Amekatazwa kwa sababu kabila zote hizo zilikuwa hata hazijachukua khatua ya mwanzo ya kuamini Mungu Mmoja.  Kabila hizo na mataifa hayo yalikuwa makafiri ama wa kuabudu masanamu, au kuabudu mapango au miti au viumbe vyengine au kuabudu wanaadamu wenzao.  Na ujumbe wake Yesu ni kutengeneza mwenendo, tabia ya watu ambao tangu hapo wanayo imani ya Mungu mmoja. Yeye hakuwa na uwezo wala muda wa kujenga tangu chini.  Yeye kazaliwa katika umma wenye kuamini Mungu Mmoja, umma wenye sharia ya Mwenyezi Mungu.  Kazi yake kwa muda mchache alioishi na kuhubiri ni kiasi ya kuwapiga msasa tu Mayahudi ambao walikwisha tahiriwa, wanajua cha halali na haramu, na muhimu kabisa wanamjua Mwenyezi Mungu Mmoja, asiyezaa wala kuzaliwa.  Ila yao Mayahudi ni kutokuwa na huruma, na kuifanya dini sharia tu isiyo na roho na imani. Mayahudi waliishika sharia ya Musa kwa dhaahiri yake, lakini waliutupilia mbali uchamngu wa Ibrahimu, wakashika ya kuonekana na watu, na wakatupa ya ndani anayoyaona Mwenyezi Mungu na dhamiri zao.  Walipoacha "mitume" wa Yesu amri hiyo ya Mungu ya kutowendea makafiri wasiomjua Mungu wala msingi wa sharia, ndipo mafunzo ya Yesu yalipochafuka.   Kwani hao makafiri walipoingia katika Ukristo walijigeuza jina tu, lakini waliingiza karibu yao yote ya kikafiri katika dini ya Yesu, ikaitwa Ukristo, na hali sio Ukristo kabisa aliyoufundisha Yesu.  Mahekalu yao ya kipagani yakageuzwa makanisa, na mizimu na mapango yao yakawa ndio monastari za Kikristo. Lau kuwa Wana wa Israili wangeli mwitikia Yesu, basi Ukristo usingelichafuka kama ulivyo chafuka.

Upton Sinclair akiandika juu ya wakati ilipoingia Dola ya Kirumi katika Ukristo na ikaufanya ndio dini rasmi ya taifa, amesema kwa masikitiko: "Ulikuwa ni ushindi kwa Kanisa, na kwa mwenyewe mwenye kuanzisha (yaani Yesu) ni kushindwa kwa muda. Maana yake ni kuwa maadui zake wamelichukua jina lake, mafunzo yake, na nguvu zake."
Yesu alionya, lakini Paulo hakusikia:
"Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.  Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.  Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na wakawararua."

Yaliyosemwa yamekuwa.  Kwa kitendo cha Paulo kuwaingiza mapagani wa Kizungu katika dini ya Yesu sharia ya Mwenyezi Mungu ikaambiwa ni laana, ikatolewa ruhusa kula nyamafu, nguruwe na damu, na kila kiuzwacho sokoni bila ya kutia wasiwasi wo wote katika dhamiri. Tohara aliyoamrishwa Ibrahimu na Mwenyezi Mungu na Manabii wote wakaifuata mpaka mwenyewe Yesu na wanafunzi wake, Paulo aliipuuza kuwaridhi makafiri. Imani za kipagani za mungu mwana na utatu zilizoenea katika mila za Mithra, Osiris, Attis n.k. zikaingizwa katika dini ya Kikristo.

Katika ufalme wa mbinguni Yesu ana yakini kuwa hatokuwa nao ila wana wa Israili tu. Injili ya Mathayo inasema:
Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
Mathayo 19.28
Hata katika maombi yake inaonyesha kuwa Yesu alikuwa anajua mipaka yake na uwezo wake. Madai ya kuwa yeye ni mwombezi, mbali kuwa ni mwokozi, wa ulimwengu mzima ni kumsingizia jambo ambalo mwenyewe hakulidhania. Kumpa mtu cheo asichokuwa nacho ni kumtukana, ni kumvika kilemba cha ukoka, kama Mayahudi walivyotaka kumkejeli kwa kumvika taji la miba. Cheo alicho nacho kwa hakika si kidogo.  Kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mitume na Manabii watukufu ni jambo kuu kweli kweli. Kuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu mwenye kupendeza si utukufu mdogo. Na Yesu alitafakhari nao, na alitafakhari kuwa yeye hakutumwa ila kwa  kondoo waliopotea wa Ki-Israili. Na hayo si kwa upungufu wo wote kwa upande wake, ila ni kuutumikia ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kuulinda usiharibiwe na washirikina mpaka ufike wakati wa kuja huyo atayekuwa kazi yake ni kuitangazia risala ya Mungu kwa ulimwengu mzima.
Katika Injili ya Yohana ananukuliwa Yesu kusema:
Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa.
Yohana 17.9
Tukiyachungua vilivyo maneno ya Yesu kama yalivyosimuliwa na Mathayo na Marko ya kuwa yeye alitumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israili, na maamrisho yake yalio wazi kuwapa "mitume" wake wasende kwenye mataifa mengine isipokuwa Mayahudi tu, na kuwa yeye na wanafunzi wake kumi na mbili watakaa katika viti vyao vya utukufu wakizihukumu kabila kumi na mbili za Israili katika ulimwengu mpya wa mbinguni, hatuwezi ila kuhukumu kuwa hao watu anaowaombea Yesu ni hao hao waliokwisha tajwa kabla, yaani wana wa Israili, sio ulimwengu, sio mimi na wewe. Mimi na wewe si Wana wa Israili.  Mimi na wewe ni mataifa mengine.  Mimi na wewe na ulimwengu, usiokuwa wa Kiyahudi, Yesu kesha sema hatuombei, ikiwa tutakubali maneno yaliyoandikwa katika Injili zote.

Ni jambo linalojuulikana katika historia - na hata ukisoma katika Biblia kitabu cha Matendo ya Mitume utaona - ya kuwa Ukristo kwanza haukuhubiriwa kwa mataifa mengine mpaka alipoingia Paulo. Na yeye alipingwa vikali sana kwa kutoa shauri hiyo na wanafunzi wake Yesu waliomwona na wakawa naye siku zote na wakajifunza vilivyo mafunzo yake na makatazo yake ya kwenda kuwahubiria watu ambao bado ni makafiri.
Dr. Marcello Craveri anaandika katika kitabu chake The Life of Jesus:
"Na hapo Paulo akaingia uwanjani.  Kwa heba yake ya kitisho na tamaa yake, hakupoteza wakati ila alijifanya kuwa ni mmoja miongoni mwa 'nguzo' za kikundi kile, kama mwenyewe alivyokuwa kwa kejeli akiwaita Yakobo na Petro. Ukazuka ugomvi na ushindani baina yao na Paulo, na khasa katika shauri ovu la huyu Mkristo mpya kutaka kuivusha dini mipaka ya Uyahudi."

Mtaalamu wa Biblia, Dr. Hugh Schonfield, katika kitabu chake, Those Incredible Christians, (Wale Wakristo wa Ajabu) ameandika juu ya Paulo na ugomvi wake na wafuasi wa kweli wa asli wa Yesu hivi:
"Saulo wa leo, aliyetumia jina la Kirumi la Paulo, alionekana kama ni adui aliyepandwa na shetani wa Daudi mpya.  Hatimaye alipokuwa mfungwa wa Warumi, hapana Mkristo aliyenyanyua hata udole kumsaidia, la Wakristo wa Yerusalemu wala wa Roma. Juhudi zake Paulo zote, hata kule kukusanya michango kuwasaidia watakatifu masikini wa Yuda, hazikupunguza upinzani dhidi yake. Wale walioshika kani miongoni mwa wana-kanisa la halali walimwona Paulo kuwa ni mtu wa khatari na mharibifu aliyeazimia kupata wafuasi wengi katika Mataifa yasiyokuwa Mayahudi ili apate ushindi wa idadi kuweza kuwapinga Wazee walioko Yerusalemu.  Paulo alikuwa ni adui tangu mwanzo, na kwa sababu alishindwa katika ule uadui wake wa wazi, alijipenyeza kwa hila katika kikundi ili aweze kukibomoa kwa ndani. Hili aliweza kulifanya kwa kuitenga Torati takatifu na kumuingiza katika dini ye yote anayetaka kumfuata kwa kutamka tu imani. Ingelifaa asingekubaliwa kabisa mtu huyu; lakini walikuwapo watu ambao hawakujua wala hawakuwa na shaka naye kwa hivyo hawakutambua nini khasa makusudio yake. Na tazama basi ile imani yao imefikisha wapi hali ya mambo!  Unasara wote, juhudi ya Masihi mwenyewe ikaingia katika khatari ya kudharauliwa kabisa katika Israili. Kwa sababu Paulu ni mmoja katika wasemaji wao wakubwa, na yeye alikuwa akitangaza kuwa Torati ni baatili, haifai tena kwa uwokofu, ikawa inaaminiwa na Mayahudi wachamngu kuwa wafuasi wa Yesu ni makafiri wa mwisho."

Busara ya Mwenyezi Mungu kukataza mafunzo ya Yesu yasikiuke mipaka ya Israili ni kuwa isije dini ya haki ikaharibiwa na ushirikina wa makafiri ulioenea pande zote katika zama zile. Ulimwengu ulikuwa bado haujawa tayari kupokea ujumbe wa ulimwengu mzima, na huyo mwenye kuweza kubeba ujumbe ule hajazaliwa, na umma wa kutimiza jambo hilo na kulieneza bado haujapikika ukawa tayari. Yaliyotokea tumeyaona. Ukristo tuuonao na ulioenea ulimwenguni sio Ukristo aliofundisha Yesu. Wa Yesu ulitoweka na mwenyewe na wafuasi wake wa mwanzo wa kabila la Kiyahudi. Paulo kaufuja Ukristo.

Kauli zinazonukuliwa kwa kudai kuwa ni ushahidi kuwa Yesu mwenyewe alitaka mafunzo yake yakafundishwe kwa ulimwengu wote yamo katika Injili ya Mathayo 28.19-20, Injili ya Luka 24.46-49 na Marko 16.15.  Mathayo inasema:
Basi, enendeni, mkwafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi;  na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Mathayo 28.19-20
Luka anatwambia:
(Yesu) akwaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;  na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.  Na tazama, naweletea juu yenu ahadi ya Baba yangu;  lakini kueni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.
Luka 24.46-49
Na Injili ya Marko inasema:
         (Yesu) akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Marko 16.15
Je, imekuwaje?  Yesu ni kigeugeu?  Mbona huku anawakataza wanafunzi wake wasende kuwahubiria ila kabila kumi na mbili za Israili, na huku anawaambia nendeni kuwahubiria Injili ulimwengu mzima.  La, Yesu si mbabaishi, wala si kigeugeu. Hebu natuziangalie vilivyo hizo amri mbili, moja ya kuwa mafunzo yake wasifunzwe ila wana wa Israili tu, na ya pili ni hii ya kuwa watu wote wafunzwe dini.

Vipande vyote vitatu tulivyonukulu mwishoni havitaji mambo ya Yesu alipokuwa na maisha yake ya uhai wa kidunia, lakini vyaeleza mambo yaliyotukia baada ya "kufufuka kutoka wafu" kama inavyosimuliwa na Injili zote tatu.  Yajuulikana kuwa Injili ya mwanzo kuandikwa ni Injili ya Marko.  Hizo nyingine ziliandikwa baadae, na labda ujuzi wao ulitegemea hiyo hiyo Injili ya Marko. Yajuulikana vile vile kuwa maneno yote yaliyohusu kufufuka Yesu kutokana na wafu, pamoja na hayo maamrisho ya kwenda kuihubiri Injili "kwa kila kiumbe", kinyume na maamrisho yake yote ya kuwa asihubiriwe ila Muisraeli tu - maneno hayo yote hayakuwamo katik Marko ya asli, bali yaliongezwa baadae.
Encyclopaedia Brittanica, nakla ya 11, jalada 17, sahifa 730, yasema ya kuwa kipande chote hicho kiliongezwa baadae, yamkini mwanzo mwanzo wa karne ya pili, kuchukua maneno yaliyopotea, au yaliyoonekana kuwa ni mapungufu.

William Neil akiandika katika tafsiri ya Biblia iitwayo Harper's Bible Commentary anasema:
"Kama lipo jambo lolote katika uchunguzi wa Injili ambalo juu yake wataalamu wamekubaliana, ni kuwa kufika hapa (yaani Marko 16.8) Injili ya Marko inakoma.  Sehemu iliyobaki ya sura (yaani 16.9-20) ndio hiyo iitwayo "Kimalizio kirefu" cha Injili.  Kimalizio hicho hakionekani katika nakla za miswada ya zamani, na ambacho ni nyongeza iliyopachikwa katika karne ya pili kutokana na maongezo ya Mathayo, Luka na Matendo...ushahidi wa kale kabisa ulioandikwa juu ya Kufufuka (Yesu) haumo katika Injili bali katika barua ya kwanza ya Paulo kuwapelekea Wakorintho 15.3-8."

Maneno hayo ya Paulo aliyowaandikia Wakorintho na ndio mara ya kwanza kutajwa kufufuka kwa Yesu ni haya:
Kwa maana niliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko;  na ya kuwa alizikwa;  na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maaandiko;  na ya kuwa alimtokea Kefa;  tena na wale Thenashara;  baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala;  badaye akamtokea Yakobo;  tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi,  kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.
1 Wakorintho 15.3-8
Ikiwa kipande chote tangu mstari 9 mpaka mstari 20 katika sura 16 ya Injili ya Marko, kimepachikwa, basi kisa chote cha kufufuka Yesu kimebuniwa.  Mwenye kubuni kisa hichi ni Mtakatifu Paulo.  Hivyo ndivyo tunavyoweza kuagua kutokana na kuisoma Biblia, kwani maandishi ya kwanza hayamo katika Injili bali yamo katika barua ya Paulo kwa Wakorintho.
Amesema Craveri katika Maisha ya Yesu:
"Paulo alijihakikishia mwenyewe kuwa ijapokuwa Yesu ni kweli alikufa, lazima awe amefufuka, akiuwacha mwili wake wa kidunia nyuma ili avae mwili wa 'kiroho'...Paulo alichanganya mawazo yake mwenyewe ya kikafiri kafiri ya Yesu kuwa na maisha mapya kwamba ni malipo yake kwa mema yake, pamoja na imani ya Kiyahudi ya kuwajibika mapatano na Yehova (Mungu) na agano la pili.  Kwa hivyo Paulo akafunza kuwa ndiyo haya khasa yaliyokuwa ni kazi ya Yesu, na hicho ndicho cheo chake machoni mwa Mungu:  kafara ya nafsi yake kwa utakatifu wake na kutokuwa na dhambi kwake ili afutie kwa pamoja makosa ya wote."

Ikiwa basi msingi wa hadithi nzima ya kufufuka Yesu hadi ya ubora wake ni kuwa ni ya shaka shaka - licha ya kuwa ni wazi kuwa ni ya uwongo - hapana njia ya kuamini ya Kuwa Yesu wakati wo wote katika historia aliwahi kuamrisha watu "Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu," kwa sababu haya hakuyasema ila baada ya huko kunakoambiwa ni kufufuka.
Katika Biblia ya Kiswahili iliyo mbele yangu iliyotangazwa na The British and Foreign Bible Society 1950 kifungu cha Marko 16 tangu mstari wa 9 mpaka mwisho yaani mstari wa 20 kimetiwa katika mipinde miwili hivi ( ) kuonyesha kuwa maneno hayo hayakuwamo katika maandiko ya asli. Ilivyokuwa imethibitika kuwa hayo ya Marko si madhubuti, basi yaliyonukuliwa na Mathayo na Luka juu ya mambo hayo ya kufufuka, na kuamrisha kwenda kuhubiria watu wa ulimwengu, na kuutaja Utatu, yote hayo ni baatili.
Kwa mukhtasari tunaona kuwa Biblia inashuhudia kuwa Yesu alikuwa ni Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa Waisraili waliopotea njia.  Hadithi ya kuwa aliamrisha mafunzo yake yakatangazwe kwa watu wote "kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu" imebuniwa na kuongezwa mwishoni mwa Injili tatu za Mathayo, Marko na Luka.  Kadhaalika kuwa Yesu alifufuka kutoka wafu kwa njia ya kimiujiza imeongezwa, na kauli ya Utatu basi ya kuwa mafunzo yakatangazwe "kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu" pia nayo imebuniwa na wala haina asli yo yote ya kweli.


11- KUOKOKA KWA DAMU

Yasemekana kuwa watu wote tangu Adam na Hawa wana dhambi kwa kuwa wazee wao hao walimkosa Mungu kwa kwenda kula mti waliokatazwa.  Kwa hivyo wanamnyima Mungu sehemu ya haki yake. Hapana njia kuepukana na adhabu isipokuwa kwa kumrejeshea Mungu kile alichokhasiriwa na wanaadamu. Hoja iliopo ni kuwa ilivyokuwa wema wote uwezekanao kutendeka tokea hapo ni haki yake Mungu, hapana faida ipatikanayo kwa kutengeneza makosa yakisha tendeka.  Kwa hivyo ni mtu kamili asiye na dhambi kabisa anayekubali kuadhibiwa kwa madhambi ya watu wengine, ndiye awezae kumtuza Mungu kukasirika kwake. Ilivyokuwa ni Mungu tu ndiye asiye na dhambi, basi ni Yeye ndiye yampasa achukue umbo la mwanaadamu ajitolee, ajiachilie ateswe na  auwawe kwa makosa ya viumbe vyake.

Craveri anasema:
"Basi ndio tumezunguka mpaka tumelifikilia wazo la kushutua la mungu anayejiadhibu mwenyewe ili apate kuwasamehe wanaume na wanawake waliomuasi."

Hebu tuangalie hoja zinazotumiwa kutoka katika Biblia za kuleta imani ya kuokoka kwa damu ya Yesu.  Injili ya Marko inasema:
Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa watu wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.  Lakini haitakuwa hivyo kwenu;  bali anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.  Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Marko 10.42-45
Kifungu hicho tulichokinukulu ni moja katika ushahidi unaotolewa katika thiolojia (ilimu ya Ungu) ya Kikristo kuthibitisha imani ya kuwa Yesu kaja duniani auwawe na damu yake iwe ni kafara au fidia kwa dhambi za wanaadamu. Hebu natukiangalie vyema kifungu hichi, chasema nini?
  1. Yesu anasema "hakuja kutumikiwa bali kutumika", licha kuabudiwa.
  2. Maneno yasemayo: "kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi" ni wazi kuwa ni mfano, kama usemi: "anayetaka kuwa wa kwanza, atakuwa mtumwa wa wote."  Bila ya shaka hapana atakayeona kuwa Yesu alikusudia kwa neno "mtumwa" ni kiumbe wa kuuzwa na kununuliwa. Hali kadhaalika "kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi" sio maana yake lazima kuuwawa.  Tafsiri ya Biblia The Interpreter's Bible inasema wazi juu ya kauli hiyo ya Yesu kuwa haiwezekani kuitumia kuwa ni ushahidi wa thiolojia ya Paulo ya kuokoka kwa damu.  Kauli hii lazima ichukuliwe kama ni mfano, kama usemi wa kishairi, kama ni mshabaha.  Wako baadhi ya wataalamu wa Kikristo ambao wanasema kauli hii ama iliongezwa na Marko au na mtu mwenginewe baadae, lakini Yesu hakusema hayo.  Lakini wenye kuandika hiyo tafsiri ya Biblia wanaona kwamba maneno hayo kayasema Yesu na yana maana ya mfano kama "vile mashahidi wa Kiyahudi walivyokufa kwa kuwaokoa watu wao (II Macc. 7.37-38; IV Macc. 17.22)"  Ikiwa maana yake ni hivyo wanaona wafasiri wa Interpreter's Bible yaweza kuwa kauli hiyo ni kweli ya Yesu, kama ikichukuliwa maana nyengine haiwezi kuwa ni kweli.
Katika gazeti moja la Misri ilitoka picha ya kuchora ya kuwapiga vijembe wale wanaotetea viti vya bunge.  Picha ilionyesha mazishi. Watu wamechukua jeneza ambalo limezungushwa bendera kubwa ilioandikwa:  "Mtu Anayekufa kwa Ajili Yenu".  Utepe uliotatiza shada la mauwa liliochukuliwa mbele ya jeneza uliandikwa: "Mpaka Makao yake ya Mwisho ya Kupumzika, Kiti cha Bunge."  Na mtu mmoja akisoma: "Mtilieni Voti!"  Katika wale wendao mazikoni mmoja lilimdondoka chozi, mwenzie akamzindua:

"Jizuie, mwanamume wee! Hii na kampeni tu!"

Ikiwa basi Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za watu, na ikiwa kweli yeye ni Mungu, basi mambo yote hayo ni kama sarkasi tu, mchezo wa kuigiza, au kiini macho.  Kwani hakika Mungu haiwezi kuwa aliona uchungu kwa yale mateso, na kufa kwake kulikuwa hakuna maana, kwani kumbe hakufa.  Mungu hufa?  Yote hayo yaonyesha kuwa ni udanganyifu mkubwa.
Na ikiwa yote hayo yalikuwa yamekwisha kadiriwa tangu mwanzo na kupangwa na kutimiza bishara za kinabii na kwa kupenda kwake Yesu, basi hao waliomtesa na wakamwua yafaa wafikiriwe na watukuzwe kama ni watu wema waliowaletea kheri wanaadamu wote, na wakamsaidia Yesu kutimiza lile alilolijia.  Hao akina Yuda, na Pilato, na lile baraza la wakuu wa Kiyahudi, wote hao ndio vipenzi vya Mungu, waliotimiza mapenzi ya Mungu baraabara.
Kifungu kingine cha maneno ya Biblia kinachonukuliwa mara nyingi kutilia nguvu imani ya kuokoka kwa damu ya Yesu ni hiki kutokana na Luka:
Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.
Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Luka 1.67-71
Bishara  hii ni ya Zakaria alipozaliwa mwanawe Yohana (Nabii Yahya). Lakini ni wazi kuwa anasema ni Bwana Mungu ndiye aliyewaokoa watu wake kwa "kuwasimamishia pembe ya wokovu", naye ni Masihi aliyekuwa akitarajiwa na Mayahudi kuja kuwakomboa kutokana na adui zao wanaowachukia, nao ni watawala wa Kirumi. Kuja huyo mwokozi, anasema Zakaria, ni kutimiza yale maneno waliyoyasema manabii wa zamani.  Ni kuyapotoa maana ya maneno tukifasiri utabiri huu kuwa maana yake ni kuokolewa kwa damu ya Yesu.
Ushahidi mwingine unaodaiwa kuwa ni dalili ya uwokovu kwa damu ni huu:
 Siku ya pili yake (Yohana Mbatizaji) amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
Yohana 1.29
Hata tukijaalia maneno haya ya Injili ya Yohana ni kweli (kwani hayathibitishwi na Injili zote nyenginezo) basi si kama tunavyomtaja kiongozi ye yote wa kidunia hivi leo kwa kusema: "Muangalieni huyo anayetubebea mizigo yetu yote"? Au tunapomwonya mmoja wetu: "Baba, utajiua nafsi yako kutaka kujitwika mambo ya ulimwengu mzima kwenye mabega yako hayo!" Kuchukua dhambi si lazima iwe maana yake ni kusamehewa dhambi kwa kuuliwa Yesu; bali ni kwa kuyafuata mafunzo yake na kwenda mwendo wake ndio watu watapata uwokovu.  Ni kwa kuyatenda mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliyemtuma mtumishi wake Yesu, kuwa ni Nabii na Mtume, kama mwenyewe mara nyingi alivyosema, ndio watu wataokoka.  Ni kwa kutenda mema na yaliyokuwa ya murwa kwa mujibu wa mapendo na sharia za Mwenyezi Mungu ndio kila mtu ataweza kujiokoa nafsi yake. Sifa, bila ya shaka, itamrejea yule mwenye kuonyesha njia, na kwa hakika hivyo ndio amekuwa ni mwokozi wa watu. Mafunzo na maisha yake Yesu ndio muhimu yenye maana, na ndio hayo amejia duniani. Ama mateso yaliyompata ni matukizi yaliyomzukia katika ile kazi yake, wala yeye hakuyapenda; au asingekimbia na kujificha na kumwomba Mungu amwondolee kikombe cha mateso na mauti.  Yatufalia basi kuyatupa kando yaliyo muhimu na yenye maana, na tukan'gan'ganilia yaliyozuka tu?

Kifungu hichi kifwatacho kutokana na Injili ndicho kinachoonekana chenye ushahidi mkubwa wa imani ya kuokoka kwa damu:
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
Yohana 3.16-17
Hapa yafaa tutambue kuwa hii Injili ya Yohana ni khitilafu kabisa na zile nyengine tatu.  Hii iliandikwa mwishoni kabisa baada ya zile.  Tangu awali haikukusudiwa hii kuwa ni maelezo ya kweli kueleza maisha ya Yesu kama yalivyokuwa, bali ilikusudiwa kuwa ni maoni ya huyo mwandikaji, naye amejaza humo mawazo yake mwenyewe.  Ni dhaahiri kuwa Injili ya Yohana ilikusudiwa kuthibitisha imani ambazo alikuwa zilikwisha mvaa mwandikaji. Wakati ilipoandikwa Injili hii Ukristo wa Paulo ulikuwa umekwisha pata nguvu na huyu mwandikaji alikuwa bila ya shaka ni mfuasi wa Ukristo wa Paulo, sio ule wa Yesu uliokuwa ukifuatwa na wanafunzi wake wa mwanzo. Katika Injili hii ungu wa Yesu unatiliwa mkazo, na Yesu ndio anaitwa "Mwana wa pekee wa Mungu."  Juu ya hivyo hii imani ya kuokoka kwa damu hata katika Injili hii haikusemwa kwa uwazi. Sana sana, itakuwa kama imegusiwa tu.  Ni yule mtu ambaye akili yake tangu hapo imekwisha pikwa ndiye atafasiri maneno haya:
 "Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye," kuwa maana yake ni kwa kufa kwake juu ya msalaba; au akafasiri "kila mtu amwaminiye" kuwa maana yake ni kuamini kuwa kifo chake kitakuwa ni fidia kwa dhambi za watu.

Dr. Hugh Schonfield katika Those Incredible Christians anatueleza kwa vizuri nini thamani ya Injili hii  kama alivyoiandika Yohana katika kusimulia maisha na mafunzo ya Yesu Kristo.  Anasema:
"Basi ndio hivyo katika Injili Yane,  kama katika barua ziliopelekwa kwa Makanisa Saba, si Yesu wa hakika ndio asemae, lakini ni Yohana Mkubwa ndiye anayesema kwa jina lake.  Juu ya hivyo uzushi hapo unaweza kutambulikana, si tu kwa kuwa Kristo wa Injili Yane anajieleza kwa namna ambayo si ya Kiyahudi, lakini zaidi ya hayo kwa sababu ushahidi wa waraka wa kwanza wa Yohana unadhihirisha kuwa Yesu anasema kwa njia anavyoandika huyo aliyebuni hayo yanayodhaniwa kuwa ni maneno yake. Yafaa tuwe na shukrani sana kwa kuwepo waraka huu.  Hapana haja ya kutishika kwa wazo la kuwa Mkristo hodari na hata kuwa ni mwenye mawazo ya kiroho ambaye maandishi yake yametiwa katika mkusanyo wa nyaraka takatifu, kuwa anaweza kuwa na khatia ya udanganyifu mkubwa kama huu. Yafaa iwe wazi kwetu hivi sasa ya kwamba viko vitabu kadhaa wa kadhaa katika Agano Jipya ambavyo ni vya uwongo, na vingine ambavyo vimekusudiwa kupotoa.  Hukumu yetu ya nini jema na nini baya tusiitumilie katika haya maandishi ya kale, katika zama ambazo haikuonekana kuwa ni makosa kuzua, kuongeza, au kugeuza nyaraka kwa sababu ya jambo la kheri. Kwa yakini Yohana alikuwa anaamini kuwa hizo mbinu zake ni za kuhesabiwa kuwa ni za haki na kuwa linaongozwa na Mungu. Hakuwa na shaka hata chembe kuwa alikuwa akiamini ya kwamba yeye kaletwa na Mungu kwa ajili ya kazi hiyo aifanyayo, na kwamba yeye anaongozwa na Roho (Mtakatifu). Yalivyokuwa mambo yote yanamwendea sawa yalizidi kuthibitisha hiyo imani yake."



12- PAULO AU YESU? IMANI AU MATENDO?

Hebu yazingatie Mahubiri ya Yesu aliyotoa juu ya Mlima wa Zaituni:
Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii;  la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.  Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni;  bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5.17-20
Mnamo mahubiri ya Mlima wa Zaituni ndio yanapatikana mafunzo makubwa ya Yesu Kristo.  Tunaweza kusema kuwa humu, khasa, ndio umo Ukristo;  yaani ikiwa tunaamini ya kuwa Yesu ndiye Katika kifungu cha maneno hayo tuliyoyanukulu ya Yesu tunaona ya kuwa ni muhali mtu kuingia katika ufalme wa mbinguni, yaani Peponi, mpaka haki ya mtu izidi ile ya waandishi na Mafarisayo. Yaani wema uutendao uzidi ule wa wanazuoni wa Kiyahudi.  Ni nini hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo?  Ni kuifuata sharia ya Taurati neno kwa neno, na pia waliofunza manabii wengineo.  Ndio maana Yesu akasema:  "Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, sikuja kutangua, bali kutimiliza." Kazi yake haikuwa kutengua sharia ya Taurati na kuleta kitu kingine cha kutengua au kugonganisha na mafunzo ya sharia ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, bali kaja yeye kutimiliza kwa kuwafunza Mayahudi umuhimu wa mambo ya kiroho katika sharia. Kutii madhaahiri ya sharia tu na kuwacha undani wake, uchamngu, hakutoshi. Mwenyezi Mungu atiiwe kwa dhaahiri na kwa siri.  Yesu alishikilia sana kufundisha na kutenda, aliposema:  "Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni;  bali atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni."

Katika amri za Taurati ni kama hii iliyomo katika Biblia:
Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao;  hao ni najisi kwenu.
Mambo ya Walawi 11.7-8
Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake;  atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.  Tena kila mtu atakeykula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni;  ndipo atakapokuwa safi.
Walawi 17.14-15
Hizo ni amri ziliomo katika Taurati, sharia ya Mungu, ambayo Yesu amesema kama ilivyo katika Injili ya Mathayo kuwa mwenye kuivunja ndogo yao na akawafundisha watu hivyo basi ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni.  Na kuvunja hayo khasa ndio Paulo kafundisha. Msikieni:
Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;  maana Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.
1 Wakorintho 10.25-26
Mnamwona Paulo anavyobomoa sharia ya Taurati  waliyoifwata Manabii wote, hata Yesu na wanafunzi wake thenashara, ya kuwa kuna vyakula vilivyo halali na kuna vingine ni najisi, haramu kuliwa, kama nguruwe, vya kunyongwa na damu?  Yesu kafunza nini, na Paulo anafunza nini!
Katika waraka wake aliowapelekea Wagalatia Paulo anasema:
Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema, Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.
Wagalatia 5.4-6
Kwa kauli moja Paulo ameitengua sharia yote. Yesu kasema nini juu ya Mlima wa Zaituni na Paulo anasema nini katika barua yake kwa Wagalatia?  Yesu alifuata sharia ya Mwenyezi Mungu na aliihishimu na akaahidi kuwa yeye hatoitengua kabisa, ila ataitimiza. Paulo anaibeza sharia na kuiona kuwa ni laana. Yesu akila kilicho halalishwa na Mungu, na alikiepuka kilicho harimishwa na Mungu. Paulo anatwambia tule kila kiuzwacho sokoni bila ya kujali dhamiri yetu.  Yesu na Manabii wote tangu Nabii Ibrahim walitahiriwa kwa kufuata amri ya Mungu kama isemavyo Biblia:
Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.  Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.
Mwanzo 17.9-10
Paulo mjuaji, anasema kumpinga Mungu:
Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.
Wagalatia 6.15
Katika barua yake aliyowapelekea Warumi ndio kabisa Paulo anaiangamiza sharia ya Mungu na kufanya vitendo kuwa havina maana yo yote.Chenye maana peke yake ni imani tu.
Basi, twaona ya kuwa wanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
Warumi 3.28
Kwa Paulo kuamini kuwa Yesu kafa msalabani na damu yake kuwa ni fidia kwa dhambi zetu ndio kwenye maana, sio kufuata sharia wala vitendo.  Kwake yeye ile Taurati, ambayo Yesu mwenyewe hakuja kuitengua bali kaja makusudi kuitimiza, ni kifungo na pingamizi. Anawaambia Warumi:
Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
Warumi 7.6
Paulo anaiona Taurati ni kifungo, pingamizi, bali ni laana. Hayo sio maoni ya Yesu ambaye amesema: "Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka." Je, kwa kuingia Paulo katika umoja wa Kikristo ndio tusema mbingu na nchi zimeondoka?  Au kwa kutundikwa Yesu msalabani (ikiwa kweli katundikwa) ndio tuseme mbingu na nchi zimeondoka? Mbona watu wameyasahau upesi maneno ya Yesu mwenyewe, na kuyasikiliza ya Paulo? Kwa sababu yanakubaliana na matamanio yao?
Mafunzo ya Paulo yalileta mzozano na ubishi mkubwa tangu pale mwanzo katika historia ya Kanisa baina ya kikundi chake cha Wakristo waliomfuata kutoka upagani, na wale Wakristo wa asli ya Kiyahudi.  Wao walipinga moja kwa moja ile shauri ya kwenda kupelekewa mafunzo ya Ukristo mataifa waliokuwa hawakutahiriwa, wala hawaikubali sharia ya Taurati.  Baadhi ya wanafunzi wa Yesu walikuwa hawakubali hata kula nao wale "wasiotahiriwa".  Wao walikuwa wanajua vyema kuwa Yesu aliwakataza wasend kuwahubiria mataifa mengine isipokuwa Mayahudi tu, kwani ni wao ndio walikuwa wanaamini Mungu Mmoja na wao ndio wakiifuata sharia ya Mungu. Mwishoe ulifanywa mkutano na yakawapo baadhi ya masikilizano kuwa yafaa kuhubiriwa Ukristo kwa mataifa yasiokuwa ya Kiyahudu, na wao wasilazimishwe kubeba mizigo mizito katika dini kama vile wenye asli ya Kiyahudi.  Walitumwa Paulo na Barnaba kuwaendea hao mataifa, nao ni Wazungu wa Kirumi na Kigiriki, na wakachukua barua iliomalizikia maneno haya muhimu:
Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa na uasherati.  Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu.
Matendo 15.28-29
Nyama zilizosongolewa, yaani nyama za kunyonga, zisiochinjwa. Yazingatieni haya si maamrisho ya Yesu, lakini ni masikilizano baina akina Paulo na wanafunzi wake Yesu,(kwa ridhaa ya Roho Mtakatifu) baada ya kuwa Yesu mwenyewe hayupo tena. Ikiwa hayo ndiyo waliokubaliana ilikuwaje Paulo tena kuwaandikia Wakorintho: "Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni bila ya kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri"? Lakini Paulo ni Paulo.

Mtakatifu Paulo anadai kuwa yeye aliteuliwa makhsusi kuwa ni mtume wa Yesu katika ufunuo (Wahyi), na kuwa bado yeye anaendelea kupata amri moja kwa moja kutokana na mwenyewe Bwana Yesu, ijapokuwa amri hizo na mafunzo hayo yanapingana kabisa na yale waliyoyapata wale wanafunzi wake Ysu waliokuwa naye mwenyewe alipokuwa hai. Yeye Paulo hakupata kuonana na Yesu, bali yeye alikuwa ni mpinzani mkubwa wa Ukristo na akawa ni sababu ya kuteswa na kuuwawa Wakristo kadhaa wa kadhaa, mmoja wao ni Mtakatifu Stefano, shahidi wa mwanzo katika Wakristo. Paulo alikuwa na asli ya Kiyahudi, na dini yake rasmi ilikuwa ya Kiyahudi.  Kwa kuwa alizaliwa nje ya Palastina katika mamlaka ya Kirumi alikuwa na uraia kamili wa Kirumi, na huko alipata fursa ya kusoma ilimu na falsafa za Kiyunani.  Mazingara yake yote ya Kigiriki na Kirumi yalikuwa ya kikafiri, kipagani.  Kwani Magiriki na Warumi walikuwa washirikina wenye kuamini chungu ya miungu, kama ilivyokuwa ada ya karibu mataifa yote ya wakati ule isipokuwa Mayahudi. Yalipozuka mafunzo ya Yesu Kristo, ambayo kwa asli yake hayakuwa ila ni kuendeleza ile ile imani ya Kiyahudi ya Mungu Mmoja na kufuata sharia ya Taurati na kuongeza uchamngu, na ikawa mafunzo hayo yanaendelea juu ya kupingwa, Paulo aliona anaweza kuipa nguvu hiyo dini au kwa hakika madhehebu mpya kwa kuwatia wale Warumi na Magiriki kwa kuchanganya imani zao na falsafa zao pamoja na imani ya Kiyahudi.  Mayahudi wanaamini Mungu Mmoja, ndio. Ukristo unaamini Mungu Mmoja.  Magiriki na Warumi wanaamini miungu mingi, si chini ya watatu, ndio na Ukristo nao unaamini hivyo. Jee, si pana mgongano hapo? La, katika Ukristo imani ni ya Mungu Mmoja katika Utatu Mtakatifu: Mungu Mmoja, mwenye nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mapagani wa Kigiriki na Kirumi wakiamini mungu aliyekufa, akafufuka na akapaa mbinguni. Hilo si kitu wanaweza kuendelea na imani hiyo katika Ukristo. Wazungu magovi hawataki kutahiriwa. Hapana kitu, kutahiriwa si kitu wala kutotahiriwa. Hoja ipatikane tahara ya roho. Wazungu wamezoea kula kila kitu, nguruwe, damu, kilichochinjwa na kisichochinjwa. Hilo si tatizo, mtaendelea vivyo hivyo, kwani dhambi ni kitokacho mdomoni, sio kiingiacho.  Kuleni kila kiuzwacho sokoni. Hapana halali wala haramu.  Huo ndio Ukristo mpya wa Paulo, na hiyo ndio Thiolojia yake ambayo, inasikitisha Wakristo wameifuata, wakayaacha mafunzo mepesi na yaliyonyooka ya mwenyewe Yesu Kristo.
Hayo ni maji makuu, letu sisi ni kuangalia yaliyomo ndani ya Biblia Takatifu. Tuiache hiyo iseme.  Khabari za kugeuka Paulo akaacha kumpinga Yesu, na badala yake akawa mfuasi wake zinasimuliwa pahala patatu katika Matendo ya Mitume katika Agano Jipya la Biblia. Na katika zote mara tatu kisa hicho kinakhitalifiana katika mambo muhimu. Kwanza tunasoma katika Sura ya 9 mstari wa 3 mpaka wa 7:
Hata (Paulo) alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, (yaani Paulo) mbona waniudhi?  Akasema, U nani wewe, Bwana?  Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.  Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.  Na wale waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.
Matendo 9.3-7
Katika maelezo hayo hapo ni mwandikaji anasimulia. Yapo mambo mane lazima tuyazingatie vizuri katika maelezo hayo:
  1. Mwangaza ambao Paulo ulimwangaza.  Haikusemwa kuwa wengine waliuona mwangaza ule au la, lakini waliisikia sauti.
  2. Ni Paulo ambaye "akaanguka chini."
  3. Yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye waliisikia sauti, lakini hawakumwona mtu.
  4. Sauti ya Yesu ilimuamuru "aingie mjini, naye ataambiwa yampasayo kutenda."  Hapo hakuambiwa nini la kutenda.
Katika Biblia hiyo hiyo, katika kitabu hicho hicho cha Matendo ya Mitume, sura 22, mstari wa 6 mpaka wa 10 ipo ncha ya pili ya hadithi kusimulia tukio lile lile. Msimulizi hapa ni Paulo mwenyewe:
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi (yaani chini), nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?  Nikajibu, Wewe u nani, Bwana?  Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.  Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana?  Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.
Matendo 22.6-10
Ncha hii yakubaliana na ile ya mwanzo katika mambo haya:
  1. Aliyeanguka chini ni Paulo na sio wale waliokuwa pamoja naye.
  2. Aliloambiwa Paulo ni kuingia mjini na huko ndiko atakoambiwa nini la kulifanya.
Ncha hii lakini inakosana na ile ya kwanza kuwa ya kwanza yasema ya kuwa wale waliokuwa naye "wakasimama kimya, wakisikia sauti, lakini haikusema kuwa waliona nuru.

Katika ncha hii ya pili twaambiwa: waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti.

Ncha ya tatu  ya tukio hilo hilo muhimu kabisa katika historia ya Ukristo inaelezwa katika maneno yake mwenyewe Paulo vile vile kama inavyosimuliwa katika kitabu kile kile cha Matendo ya Mitume sura ya 26 mstari wa 12 mpaka wa 18:
Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;  Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi (chini) sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli!  mbona waniudhi? ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo (ujiti wenye ncha wa kuchokolea). Nami nikasema,Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.  Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;  nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;  uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.
Matendo 26.12-18
Sasa hapa tunaona khitilafu kubwa na zile ncha za hadithi ziliomo katika sura ya 9 na sura ya 22 katika hicho hicho kitabu kimoja cha Matendo ya Mitume. Hebu tuchungue:
  1. Kwa mujibu wa ncha hii si Paulo pekee aliyeona nuru - kama ilivyoelezwa pale mara ya kwanza - lakini wote waliokuwa naye waliona nuru, kama ilivyoelezwa mara ya pili.
  2. Hapa Paulo anasema: Tukaanguka nchi sote. Haya yanapinga ncha ya kwanza na ya pili zilizosema kuwa ni Paulo tu peke yake ndiye aliyeanguka chini.
  3. Katika masimulizi ya kwanza na ya pili ilisemwa wazi kuwa Paulo aliambiwa aingie mjini Demeski na huko ataambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa ayafanye.  Hii mara ya tatu mambo yote ameamuriwa hapo hapo kabla ya kuingia mjini, kinyume na ilivyosimuliwa mara ya kwanza na ilivyosimuliwa mara ya pili. Tena hapo Paulo alimsikia Yesu anamuamrisha amri kinyume na alivyokuwa akiwafunza na kuwaamrisha wanafunzi wake siku zote katika uhai wake - anamuamrisha Paulo apeleke utume wa Yesu kwa mataifa mengine yasiyokuwa Mayahudi. Kadhaalika kinyume na mafunzo ya Yesu katika uhai wake anamuamrisha afunze kuhesabiwa haki kwa imani na kufutiwa dhambi.
Ni wazi kuwa Paulo kabla ya kutanasari kwake alikwisha jitayarisha namna gani atavyougeuza Ukristo wa Yesu, waliokuwa wakiujua wote wanafunzi wake kumi na mbili, uwe Ukristo wake yeye Paulo.
Na kwa nini Paulo aliongeza mengi aliposimulia mara hii ya tatu kuliko ilivyosimuliwa zile mara mbili za mwanzo?  Ni kwa sababu hapa anasema na Mfalme Agripa.  Lakini yafaa tusite na tujiulize:  Nini thamani ya shahidi anayetoa ushahidi wake kwa polisi, akaubadilisha kidogo akifika kwa hakimu, na akatoa hadithi nyengine kabisa anapofika mahkama kuu kwa jaji?  Hapana awezae kumueleza Paulo alivyo kama alivyojieleza mwenyewe katika barua yake aliyowapelekea Wakorintho.  Amesema:
Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi.  Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi;  kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria,) ili niwapate walio chini ya sheria.  Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.  Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.
1 Wakorintho 9.19-22
Yaweza kuwa ni kweli kuwa mwenyewe Paulo akiamini kuwa hila hizo zote azitendazo ni kwa ajili apate "kuwaokoa watu."  Wengi miongoni mwa wataalamu wa Biblia wanakubaliana na Dr. Craveri na Dr. Schonfield kuwa makusudio ya Paulo ni kuwa apate yeye binafsi wafuasi wengi zaidi ili apate kuwashinda wale wanafunzi wa Yesu mwenyewe. Kwa hivyo ndio akawa hasikii haoni. Kwa lengo hilo yu tayari kufanya lo lote, hata akakhiari kugeuza mafunzo ya Kristo ili apate wafuasi yeye "kwa jina la Kristo." Kwa hakika wale wafuasi wake kutokana na mataifa walibakia kuwa vile vile makafiri ila waligeuzwa jina tu, wakaitwa Wakristo.  Ndio hivyo alivyowaandikia Warumi:
Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako:  yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
Warumi 10.8-9
Ndio hivyo Ukristo umerahisishwa na Paulo ili isiwe taabu kwa makafiri waweze kuitwa Wakristo bila ya kuufuata Ukristo wa Yesu. Katika mtindo huu Paulo alipata upinzani kutokana na wengi, kama tunavyoona katika waraka wa Yakobo, nduguye Yesu, unavyofunza imani ya matendo, si imani tupu. Natusome:
Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo?  Je! ile imani yaweza kumwokoa?  Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?  Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.  Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja;  watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.  Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? Je!  baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki;  naye aliitwa rafiki ya Mungu. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake;  si kwa imani peke yake.  Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je!  hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?  Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.
Yakobo 2.14-26
Mafunzo haya yanapingana moja kwa moja na yale ya Paulo, na yanakubaliana moja kwa moja na yale ya Yesu, mwenyewe.  Si ajabu basi kumsikia Paulo anakakamia kwa hasira isiyofichikana akisema:
Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi;  ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi.  Maana watu kama hao ni mitume wa uwongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.   Wala si ajabu.  Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake hao wakajigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.
2 Wakorintho 11.12-15
Ni dhaahiri kuwa Paulo anakusudia kwa matusi yake haya kuwatukana wale wanafunzi wa Yesu, ambao Yesu mwenyewe aliwateua, ambao wakiongozwa katika kutimiliza ujumbe wa Yesu na watu kama Yakobo, ambaye anaambiwa kuwa ni nduguye Yesu.  Je, sisi tutendeje tunapokabiliwa na maoni mbali mbali yanayogongana miongoni mwa watu ambao wote wanadai kuwa ni wanafunzi wa Yesu, ijapokuwa huyu mmoja Paulo, hata hakumwona Yesu, na huo ushahidi wa kuwa kamwona katika njozi ni wake yeye tu, tena unagongana na kupingana wenyewe kwa wenyewe?  Tutendeje? Liliopo ni tuyaendee mafunzo yake mwenyewe Yesu, ambayo ijapokuwa yametatanishwa na maongezo na mapunguzo, lakini hayaachi kuwepo ya kutosha kwa jumla kutufahamisha nini khasa mafunzo yake.  Ikiwa kweli tunatafuta hakika ya mambo na ukweli wake basi tutayachukua yale yalio wazi, dhaahiri, katika maneno yake mwenyewe Yesu, na tusiyabali yale ambayo ni maneno ya wasimulizi.  Kadhaalika yasitushughulishe yale ya mafumbo yanayotatanisha tukajaribu kuleta tafsiri na maelezo tuyapendayo nafsi zetu.  Ikiwa ni kufasiri basi tufasiri fumbo kwa kauli ya Yesu ilio wazi. Wapotoshaji hufanya kinyume cha hayo.
Mafundisho yaliyotulia kabisa ya Yesu ni yale aliyohubiri juu ya Mlima wa Zaituni.  Na maoni yake yaliyo wazi na kauli ya kukata juu ya sharia na matendo, ni yaliyomo katika sura 5 ya Mathayo. Akizungumzia juu ya wale wanaodai kuwa wao ni wafuasi wake, na kuwa ati wanafunza mafunzo yake, na huku kumbe wanayapotoa yale aliyoyafunza, Yesu anaambiwa kasema:
Si kila mtu aniambaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni;  bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.   Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?  Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.  Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile isianguke;  kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.  Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka;  nalo anguko lake likawa kubwa.
Mathayo 7.21-27
Hayo ni maneno aliyokhitimishia Yesu mawaidha yake juu ya Mlima wa Zaituni.  Ni maneno yaliyokaa sawa, yawazi, hayana ubabaishi.  Ni nani hao "watendao maovu", hao wapumbavu, wasiofuata mafunzo ya Yesu wakayatenda, mafunzo ambayo msingi wake ni kutimiliza sharia na manabii, na kutenda mapenzi ya Mungu?  Ni nani hao wanaodai kufanya miujiza na kuponyesha watu kwa jina la Yesu, na kudai kuwa ni mitume wa Kristo, na huku wanapinga mafunzo yake, na kuwaambia watu kuwa wataokoka kwa imani tu kwamba Yesu kafa msalabini kwa ajili yao, bila ya haja ya vitendo?  Ni nani hao wanaolitumia jina la Yesu naye mwenyewe atawakataa?  Kama tuna akili basi yafaa tuitumie.  Tusiwe kama mtu mpumbavu ajengaye nyumba yake juu ya fungu la mchanga.  Tutaanguka, na anguko letu litakuwa kubwa.
Mafunzo ya Yesu Kristo si haba, lakini kwa ufupi wa maisha yake (aliwahi kuhubiri kiasi miaka miwili mitatu tu) na kutokuwa tayari ulimwengu kuchukua kweli yote, hakuweza kutimiza ujumbe wote wa Mwenyezi Mungu.  Ni hikima yake Mwenyezi Mungu kuwa kila nabii aliyemleta alikuwa anaongeza juu ya yale yaliyotangulia.  Ni kweli Yesu alisema kama ilivyo katika Mathayo 5.17-20 ambayo tumekwisha yataja kuwa yeye alikuja kutimiza Taurati na mafunzo ya Manabii, hakuja kutengua lo lote katika hayo.  Ulipokaribia wakati wake wa kuondoka aliungama kuwa mengi aliyo nayo hana nafasi ya kuyasema, lakini atakuja mwenginewe ambaye atauwongoza ulimwengu kwenye kweli yote, na ataufundisha ulimwengu mafunzo kaamili juu ya dhambi na haki.
Injili ya Yohana inanukulu maneno ya Yesu:
Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?  Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.  Lakini mimi nawaambia iliyo kweli;  yawafaa ninyi mimi niondoke;  kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu;  bali mimi nikenda zangu, nitampeleka kwenu.  Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.  Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;  kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.  Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia,  lakini hamwezi kuyastahamili hivi sasa. Lakini yeye atapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote;  kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe lakini yote atayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.  Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.
Yohana 16.5-14
Kwa mujibu wa maneno hayo kama ilivyo katika Injili ya Yohana, Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa yeye yu karibu kuondoka duniani, na ya kwamba hajatimiza ujumbe wake, lakini atakuja mwenginewe ambaye ameitwa majina mbali mbali kwa mujibu wa tafsiri mbali mbali za Biblia.  Hapa anaitwa Msaidizi katika tafsiri hii ya Kiswahili inayoitwa Union Version.  Kwa mujibu wa tafsiri ya zamani ya Kiingereza, King James's Authorised Version, anaitwa Comforter, yaani Mliwazi;  na kwa mujibu wa tafisiri nyengine ya Kiingereza ya kisasa Revised Standard Version, anaitwa Counsellor, yaani Mshauri, na tafsiri nyengine mpya mpya za Kiingereza anaitwa Helper, ambayo maana yake pia ni Msaidizi. Tafsiri ya Kiarabu ya Darul Kitabul Muqaddas ya Cairo anaitwa Al Mu'azzi yaani Mliwazi.  Vyo vyote vile iwavyo huyo Msaidizi, au Mliwazi, au Mshauri, ameelezwa na Yesu kwamba:
  1. Atakuja baada yake Yesu, yaani wakati huo hayupo;
  2. Atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki na hukumu;
  3. Atauongoza ulimwengu autie kwenye kweli yote;
  4. Hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini atakayoyasikia atayanena;
  5. Atatoa khabari ya mambo yajayo;
  6. Atabakia nasi milele;
  7. Atamtukuza Yesu Kristo.
Hebu natuichungue bishara hii ya Yesu bila ya chuki, bila ya mapendeleo, na bila kutiwa pingu na mawazo tuliyofungwa nayo tangu utotoni.  Sasa tu watu wazima na tuna akili zetu, natuzitumie. Wakristo wengi wanachukulia kuwa huyo Msaidizi ni Roho Mtakatifu, nafsi ya pili ya Mungu.  Hivyo ndivyo walivyofundishwa Kanisani na mapadri.  Imani hii yazidi kutiliwa nguvu na hiyo kauli "huyo roho Mtakatifu" iliotiwa kati baada ya neno "Msaidizi" liliomo katika mstari wa 26 sura ya 14 ya hii Injili ya Yohana. Hapana lawama basi kuwa baadhi yetu tukawa tunaamini kuwa Yesu ametwambia katika Yohana 14 na 16 kuwa atakuja Roho Mtakatifu ndiye atayetuongoza na kutufundisha yote yaliyobaki sisi kufunzwa, na ambayo yeye Yesu hakuwa na wakati kufundisha au watu wakati ule walikuwa bado hawajawa tayari kuyapokea.  Kwa kuwa Roho Mtakatifu anaongoza Kanisa la Yesu (yaani ndio Mapadri, tangu Baba Mtakatifu mpaka Maaskofu na Mapadri wote, na Wazee wa Kanisa,  na Wachungaji) ndio Wakristo hawana wasiwasi wala hawajiulizi kwa nini leo wanafundishwa mambo ambayo Yesu hakuyafundisha, na wanapewa amri, au kukatazwa jambo, ambalo Yesu hakuliamrisha au hakulikataza. Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Mungu, ni sawa sawa na Yesu, basi ana madaraka kuendelea kufunza, kuamrisha na kukataza, kama Yesu, Mungu Mwana, na Mwenyezi Mungu, Mungu Baba.  Yesu alionekana na watu walimwona. Alisema na maneno yake yameandikwa. Lakini Roho Mtakatifu ananon'gona na Mapadri tu na Wakristo wanafuata wanayoambiwa na Kanisa, yaani Mapadri. Si ajabu kuona wanaojiita Wakristo wanafuata Kanisa zaidi kuliko kumfuata Yesu Kristo mwenyewe kwa sababu wamejazwa katika akili zao kuwa nafsi ya pili ya Mungu ipo Kanisani ikiendeleza kuugeuza Ukristo wa Yesu kama ipendavyo hiyo nafsi. Lakini natuyazingatie haya:
Kwa mujibu wa imani ya Kanisa, Roho Mtakatifu ni Mungu, ambaye ni sawa na Mungu Baba, na Mungu Mwana.  Tumeona katika maneno ya Yesu kuwa Msaidizi atakuja baada yake Yesu, yaani wakati huo hakuwako. Je, tuseme kuwa wakati wa Yesu hakuwako Mungu Roho Mtakatifu?  Mbali ya kuwa Roho ameelezwa mara nyingi sana katika Agano la Kale, na kuwa ndio akiwaongoza manabii wote, bali Wakristo wanaamini kuwa waandishi wote wa vitabu vya Biblia, kabla na baada ya Yesu, waliongozwa na Roho Mtakatifu. Tunasoma humu humu katika Injili ya Yohana sura ya kwanza mstari wa 32:
Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni;  naye akakaa juu yake (Yesu).
Yohana 1.32
Tena tunasoma katika Injili ya Marko:
Mara Roho akamtoa (Yesu) aende nyikani.
Marko 1.12
Na tunaona katika Luka:
Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo;  naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.  Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.
Luka 1.15-16
Roho Mtakatifu daima dawamu yu pamoja na Yesu, hangojei kuondoka kwake ndio aje. Alikuwa na Yohana Mbatizaji (Nabii Yahya) tangu tumboni mwa mamaake.  Luka hapo anatupa ushahidi kuwa Yohana hakupata kunywa divai wala kileo "kwa sababu atakuwa mkuu mbele ya Mungu" .  Ni nani, basi aliyewahalalishia Wakristo kunywa ulevi, hata ikawa ibada yao haitimii ila wanywe mvinyo?  Labda ni Paulo akiongozwa na Roho Mtakatifu. Ni kweli wafuasi wa kweli wa Yesu sio wale wapigao kelele, Bwana, Bwana, sisi twaamini uwokozi wa damu yako. Wafuasi wake wa kweli ni wale wanaotenda aliyofundisha, na wanaokwenda mwendo wake. Hao hata hawana haja ya kujiita Wakristo.

Si kama Roho Mtakatifu alikuwa na Yesu tangu tumboni mwa mamaake tu kama Yohana, bali tunaambiwa na Injili ya Mathayo kuwa hiyo mimba yenyewe kaichukua mama yake, Mariamu, "kwa uweza wa Roho Mtakatifu." (Mathayo 1.18).

Ni wazi kabisa kuwa Roho Mtakatifu hakungojea Yesu aondoke ndio aje, bali daima milele yupo, kwa ushahidi wa Biblia yenyewe. Kwa ushahidi huu tu tunayakinika kuwa huyo Msaidizi ajaye, siye Roho Mtakatifu, nafsi ya pili ya Mungu.
Tena tunaambiwa kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayeongoza Kanisa mpaka hii leo. Lifanywalo na lisemwalo na Kanisa basi ni kwa uwongozi na ufunuo wa Roho Mtakatifu, huyo aliyebashiriwa na Yesu kama ilivyosimuliwa katika Injili ya Yohana. Lakini ilivyokuwa Ukristo ulivyogawika katika makanisa, au madhehebu, yasiokuwa na hisabu, na kila kanisa linafunza mambo ambayo tangu msingi wake yanakhitalifiana na mengineyo, jee ni madhehebu gani, au kanisa gani, linaloongozwa na Roho Mtakatifu.

Kama wote hao wanaongozwa na Roho huyo huyo basi mbona wanagongana katika mambo ya msingi? Bali hata kanisa moja, mathalan, Kanisa Katoliki la Roma, ndilo kubwa lao na lenye nidhamu kuliko yote, mbona mara nyingi hugeuza geuza maoni yake?  Zamani tulipokuwa wadogo ilikuwa mwiko kwa Wakatoliki kula nyama siku ya Ijumaa, kwa kuwa ndio siku aliyotundikwa Bwana Yesu. Sasa ni halali. Zamani ilikuwa mwenye kuwa na wake zaidi ya mmoja akitengwa, na wala hapati ibada fulani za sakramento, kama Kushiriki katika Chakula cha Bwana.  Leo wanakubaliwa, na inakubaliwa kuwa kuoa mke mmoja si sharia ya Kikristo bali ni mila za Kizungu zilizoingizwa katika dini. Aliyewazindua Wazee wa Kanisa ni Roho Mtakatifu?  Ikiwa ni yeye kwa nini huyo Roho Mtakatifu alinyamaza kimya miaka yote hiyo? Wangapi waliotengwa na Kanisa, wakalaaniwa, na wakachomwa moto hadharani, na baadae watu hao hao baada ya miaka kupita wakaja wakatakaswa na kubarikiwa na kutangazwa na Kanisa lile lile kuwa niWatakatifu? Na wakati huo huo tuone ni Roho Mtakatifu, Mungu, asiyekosea, ndiye amelijaa Kanisa na analiongoza!  Bila ya shaka huyu siye aliyebashiriwa na Yesu. Kanisa la Roma linasema ni haramu kwa padri kuoa. Hivi sasa wapo mapadri si chini ya 80,000 duniani wa Kanisa la Roma ambao wana wake, miongoni mwao 18,000 wako Amerika (U.S.A.). Si ajabu kutokea siku yo yote kuwa Baba Mtakatifu, huku akiongozwa na Roho Mtakatifu, akiona mambo ni ya mno, akatoa amri kuwa sasa ni halali kwa mapadri kuoa bila ya kificho, na bila kuleta nuksani yo yote.

Yesu ametwambia kuwa huyo ajaye hatanena kwa shauri lake mwenyewe. Je, Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu, hunena kwa shauri ya nani?  Mungu hunena anayoyasikia au hunena yake mwenyewe? Ikiwa hunena anayoyasikia, basi anayasikia kwa nani? Kwa Mungu Baba, au kwa Mungu Mwana, na hali tunaambiwa katika Utatu, nafsi zote tatu ni sawa.   Ikiwa yeye ni Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu, pana lipi la ajabu hata ihitajie Yesu kusema kuwa atatoa habari ya mambo yajayo? Hapana ajabu Mungu kuagua yajayo, na hali ni Yeye aliyeyaumba.

Huyo ajaye, Yesu anasema, atamtukuza Yesu. Kwani Mungu Mwana ana haja gani ya kutukuzwa na Mungu Roho?

Hayo yote tukiyazingatia kwa nia safi tutaona kuwa hayamuelekei Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu kama lisemavyo Kanisa, hata chembe.  Je, kama bishara hii haimuelekei Roho Mtakatifu, inamuelekea nani?  Ni mtu gani huyo ambaye alikuja ulimwenguni baada ya kuondoka Yesu, akauhakikisha ulimwengu kwa khabari ya dhambi na hukumu, akauongoza ulimwengu na kuutia kwenye kweli yote, akawa haneni kwa shauri lake wala mapenzi yake bali husema kwa aambiwayo na Mwenyezi Mungu, akatoa khabari ya dhambi na mambo yajayo, akatwachia mafunzo katika Kitabu kisichobadilika milele na mafunzo yake yakakaa nasi milele mpaka mwisho wa dunia, akamtukuza Yesu Kristo?  Katika historia yote hakutokea mtu mwenye kukusanya sifa zote hizo ila Nabii Muhammad tu.

Mtume Muhammad s.a.w. ndiye aliyekuja baada ya Nabii Isa a.s. Yeye peke yake katika Manabii na Mitume wote ndiye aliyesema maneno ya kutimiza ujumbe wote wa Mwenyezi Mungu, ndiye aliyeleta kweli yote.  Kila Nabii aliyetangulia alibashiri kuja mwinginewe baadae. Musa alisema hayo, na Yesu kasema hayo, na wenginewe wote wamesema.  Ila Nabii Muhammad ndiye aliyesema: "Hapana Nabii baada yangu."  Na Mwenyezi Mungu alimwambia karibu ya kufa kwake:
Leo waliokufuru wamekata tamaa katika Dini yenu, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi.  Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.
(Qur'ani) Al Maida 5.3
Mwenye kukamilishiwa Dini na kutimiliziwa Neema, amekamilishiwa na kutimiliziwa kila kitu: ndiyo kweli yote, na hukumu na khabari ya dhambi.  Ni Muhammad ndiye ambaye alikuwa akijuulikana hata na maadui wake kuwa ni msema kweli, wa kuaminiwa, Assaadiq, Al Amin, "Mkweli Muaminifu" na kweli ndiye Roho wa kweli.

Huyo ajaye, Yesu anatwambia, hatanena kwa shauri lake.  Ni Mtume Muhammad, peke yake, ndiye ambaye historia inatwambia kuwa mafunzo yake ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu yote ni maneno ya Mungu, moja kwa moja.  Qur'ani haikutungwa na Muhammad wala na ye yote katika wanaadamu.  Sio kama vitabu vya Biblia, ambavyo vinajuulikana vimeandikwa na watu fulani kama vile Injili ya Mathayo, ya Marko n.k. na Torati ya Musa.  Hii ni Qur'ani ya Mwenyezi Mungu, si ya Muhammad.  Kama isemavyo hiyo Qur'ani:
Arrahman (Mwingi wa Rehema) amefundisha Qur'ani.
 (Qur'ani) Arrahman 55.1-2
Na ilivyobainishwa katika Sura An Najm:
Wala (Muhammad) hasemi kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo uliofunuliwa;  amemfundisha Mwenye nguvu kweli.
 (Qur'ani) Annajm 53.3-5
 Na ilivyosemwa katika Sura An Nisaa:
Hawaizangatii Qur'ani? Na lau kama imetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.
 (Qur'ani) An Nisaa 4.82
Mkristo wa Kiingereza, Dr. John B. Taylor, Mwalimu wa Masomo ya Kiislamu katika Chuo cha Birmingham, ameandika katika kitabu chake: Thinking About Islam (Kuufikiria Uislamu):
"Tumethibitisha ya kuwa Waislamu hawasemi kuwa Muhammad ndiye aliyeandika Qur'ani, lakini kuwa yeye ameipokea na akaisoma.  Kama alivyokuwa Muhammad mwenyewe akishughulika mno kuyaweka safi maandiko (matini) ya Qur'ani, basi hali kadhaalika wale  Waislamu waliokuja baada yake walifanya juhudi kuhifadhi bila ya kukosea ko kote vipande mbali mbali vya Qur'ani.  Miaka miwili tu baada ya kufa Muhammad, kwa kuwa walikufa vitani baadhi ya wale waliokuwa wameihifadhi kwa moyo, sehemu mbali mbali za Qur'ani zilikusanywa...
"Baada ya miaka michache, katika enzi ya Uthman, Khalifa wa tatu kuwatawala Waislamu baada ya Muhammad, ilipitiwa mara ya mwisho kusahihishwa matini ya Qur'ani.  Twaweza kutambua vipi walivyokuwa na hadhari kubwa wale Waislamu wa mwanzo kwa vile hata kukhitalifiana matamshi baina ya sehemu moja ya nchi za Kiislamu na nyengine, hakukuruhusiwa.  Kwa hivyo yale maandishi ya rasmi yakathibitishwa kufuata lafdhi ya Makka, na zile ziliobaki zikateketezwa kwa amri ya Khalifa.  Kwa hivyo tunaweza kuwa na yakini kuwa hii Qur'ani tulio nayo hii leo, kama iwezekanavyo kibinaadamu, ndio ile ile iliyothibitishwa miaka michache tu baada ya kufa Mtume."

Hayo ni maneno ya Mkristo ambaye kazi yake ni kuutafutia ila na nuksani Uislamu.  Qur'ani ni neno la Mwenyezi Mungu lisio na upungufu wo wote kwa sababu ni maneno yake mwenyewe.  Hayo ndiyo makusudio ya Yesu aliposema kuwa huyo Msaidizi ajaye, "hatanena kwa shauri lake mwenyewe."
Yesu kadhaalika ametwambia kuwa Msaidizi atakayekuja atatoa khabari ya mambo yajayo. Kila alilosema Mtume Muhammad s.a.w. kuwa litakuja basi limetokea vile vile alivyosema.  Katika alilosema ni kuwa Warumi baada ya kushindwa na Waajemi wao watakuja shinda mnamo miaka michache na hapo Waislamu watafurahi. Na kweli walishindwa Waajemi mwaka 624 B.K. na ndio mwaka Waislamu walipowashinda makafiri wa Kikureshi katika vita vya Badru.

Mtume alipokubali mkataba wa suluhu pale alipozuiliwa kuingia Makka alisema kuwa Waislamu watakuja kuikomboa Makka karibuni, na hakika hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya miaka miwili, na ikawa ndio ushindi ulioenea Arabuni kote.

Mtume Muhammad alipokuwa akichimba handaki, pamoja na Masahaba zake, kuilinda Madina na maadui, kulimetuka cheche tatu alipokuwa akipiga mtaimbo kulisukua jiwe. Cheche moja ilielekea kusini, Mtume akasema Yaman itasilimu. Cheche ya pili ikaelekea mashariki, na Mtume akasema Iran itasilimu. Cheche ya tatu ilipometukia kaskazini Mtume s.a.w. akasema Sham iliyokuwa chini ya utawala wa Kikristo wa Kirumi itasilimu.   Na zote zikaja kusalimu amri na kusilimu hivyo hivyo kama alivyobashiri, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, katika zama ambazo Warumi walikuwa ndio kama Marekani walivyo sasa, na Waajemi ndio kama Warusi walivyo sasa. Hizo ndizo dola kubwa kabisa, na Muhammad ni bedui mnyonge ambaye ndiye kwanza kachipuka huko jangwani akiwahubiria makafiri wa miji miwili midogo kabisa Makka na Madina.  Na mengi, kabisa, aliyokuwa akiyasema Mtume Muhammad s.a.w. na yote yalikuwa hayaanguki chini.  Nimeyataja hayo ambayo yamo katika vitabu vya historia vilivyoandikwa hata na wasiokuwa Waislamu.

Yesu tena amesema huyo Msaidizi "atanitukuza mimi."  Na kweli Yesu Kristo au Isa Masihi (wamuitavyo Waislamu) alitukanwa na  maadui zake, Mayahudi, kwa kumwambia kuwa ati ni mwana haramu, mzushi, mlaanifu.  Wakidai kuwa uthibitisho wa laana hiyo ni kuwa waliweza kumwua kwa kumtundika msalabani. Taurati ilisema kuwa ye yote anayekufa kwa kutundikwa kwenye mti basi amelaanika, na hayo ndiyo yalikuwa makusudio yao. Hali kadhaalika waliokuwa wakijiona kuwa ni wafuasi wake Yesu watiifu walimvunjia daraja yake kwa kukubali madai ya Mayahudi kwa kuwa alikufa msalabani, na pia kwa kumfanya yeye ni sawa na ile miungu ya bandia ya uwongo sawa na ya akina Mithra, na Apollo, na Osiris ya kipagani, na kwa kumtoa kwenye cheo chake kitukufu ambacho yeye mwenyewe alikuwa akitafakhari nacho kama isemavyo Biblia.  Daima Yesu akitafakhari na kujiita yeye ni mwanaadamu, mtumishi wa Mwenyezi Mungu, ambaye hawezi kusema kitu wala kutenda kitu ila kama anavyoamrishwa na Mungu. Yesu akitafakhari kuwa ni Nabii wa Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, sio kuwa mungu kama miungu iliyojaa katika pande zile kwa zama zile. Hata wafalme madhaalimu wa Kirumi walikuwa wakiitwa miungu.  Wao hao wajiitao Wakristo waliacha kufuata mafundisho yake Yesu na kuyatenda, na badala yake wakafuata mafundisho ya wale wale washirikina ambao Yesu kaja kuwapinga.  Ndio maana akasema:  "Wengi watanambia  siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?  Ndipo nitwaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu."
Ni kwa kupitia Mtume Muhammad, huyo Msaidizi aliyetwambia Yesu kuwa atakuja kumtukuza, ndio tunasoma maneno ya Qur'ani Tukufu:
Enyi watu wa Kitabu (yaani Biblia)!  Msipite kiasi katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli.  Hakika Masihi, Isa bin Maryam, ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake alilompelekea Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake; wala msiseme, "Watatu".  Wacheni!  Itakuwa kheri kwenu.  Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu.  Ametakasika Yeye kuwa na mwana.  Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani;  na Mwenyezi Mungu ni mtegemewa wa kutosha.  Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika waliokurubishwa.  Na watakaouona uvunjifu utumwa wa Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.
(Qur'ani) An Nisaa 4.171-172
Katika Sura Al Imran tunasoma vipi alivyotukuzwa Yesu:
Waliposema Malaika: Ewe Maryam!  Mwenyezi Mungu anakubashiria kwa neno litokalo kwake, jina lake ni Masihi Isa, mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa waliokaribishwa (kwa Mungu). Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.  (Maryam) akasema: Mola wangu!  Vipi nitampata mtoto na hali hajanigusa mwanaadamu ye yote?  Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho; anapohukumu jambo, huliambia: Kuwa, basi huwa.  Na atamfunza Kitabu na Hikima na Taurati na  Injili.  Na ni Mtume kwa wana wa Israili.
(Qur'ani) Al Imran 3.45-49
Na kabla ya aya hizi inasimuliwa vipi alivyoteuliwa mama yake Yesu na kutukuzwa:
Na Malaika waliposema:  Ewe Maryam, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa na kakutukuza kuliko wanawake wa ulimwengu.
 (Qur'ani) Al Imran 3.42


13- BIBLIA NA QUR'ANI

Yesu aliungama kuwa hakuyasema yote aliyoyataka kuyasema, lakini huyo atakaye kuja yeye ndiye ataitimiza kazi.  Mafunzo ya Muhammad juu ya dhambi, juu ya kuhisabiwa haki, na juu ya hukumu yamo katika Qur'ani, kitabu cha namna ya pekee ulimwenguni kwa usafi wake, kutokuwa na migongano yo yote na kuwa hakiwezekani kuigwa mfano wake.  Tangu kilipoteremka kwa Mtume s.a.w. miaka 1400 iliyokwisha pita hakikubadilika hata kwa neno moja, na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, hakitobadilika mpaka Siku ya Kiyama.  Sir William Muir, mtoa kombo maarufu wa Uislamu, akiandika katika kitabu chake The life of Mohamet (Maisha ya Muhammad) amesema:
"Labda hapana kitabu cho chote kinginecho duniani ambacho kwa muda wa karne kumi na mbili kilichobaki na maandiko yake safi namna hii."

Tangu Sir William alipoandika hayo karne mbili nyenginezo zimekwisha biringita na Qur'ani imebaki vile vile safi kama siku alipoipokea Mtume Muhammad s.a.w. kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mintaraf ya Biblia lakini hatuwezi kuona  msimamo  mmoja, kwa sababu kwanza kuwa Biblia si kitabu kimoja, bali ni mkusanyiko wa vitabu vingi vilivyoandikwa na watu mbali mbali, katika zama mbali mbali.  Makanisa yanazozana hata kuwa vitabu vipi vikubaliwe kuwa ndio Biblia, na vipi sivyo, vipi vimeandikwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu na vipi sivyo.  Mara nyingi inatokea katika kitabu kimojawapo hicho hicho kinapingana wenyewe kwa wenyewe, kama tulivyokwisha ona mfano wake katika hadithi ya kutanasari Paulo iliomo katika kitabu cha Matendo ya Mitume.

Hugh Schonfield akiandika katika kitabu chake Those Incredible Christians, anasema:
"Ndani ya jalada za Biblia twaweza kukuta udanganyifu, mageuzo, na uzushi wa kukusudia kama unavyokuta katika vitabu vyenginevyo nje.  Wataalamu wanajua vyema haya;  lakini inapokuwa andiko la ndani ya Biblia si la huyo anayedai kuwa ndiye muandishi kila juhudi inafanywa lisitumiwe neno udanganyifu.  Hali ni hiyo hiyo kwa maneno anayoambiwa Yesu kayasema na yanajuulikana kuwa si kweli. Tunaviita vitabu kama hivyo kuwa ni vya kikundi cha mawazo ya Kipaulo au Kipetro, na maneno yaliyogeuzwa au yaliyozuliwa tunayaita kuwa ni "ya pili"(Secondary). Kama hatukutumia hila itaonekana kuwa Roho Mtakatifu alishirikiana katika udanganyifu.
Ni jambo lililoandikwa na kujuulikana kuwa mpaka ilipokatwa shauri mwishoe vitabu gani vihisabiwe kuwa ni Maandiko Matakatifu baadhi ya vitabu viliomo katika Biblia vilipingwa. Ilitolewa hoja na Wakristo wa kweli kwamba vitabu fulani havikuwa hakika vimeandikwa na hao wanaodaiwa kuwa ni waandishi wake. Pengine jina la mwenye kufanya udanganyifu lilidhukuriwa. Paulo anataja wakati wa uhai wake zilikuwepo barua za uwongo zikienezwa kwa jina lake yeye. Liliokuwa  laonekana  lafaa ni maslaha ya Kanisa tu. Mawazo yasiyokhusiana hata chembe na ukweli yakitumika kuelekeza maandishi na fikra kinyume na hakika ya walivyosema wenyewe watu kadhaa wa kadhaa wenye maana.  Mtindo kama huu ulikuwa ni jambo la kawaida katika kazi ya uenezi hapo kale, na yafaa tuelewe kuwa ilikuwa ni kawaida vile vile miongoni mwa Wakristo wa zamani.  Hivi ndivyo mchezo wa kueneza na kupendekeza ulivyokuwa ukichezwa. Na kwa wale wasio na dhamiri wala haya, wanaoamini kuwa muhimu ni lengo sio njia uitumiayo, mchezo huo unachezwa hata hivi sasa."

Asli ya vitabu vya Biblia haipo na haijuulikani, kwa hivyo ndio tunapata nakala nyingi sana. Inakubaliwa kuwa vitabu hivyo kama vilivyo sasa vimeandikwa na waandishi wanaadamu.  Juu ya hivyo waweza kugundua baadhi ya maneno ambayo yametokana na Mungu asli yake. Lakini jinsi maandishi yalivyochanganyika, na yalivyoongezwa na kupunguzwa hata inakaribia kuwa ni muhali kulitambua lipi la Mungu na lipi la mwanaadamu ambaye alikuwa anawania madhehebu yake fulani au wazo lake maalumu. Qur'ani ni kinyume cha hayo.  Kila neno lake ni la mwenyewe Mwenyezi Mungu. Yote ni maneno yake Mola Mlezi kama alivyofunuliwa kwa ufunuo (Wahyi) Mtume s.a.w., neno kwa neno, na yeye Mtume akiyatamka na wenye kuhifadhi kwa moyo wakihifadhi, na waandishi waaminifu wakiandika.
Mkristo, Dr. John B. Taylor, Mwalimu wa Masomo ya Kiislamu katika Selly Oak Colleges, Birmingham anaandika katika kitabu chake Thinking About Islam:
"Tumekwisha hakikisha kwamba Waislamu hawasemi kuwa Muhammad kaandika Qur'ani, lakini kuwa kaipokea na akaisoma.  Kama alivyokuwa Muhammad mwenyewe alivyoishughulikia matini ya Qur'ani, vile vile Waislamu wa baada yake walichukua kila taabu kuuhifadhi kwa ukamilifu usafi wa vipande vyote vya Qur'ani.  Miaka miwili tu baada ya kufa Muhammad, na kuwa baadhi ya wale waliokuwa wameihifadhi Qur'ani kwa moyo, wakifa vitani, vipande mbali mbali vilikusanywa...
Miaka michache baadaye, katika enzi ya Uthman, Khalifa wa tatu kuwatawala Waislamu baada ya kifo cha Muhammad, matini ilipitiwa tena kusahihishwa.  Twaweza kusema vipi wale Waislamu wa kwanza walivyoshughulikia na kuwa na hamu kwa kuwa hata khitilafu za matamshi ya pande mbali mbali za ulimwengu wa Kiislamu hazikuruhusiwa katika kuisoma Qur'ani; na kwa hivyo matini rasmi ikahakikishwa inayofuata lafdhi ya Makka, na nakala nyenginezo zote ziliteketezwa kwa amri ya Khalifa.  Kwa hivyo tunaweza kuwa na imani ya yakini kuwa hii Quran tuliyo nayo hii leo kama inavyomkinika kibinaadamu ndio ile ile iliyohakikishwa mnamo miaka michache tu baada ya kufa Mtume."

Hayo ni maoni ya mtoa kombo wa Kikristo. Qur'ani ni neno la Mwenyezi Mungu lisio na toa. Hiyo ndiyo maana ya maneno ya Yesu aliponena: "Hatanena kwa shauri lake mwenyewe lakini yote atayoyasikia atanena."


14- KIFO MSALABANI

Mtume Muhammad ndiye aliyekuja kumtukuza Yesu.  Aliyapinga madai ya Mayahudi kumshutumu Maryam na kumshutumu Yesu, na akauhakikisha ulimwengu kuwa Yesu ni mwana wa halali, ni Nabii mtukufu aliyetumwa kwa Wana wa Israili, wala si maluuni kama walivyodai Mayahudi, na wala si mungu wa bandia wa kishirikina, kama walivyomfanya Wakristo bila ya wenyewe kutambua nini walitendalo. Kwa watu wanaoamini kuwa Adam alikuwa hana baba wala mama kwa nini  ikawa ni vigumu kuamini kuwa Yesu alikuwa hana baba? Yohana Mbatizaji anasema:
Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.
Mathayo 3.9
Je, Mungu awezaye kuinua watoto katika mawe, kama alivyomuumba Adam  kutokana na udongo, atashindwa kumzalisha mwanamke bila ya mume? Mtume Muhammad aliwahakikishia maadui wa Kiyahudi kuwa Yesu ndiye Kristo, ndiye Masihi ambaye  amebashiriwa katika maandiko yao wenyewe.  Aliwakanya Mayahudi walipodai kuwa Yesu amelaanika kwa sababu wao waliweza kumuua kwa kumbandika msalabani. Qur'ani imesema:
Hali hawakumuua wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa.  Na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika haya wamo katika shaka nayo.  Wao hawana yakini juu yake, isipokuwa wanafuata dhana tu.  Na hawakumuua kwa yakini.
 (Qur'ani) An Nisaa  4.157
Utafiti wa ilimu za kisasa katika masomo ya Biblia unathibitisha huu ukweli wa Qur'ani. Yajuulikana kuwa zipo Injili nyengine zenye maelezo mbali juu ya mateso ya Masihi yanayokhitalifiana na ya hizi Injili nne zilizokubaliwa na Kanisa. Katika miaka ya karibuni mwangaza  mpya umepatikana kutufahmisha nini khasa zilikuwa imani za wale Wakristo wa mwanzo. Zimepatikana nyaraka za zamani sana ambazo ziko katika jumba la kuhifadhi nyaraka huko Istambul, Uturuki. Aliyegundua ni Dr. Samuel Stern wa Chuo Kikuu cha Oxford.  Wale Wakristo wa kwanza, ambao wakiitwa Wanasoria au Wanazaria (ambayo yanaelekana na jina litumiwalo katika Qur'ani kuwaita Wakristo "Wanasara") hapo awali ndio waliokuwa wengi na wenye nguvu.  Hao Wanasara wakidai kuwa wao wamezalikana na wanafunzi wake Yesu wa kwanza kabisa.  Wakaja wakapambana na Wakristo wamfuatao Mt Paulo.  Hao Wanasara wakimuamini Yesu kuwa ni Nabii mtukufu na mwanaadamu mwema mwenye haki.  Wakamshutumu Paulo kuwa  amezua kwa kutumbukiza mila za Kirumi badala ya mafunzo ya asli ya Yesu, na kumsingizia Yesu kuwa ni Mungu.  Walikataa kusherehekea Krismasi kwa kuwa waliona hiyo ni sikukuu ya kikafiri ya kipagani.

Hadithi ya mateso ya Yesu iliyomo katika hizo nyaraka za kale ni kuwa Yuda aliwakhadaa Mayahudi kwa kuwaletea mtu mwingine badala ya Yesu.  Huyu mtu mwingine alikataa kata-kata mbele ya Hirodi (Mfalme wa Mayahudi) na Pilato (Liwali wa Kirumi) hayo mashtaka kuwa yeye anadai Umasihi.  Kwa mujibu wa hadithi hii ilikuwa Hirodi, wala si Pilato (kama isemavyo Biblia) ndiye aliyechukua maji akanawa mikono kuikosha na dhambi ya damu yake, kudhihirisha kuwa yeye hakumwona na kosa.  Tena Hirodi akamfungia ndani huyo aliyedhaniwa kuwa ni Yesu usiku kucha;  lakini asubuhi yake alishikwa na Mayahudi wakamtesa na mwishoe wakamsalibu.
Hadithi hii ya kusalibiwa walau inatupa sura njema kuliko ile iliomo katika Biblia inayomueleza Yesu kuwa aliyayatika kama asiye na imani ya kutosha, pale alipokuwa msalabani.  Kwani katika Injili ziliomo katika Biblia, yaani zile walizozikubali wakuu wa Kanisa, yasimuliwa kuwa Yesu alilia: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"   Kwa mtu wa hivi hivi, mchache wa imani, aweza kusamehewa akifanya hivyo, lakini hayamuelekei hayo mwenye kuongoza watu, seuze Nabii, seuze Mwana wa Mungu, kama tunavyoambiwa.  Tena Mwana Mungu wenyewe ambaye amekuja makusudi huku duniani kwa kazi hiyo ya kutundikwa msalabani ili waokoke viumbe vyake.

Ikiwa aliyesalibiwa ni Yesu, na Yesu ni Mungu, hadithi hiyo haingii akilini. 
Upton Sinclair anaandika katika kitabu chake A Personal Jesus (Yesu Mtu):
"Waona kuwa wale wanaosimulia hadithi hii hawawezi kukata shauri katika akili zao kuwa Yesu ni Mungu au ni mtu.  Kwa hakika ni tatizo zito mara unapokubali kuwa yamkinika Mwenyezi Mungu awe na sura ya mtu na ateremke duniani.  Je, pale anapokuwa mtu anakuwa Yeye ni mtu au bado ni Mungu?  Na vipi anaweza kusalitiwa, na hali Yeye anajua kuwa anakwenda kusalitiwa?  Masimulizi hayo hayatubainishii waziwazi, kwani kwa msingi wa mambo, yote hayo ni muhali, hayaingii akilini, na hatuwezi kupata jawabu, wala hayumkini kuweza kuyafikiri vilivyo mambo namna hii.
Ikiwa Yesu ni Mungu, basi anajua mbele kila kitu.  Lakini kwa hivyo yote hayo ni upuuzi mtupu kwake;  Yeye anakuwa kama mwenye kucheza mchezo wa kuigiza sinema, na bila ya shaka mchezo kama huo ni wa kumnyon'gonyesha Mwenyezi Mungu Mjuzi wa kila kitu. Je, anafanya haya kufurahisha watoto wadogo?  Ikiwa ni hivyo, kwa nini hawasaidiwi watoto wakue akili zao waweze kuukabili vilivyo ukweli wa mambo?  Upande wa pili, ikiwa yeye ni mtu, na ana akili ya kiutu, basi hajui hakika ya mambo, hana ile raha ya kujua kila kitu, ambayo ni sifa ya Kiungu.  Hizo hadithi za kitoto zatutaka sisi tuamini yote mawili kwa wakati mmoja;  lakini ni wazi kabisa, kuwa mtu hawezi kujua kitu na wakati huo huo akawa anapapasa- papasa kama asiyeona baraabara, kama tutendavyo sisi katika maisha yetu yote."

Kitandawili kinacho watatanisha wasomaji wenye akili zao kama Upton Sinclair kinatatuliwa na vile wale Wanasara wa kale wanavyoeleza kile kisa cha kusalibiwa.  Kwa maelezo yao Yesu anatakasika na tuhuma ya woga na ukosefu wa imani ya rehema ya Mwenyezi Mung, kama alivyoonyesha yule mtu aliyesalibiwa.  Hali kadhaalika tunaweza kuelewa kwa nini wanafunzi wa Yesu aliowateuwa mwenyewe  walivyomkana  na  sote  tukaona  wamefanya  kitendo  cha woga  na  ukhaini.   Wakati  ule  wa   shida  vipi wafuasi wake wote wamkatae?   Wangapi waliokhiari kufa kwa ajili ya waja wa kawaida kama sisi tuliojaa dhambi, itakuwa wanafunzi aliowateuwa mwenyewe Yesu kuwa ndio watakao eneza mafunzo yake wamtupilie mbali kama tambara bovu mara baada ya kuingia matesoni? Na miongoni mwa watu hao awemo Petro ambaye Yesu alimwita mwamba ambaye juu yake atajenga Kanisa lake?  Kudai kuwa yote hayo ni kutimiza bishara ziliomo katika Agano la Kale ni kutumwagia mchanga wa macho.  Lakini walivyoeleza wale Manasara wa mwanzo yanaingia sana akilini.  Ni kweli yule aliyekamatwa na kubandikwa msalabani akayayatika kama mtu asiye na imani si Yesu, siye Bwana wao, siye mwongozi wao, siye Mwalimu wao.  Ni kweli hawamjui mtu yule.  Yule mtu waliyemsaliti, waliyemkataa, waliyemwacha ateseke na auliwe bila ya kunyanyua kidole kumtetea, wala kutoa kauli kumsemea wala dua kumwombea, ni kweli hawamjui.

Injili ya Barnaba ambayo Kanisa limeikataa inaeleza kuwa yule aliyesalibiwa ni Yuda; na madhehebu ya Kikristo ya kale iitwayo Basilidoni ikiamini kuwa ni Simoni Mkirene ndiye aliyesalibiwa, si Yesu.  Kwa mujibu wa Injili tatu za mwanzo, yaani Mathayo, Marko na Luka, ni huyo Simoni ndiye aliyebeba msalaba. Ni Injili ya Yohana tu ndiyo inayotwambia kwamba ni Yesu mwenyewe aliyebeba msalaba wake. Jambo hili lafaa kuzingatiwa na kutiwa maanani.

Wataalamu wengine, wanaotegemeza utafiti wao juu ya hizi hizi Injili nne zilizokubaliwa na Kanisa na kutiwa katika Biblia, wana mawazo mengine juu ya hichi kisa cha kusalibiwa. 
Mmoja wao ni Dr. Hugh Schonfield, ambaye ametoa maoni yake katika kitabu chake chenye kuzua majadiliano mengi.  Kitabu hicho kinaitwa The Passover Plot (Njama ya Pasaka).  Yeye anadai kuwa ni Yesu kweli aliyetundikwa msalabani, lakini hakufa hapo msalabani;  alionekana tu kama kwamba kafa, kwa kunywa dawa ya kuzimia inayoelezwa katika Injili ya Mathayo kuwa ni siki.
Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.  Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha;  na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.  Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena  kwa nguvu, akaitoa roho yake.
Mathayo 27.45-50
Hayo ni maelezo ya Injili ya Mathayo. Lakini Schonfield anadai ya kuwa hiyo ilikuwa ni hila tu kumwokoa Yesu asife msalabani.  Alipewa hiyo dawa ili aonekane kama aliyekufa.  Kwa mujibu wa Injili Yesu alibakia hapo msalabani kwa muda wa saa tatu tu, ilhali ilikuwa ni ada mtu kubaki ananing'inia msalabani kwa siku kadhaa wa kadhaa yupo baina ya uhai na mauti akisononeka. Tena kwa kufuata mpango maalumu uliopangwa, alitokea mfuasi wake Yesu, tajiri mmoja aitwaye Yusufu wa Arimathaya akamwendea Liwali wa Kirumi, Pilato, akamwomba ampe yeye maiti akamzike. Akapewa.
Mtaalamu wa ilimu ya binaadamu (Anthropology) Michael J. Harner wa Chuo Kikuu cha California katika kuthibitisha hayo alisema kuwa ni kweli ilikuwa ikifanywa mvinyo kutokana na mmea wa tunguje mwitu ambayo ikitumiwa kumfanya mtu kuzimia na kuonekana kama kafa ili kumwokoa na kifo cha kusononeka msalabani. Huyo Yusufu tena alimpeleka huyo aliyeonekana kama maiti kwenye pango alilolichonga kama chumba kwenye bustani yake liwe ati ni kaburi. Na jiwe kubwa likawekwa mlangoni. Hakuzikwa katika kaburi liliochimbwa chini kwenye ardhi na kufukiwa kwa udongo.


15- HAWAKUMUUA

Ukitaka hakika ni kweli kuwa mtu ye yote anayesoma hizi hizi Injili ziliomo katika Biblia kwa uangalifu ataona ushahidi wa nguvu kuwa huyo aliyetundikwa msalabani hakufa hapo msalabani, bali alionekana tu kama amekufa.  Katika Injili hizo hizo upo ushahidi mzito wa kuonyesha kuwa yamkini sana kuwa huyo aliyetundikwa msalabani hakuwa Yesu Kristo kabisa, juu ya kuwa waandishi wa Injili walikuwa wakiamini kuwa ndiye Yesu.  Hebu natuuchungue ushahidi huo.

Ni wazi kuwa Yesu wakati ule hakuwa mtu maarufu katika mji wa Yerusalemu.  Alikuwa ni mgeni kwa wale waliokuwa wakimsaka.  Yeye alikuwa mshamba, ametoka huko Galilaya.  Tangu kuanza kuhubiri ni kiasi ya miaka miwili mitatu tu, naye akitanga tanga huku na huku bila ya kutulia, hata hakuwa na pahala pa kuweka kichwa chini.
(Mathayo 8.20). Mnamo wakati huo hakupata kwenda Yerusalemu isipokuwa mara chache tu. Marko anasema alikwenda mara moja, na Yohana anasema mara nne.  Jinsi ya kuwa hajuulikani vyema hata ikalazimu Yuda amtambulishe kwa kumbusu; alisema: "Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni." (Mathayo 26.48). The Interpreter's Bible kutafuta kijisibabu kwa huko kumuashiria kwa kumbusa inasema: "Yesu angejuulikana bila ya ishara, lakini wale waliokuja kumkamata hawakutaka kubahatisha kwa sababu makosa yaweza kutendeka kwa wepesi wakati wa usiku, na khasa pangetokea pata-shika."  Vyo vyote vile iwavyo, ikiwa ni kwa ugeni, ikiwa ni kwa giza la usiku, au ikiwa kwa ghasia na fujo lililokuwapo, ni jambo lilioelekea sana kumkosea Yesu akakamatwa mtu mwingine. Wafuasi wake wote walimkataa, hata Petro naye ambaye alikuwa karibu mno na Yesu katika wanafunzi wake wote, naye pia alisema: "Simjui mtu huyu". (Mathayo 26.74). Basi je, tuukatae na kuutenga kando ushahidi wa wanafunzi wake wote wanaoitwa Watakatifu tuukubali wa khaini, msaliti mmoja, Yuda?  Tena hata yeye hakuutoa ushahidi wake mahkamani, baada ya kuapishwa, bali huko huko kwenye vurugu kizani, tena ni kwa ishara tu ya kumbusu, ambayo tunaambiwa na waandikaji kwamba walikubaliana baina yake Yuda na askari wa Kirumi faraghani, ambako bila ya shaka yo yote hao waandikaji au waliowasimulia hawakuwapo. Hayo ni mambo ya dhana tu. Kuambiwa tena kuwa hayo nayo yalikuwa ni kutimiza bishara za Agano la Kale, au zake mwenyewe Yesu, ni hadi ya kuilazimisha imani ikubali lisilokubaliwa na akili.

Tena hebu tuzichungue jawabu alizozitoa mshtakiwa huko mahkamani. Hadi yake tunaweza kusema kuwa hizo jawabu ni za ubabaishi.  Injili tatu za mwanzo, nazo ndizo zenye kueleza maisha ya Yesu, zimeshindwa kutoa ushahidi hata mmoja kuthibitisha kuwa ni nani khasa huyo mshtakiwa.  Injili ya Luka inasimulia kuwa alipoulizwa barazani: "Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie."

Akawaambia: "Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa."
Na alipoambiwa: "Basi wewe ndiwe Mwana wa Mungu?"
Akawaambia: "Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye."

Maana ya kauli hiyo sio maana yake kukubali yasemwayo, bali ni kukanya na kumsukumia jukumu yule amuulizae na  kumtuhumu kwa hayo - yeye hakimu pamoja na wote waliozua hayo mashtaka. Na vyo vyote alisemalo hasadikiwi, kwani waliomkamata wamesha kata shauri kuwa yeye ndiye Yesu Kristo, na hali siye. Basi hapana haja ya kusema lo lote.

Katika Injili ya Marko tunasoma: Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?

Akajibu, akamwambia: "Wewe wasema." Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema:
"Hujibu neno?  Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!" Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.

Kama alivyojibu kuwa yeye si Mfalme wa Wayahudi, hali kadhaalika si Mwana wa Mungu, wala si Kristo.  Kwa suala zote tatu hizo mshtakiwa anasema kuwa hayo wanayasema wale wanaomshtaki, si yeye.

Kadhaalika Injili ya Mathayo inatwambia:  Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema,"Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?"
Yesu akamwambia: "Wewe wasema."

Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.  Ndipo Pilato akamwambia: "Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?" asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Na sote lazima tustaajabu. Ikiwa yeye ni Yesu, Kristo, Mwana wa Mungu, kama ilivyodaiwa kuwa anadai, kwa nini hakubali? Hapo mahkamani sipo khasa pa kueneza ujumbe wake?

Zingatia vyema kuwa hadithi hizi ziliandikwa miaka mingi baada ya kutokea hayo mambo, tena zimeandikwa na watu wenye kuamini kabisa kuwa huyo aliyekamatwa na kusalibiwa ni kweli Yesu Kristo, mwana wa Maryam.  Juu ya hivyo hata wao hawakuweza kuleta ushahidi wo wote wa kweli au wa kubuni usipokuwa ule wa Yuda, msaliti.  Huyo mshtakiwa hakukiri hata mara moja kuwa yeye ndiye Yesu anayetuhumiwa. Na wanafunzi wake nao hawakumtambua wala hawakukiri kuwa wao wanamjua, bali walikataa kwa nguvu, na wakamkimbia.

Tukizingatia haya kwa usafi wa nia na kwa kutumia akili zetu bila ya kugubikwa na mawazo na imani tulizozoeshwa tangu utotoni, na pia tukatia maanani yale tuliyokwisha yasimulia yaliyomo katika Injili nyenginezo zisiokubaliwa na Kanisa, pamoja na nyaraka za kale zilizogundulikana karibuni zinazotufahamisha nini ilikuwa imani ya Wakristo wa asli ya kwamba Yesu hakufa msalabani, ukweli wa Qur'ani unathibiti kwa uwazi kabisa:
 Na kwa kusema kwao (Mayahudi): Sisi tumemuua Masihi Isa mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala hawkumuua wala hakumsalibu, bali walifananishiwa.  Na kwa hakika wale waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo.  Wao hawana ujuzi juu yake, isipokuwa wanafuata dhana tu. Na hawakumuua kwa yakini.
 (Qur'ani) An Nisaa 4.157
Wataalamu wa Biblia wa nchi za magharibi wa sasa baada ya uchunguzi wanakubali ukweli huu wa Qur'ani.  Na Qur'ani iliteremshwa kwa mtu asiyejua kusoma wala kuandika miaka elfu moja na mia nne iliyopita.


16- MWILI NA DAMU YA YESU

Yesu alipobashiri kuja kwa huyo "Msaidizi" ambaye atauhakikisha ulimwengu kwa khabari ya dhambi kwa sababu watu walikuwa hawamuamini yeye, alikuwa anasema kweli tupu.  Kwani yeye alikuwa kawajia Waisraili ambao walikuwa wakishikilia sana kufuata madhaahiri ya sharia na wakapuuza undani wake.  Wakiitenda sharia ila imani yao ilikuwa chache, na uchamngu wao ulikuwa dhaifu. Jitahada yake ilikuwa bure kuwahimiza kuwa yapasa vitendo vyao vinavyoonekana vichanganyike na imani ya roho.   Alijaribu kuwafanya wafahamu khitilafu iliopo baina ya mikazo inayoletwa na wanaadamu na sharia za milele za Mwenyezi Mungu. Aliwaambia:
Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.
Marko 7.9
Yesu hakuanzisha sharia yo yote mpya.  Kazi yake ilikuwa kuitimiza sharia ya Musa kwa uchamngu.  Lakini baada yake ulizuka mzozano juu ya tafsiri ya sharia. Kikundi kimoja miongoni mwa wafuasi wake kiliona kuwa maadamu yeye ni Muisraili aliyefuata sharia na hataki kutengua sharia hata nukta moja, basi ni waajibu kwa wafuasi wake wote wafuate sharia kwa kila neno, kama yeye, hata katika mambo ya kutahiri, na kuacha kula nyama za haramu kama nguruwe na visivyochinjwa kisharia na damu, na kuitukuza Jumaamosi kuwa ni siku ya Sabato. Hawa ndio wanaitwa Wakristo wa Kiyahudi.  Kikundi kingine, na mkubwa wao ni Paulo, kilichoathirika na upagani wa Kizungu, kiliona uzito kujifunga na sharia za Musa. Kilitoa hoja kuwa maadamu Yesu hakutoa sharia mwenyewe basi wao ni huru, kwani Yesu kwa kufa msalabani damu yake imekwisha wakomboa wanaomuamini na mikazo ya sharia. Sharia ni laana, na Yesu kwa kufa kifo cha laana msalabani amechukua yeye dhambi za watu, na vile vile ameondoa laana ya sharia. Liliokuwa la lazima si matendo ya sharia bali kuamini tu kuwa Yesu amekufa msalabani kwa ajili yao. Huo ni uokofu wa kutosha. Ili imani hii iingie na isaki katika akili na nyoyo za waumini ikazuliwa hiyo ibada iitwayo Ekaristi, au Chakula cha Bwana, Ushiriki au Misa takatifu. Katika ibada hii ya kuonyesha neema ya dhaahiri na ya ndani, au ya kiroho, huliwa kidogo mkate uliobarikiwa, na hunywewa mvinyo kidogo iliyobarikiwa, kwa kuwa ni mwili na damu ya Yesu. Injiili inasema:
Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle;  huu ndio mwili wangu.  Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.
Mathayo 26.26-28
Upton Sinclair katika kitabu chake A Personal Jesus anatoa maoni yake juu ya maneno hayo ya Injili tuliyoyanukulu:
"Kutokana na hayo umetokea mtindo uitwao Ekaristi, Ushiriki, Misa:  ibada ya taadhima isiyokadirika.  Badala ya kumtoa mhanga mwana kondoo asiyejifaa kitu, ni mwili wa Yesu uliotolewa mhanga msalabani, na damu yake iliyomwagwa, na kwa mageuzo ya ajabu mkate na mvinyo ikawa ni mwili wake na damu yake, na wewe unakaa kwa unyenyekevu ukila na ukinywa au unamuacha padri akulie na akunywie.  Mamilioni na mamilioni ya maneno yametumiwa katika kuhojiana, na maelfu ya vitabu vimepigwa chapa juu ya suala hili; vipi mageuzo hayo yanatokea...Wakatoliki wanaamini hayo wanayoyaita Mahudhurio ya Hakika (Real Presence); yaani, wanasema kuwa ule mkate na ile mvinyo hakika inakuwa ni mwili na damu, ijapokuwa sura yao inabaki vile vile kama mkate na mvinyo.  Wote Wakatoliki wachamngu huenda kila wiki waone kitendo hichi kikitendwa na padri, na tena hapo ndio wanajua kuwa roho zimesalimika na moto wa jahannam.  Mimi sitaki kumuudhi mtu ye yote, na kwa hivyo najitosheleza nafsi yangu kwa kusema kuwa mimi siamini kuwa Yesu alikuwa akishughulikia mtindo huu."

Marcello Craveri anasema juu ya jambo hili hili katika kitabu chake The Life of Jesus (Maisha ya Yesu):
"Ikiwa tunaamini kuwa Yesu ni mwanaadamu, basi hichi Chakula cha Bwana (Misa au Ekaristi) kinakuwa na sifa ya ibada ya wala-watu; ikiwa tumfanye kuwa ni Mwana wa Mungu, ile fikra safi na tukufu ya Mwenyezi Mungu ambayo mwenyewe Yesu akiishika, inaporomoka chini na kuwa ni itikadi ya mungu dhaalimu asiye na huruma anayetaka daima dawamu Mwanawe mteule atolewe kikoa."

Mtaalamu huyo wa Kitaliana ameendelea kueleza katika kitabu chake kuwa mtindo huu kwa hakika ameuzua Paulo kufuata mitindo ya kikafiri (kipagani) iliyokuwa imeenea wakati ule katika pande zile.  Anaendelea kusema:
"Maandishi ya Injili yakajazwa kwa kuongezwa na Paulo, ambaye alibatilisha ukweli wote wa historia (taarikh) kwa ajili ya kufuata maelekeo ya imani yake, na huku akitangaza bila ya kuona haya wala aibu kuwa kila kitu amekipata moja kwa moja kutokana na Yesu mwenyewe.  Ni yeye ndiye aliyemfanya Yesu aseme baada ya kukata mkate: Chukueni, kuleni;  huu ni mwili wangu, uliovunjwa kwa ajili yenu. Na huku akiibariki mvinyo: 'Kikombe hichi ndio agano jipya katika damu yangu.'"

Ushahidi wa kuwa hadithi hiyo, yaani kuwa Yesu kawataka wanafunzi wake wale mkate na mvinyo kuwa ndio mwili wake na damu yake, imezuliwa na kubuniwa na Paulo, umo katika barua yake mwenyewe Paulo aliyowaandikia Wakorintho:
Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliyotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu;  fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.  Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu;  fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.  Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
1 Wakorintho 11.23-26
Marcello Craveri anatwambia:
"Paulo, kwa kuwa aliathirika na dini za mazingaombwe zilizoenea katika jamii za Kigiriki na Kiasia alimoishi yeye, alimchanganya Yesu pamoja na vile vijiungu vya bandia viokozi kama Orfia, Dionisa, Attis n.k. - vilivyokuwa vikiabudiwa na mila hizo.Vijiungu hivi pia viliteseka na vikafa ili viwape watu fursa ya roho zao kufikilia rehema ya kiungu. Waumini waliingizwa katika dini hizo kwa kupitia katakismu (yaani kufahamishwa maana ya tambiko), kufunga, na kusafishwa.  Hapo tena hukubaliwa kuwa ni wanachama wa kaumu ya dini na hupata hifadhi ya mungu. Huweza kuungana au kushirikiana kiroho na huyo mungu mwenyewe kwa kula nyama ya mnyama mtakatifu ambaye ndiye ishara yake.  Nyama na damu ya mnyama yule huingiza sifa na khulka ya mungu katika roho ya mwenye kula nyama na kunywa damu. Kadhaalika Paulo aliwaza mawazo yale ya nguvu za uchawi zinazotokana na ule mkate wa Ekaristi kama wale mapagani makafiri walivyokuwa wakiwaza katika wale wanyama wao wa muhanga."

Yapasa tukumbuke kuwa Mt Paulo hakuwa mwanafunzi wa Yesu wakati wa uhai wake, wala hakuweza kudai kuwa waliwahi kukutana ila  katika hiyo "njozi" aliyodai kaiona alipokuwa njiani kwenda Dameski, na Yesu hayupo tena. Madai yake yote anayategemeza juu ya "ufunuo" huo alioupata.  Kisa hicho kinasimuliwa mara tatu katika kitabu cha Matendo ya Mitume kiliomo katika Biblia, na kila mara hadithi hiyo inakhtialifiana na nyengine, kama tulivyokwisha ona.



17- MAONI YALIYOKAA SAWA

Alipokuja Nabii Muhammad s.a.w. mambo yote yaliwekwa sawa. Mafunzo safi ya Musa yalirejeshwa pahala pake, na dini ya Yesu ilisafishwa na kutolewa takataka za Upaulo. Zote dini hizo mbili, Uyahudi na Ukristo, bali dini zote zilizogeuka zilirejeshwa kwenye umbo lao  la asli lisiloharibika, umbo la Uislamu. Muhammad s.a.w. alifunza kwa uwazi kabisa juu ya dhambi, na akalegeza mikazo iliyokuwa imewabana Mayahudi. Alifahamisha kuwa baadhi  ya mikazo hiyo ni matokeo ya inda yao wenyewe na uasi wao, na mingine ilizuliwa na makuhani wao tu ili wazidi kuwakandamiza na kuwaendesha watakavyo wafuasi wao.   Upande mwingine hakuwaacha watu wakitangatanga gizani bila ya uwongozi, wala hakuwaacha watu watende horera watakavyo au kuwaambia watazame maandishi ya kale ambayo jinsi yalivyo chafuliwa kwa maongezo na mabadiliko hata mtu hawezi kutambua lipi la kweli na lipi la uwongo, lipi la Mungu na lipi la matamanio ya binaadamu.  Kuachia mambo hivyo huzidisha zogo penye fujo. La!  Muhammad alikuja na Qur'ani, kitabu cha kusomwa, au kwa jina jingine, Furqan, yaani Kitabu cha kufarikisha, yaani kupambanua, baina ya haki na baatili, baina ya kweli na uwongo.  Alileta Sharia, Sharia ya Kweli ya Mwenyezi Mungu, iliyomkomboa binaadamu kutokana na minyororo iliyowatatiza Mayahudi, lakini haikuacha mambo ovyo kila mtu atende atakavyo kama alivyofanya Paulo kuivunja sharia kabisa. Huo ni utumwa mwingine ambao ni mbaya zaidi, kwa kuwa ni utumwa wa ubongo na  roho, kuuwachilia mwili utende upendalo na kuifunga akili isifikiri na roho isinawirike.  Sharia ya Qur'ani ni sharia ya kati na kati. Dini ya Kiislamu ni ya kati na kati. Si ya kulia wala kushoto lakini ya kuongoza mbele moja kwa moja kumfikilia Mwenyezi Mungu. Anasema Mola Mlezi katika Qur'ani:
Adhabu yangu nitamfikishia nimtakaye, na rehema yangu imekienea kila kitu.  Lakini nitawaandikia wale wanaomcha Mungu, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini Aya zetu, ambao wanamfuata Mtume, Nabii asiyejua kusoma na kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.  Basi wale waliomuamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.
(Qur'ani) Al Aaraf 7.156-57
Huyu ndiye Roho wa Kweli aliyetolewa bishara yake na Yesu kama ilivyo katika Injili ya Yohana sura ya 16.  Ni yeye ambaye amesimuliwa kuwa "akisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu...huyo roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote."  Ni huyu Muhammad s.a.w. ndiye aliyeambiwa Nabii Musa a.s. na Mwenyezi Mungu katika Kumbukumbu la torati sura ya 18:
 Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe.
Kumbukumbu 18.18
Mafunzo ya Nabii Muhammad ndiyo yale ya Nabii Isa na ndio yale ya Nabii Musa na Nabii Ibrahim na kila Nabii aliyetokana na Mwenyezi Mungu.  Msingi wao ni mmoja.  Sharia zaweza kukhitilafiana kwa mujibu wa zama na hali, ama Imani na mambo ya kiroho na wema na ubaya hayo ni mamoja.  Qur'ani imetilia nguvu sana juu ya Imani, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu, Imani kamili ya fadhila na neema ya Mwenyezi Mungu.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu asingelitakasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja.
(Qur'ani) An Nur 24.21
Lakini kumuamini Mwenyezi Mungu ni kutenda yale ayapendayo. Kama asemavyo Jalaludin Rumi, mshairi sufi mkubwa:  "Ukimuamini Mwenyezi Mungu muamini kwa vitendo vyako!  Atika mbegu, tena ndio mtegemee Mwenyezi Mungu!" Mswahili akichukua jembe kwenda kondeni husema: "Nenda omba Mungu."

Alikuwapo mtu mmoja akamuuliza Mtume s.a.w. amwachilie ngamia wake naye akimtegemea Mwenyezi Mungu?  Mtume alimjibu: "Mfunge ngamia wako, ukisha ndio mtegemee Mwenyezi Mungu."

Qur'ani imejaa maneno kama haya: "Wanaoamini wakatenda mema". Na Yesu naye amefunza haya haya kama yaliyomo katika maneno yake mwenyewe, sio ya Paulo.  Na waraka wa Yakobo, nduguye Yesu, unasema hivyo hivyo.



18- MISINGI YA KIPAGANI

Kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad s.a.w. Imani sio maana yake kuamini mwengineo atakubebea mzigo wako.  Hapana awezae kukuokoa, ila kwa kuwa anakuongoza njia ya sawa tu.  Uokofu uko mikononi mwako mwenyewe.  Qur'ani inasema:
Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.
(Qur'ani) Az Zumar 39.7
Basi anayefanya chembe ya wema atauona, na anayefanya chembe ya uovu atauona.
(Qur'ani) Az Zilzaal 99.7-8
Si padri, wala kuhani, wala shekhe, wala Yesu, wala Muhammad, atakayetubebea dhambi zetu au kutufutia dhambi zetu.  Imani kama hiyo ni imani ya uvivu na kujidanganya mwenyewe, kuamini kuwa mateso au kifo cha mtu mwengine kinatosha kutufutia dhambi zetu sisi.  Yesu hakufundisha hayo.  Tumekwisha ona ushahidi wa kutosha katika Biblia kuwa imani hiyo sio aliyofunza Yesu, wala Manabii wote waliotangulia.  Tumenukulu ushahidi kutoka Yeremia 31.29-30, kutoka Ezekieli 18.19-20, kutoka Yohana 9.1-3 na kutoka Mathayo 18.3.  Mafunzo ya imani ya kuwa Yesu kachukua dhambi za watu kwa kifo chake msalabani kayazua Paulo kwa kuyanukulu kutokana na imani za kikafiri za kipagani zilizoenea katika Mashariki ya Kati na Ulaya Mashariki tangu karne za kabla ya kuja Yesu.  Attis katika Frigia, Adonis katika Syria, Dionisa au Bakkus katika Ugiriki, Mithra katika Iran na Osiris na Horus katika Misri, walikuwa miungu ya uwongo, miungu ya bandia, iliyokuwa na visa vile vile vya uokozi, na kufutia dhambi kwa kufa kwao na kufufuka kwao kutokana wafu kama inavyosimuliwa yaliyompitia Yesu. Kwa mfano Attis, mungu wa kipagani wa Frigia, anaambiwa alizaliwa na bikra Nana, na akiitwa Mwana wa Pekee na Mwokozi.  Aliuliwa chini ya mti wa msonobari kwa kumwagwa damu yake, na damu  yake ikiaminiwa kuwa ilitia rutba katika ardhi na ikaleta maisha mapya kwa wanaadamu.  Kifo chake kilitokea taarikh 24 mwezi wa Machi. akafufuka kutoka wafu, na kifo chake na kufufuka kwake kulisherehekewa na wafuasi wake kila mwaka.

Adonis, mungu bandia wa Syria, vile vile alizaliwa na bikra. Yeye pia aliteswa na akafa kwa kuokoa wanaadamu, na akafufuka kutoka wafu katika nyakati zile zile za Pasaka.

Dionisa au Bakkus wa Ugiriki akiitwa Mwana wa Pekee wa mungu Jupita.  Alizaliwa na mama bikra 25 Desemba!  Kwa wafuasi wake alikuwa ni Mwokozi.  Alijiita mwenyewe Alfa na Omega, yaani wa mwanzo na wa mwisho.  Kisa cha mateso yake kikisherehekewa kila mwaka, na mateso yenyewe ni kufa, kuteremka jahannam na kufufuka.

Osiris, mungu bandia wa Misri, naye alizaliwa 29 Desemba na mama aliyekuwa bikra.  Alisalitiwa na mtu mmoja aitwae Tifeni na akauliwa.  Alizikwa na akabaki katika jahannam muda wa siku mbili au tatu na masiku yake, na tena akafufuka kutoka wafu.

Mithra alikuwa mungu-jua wa Waajemi (Wairani).  Pia naye kazaliwa na bikra 25 Desemba. Krismasi na Pasaka ndio sikukuu zao muhimu kabisa, kama zilivyokuwa za dini nyenginezo za kikafiri, kipagani. Hawa Wamithra walikuwa na tambiko (sakramenti) saba; muhimu kabisa katika hizo ni ubatizo, na Ekaristi (Misa), ambapo hao washirika hula mkate na hunywa mvinyo, kwa kuwa ndio wanakula nyama ya Mithra, na kunywa damu yake.

Mwenye kujua ukweli huu lazima ajiulize nafsi yake kuwa Mtakatifu Paulo na wakuu wa Kanisa wenginewe wamepata tambiko za kufutiwa dhambi kwa damu ya Yesu, kuzaliwa kwake mwisho wa Desemba, kufa kwake na kufufuka kwake, na Pasaka, na Misa, na Utatu, kutokana na yeye Bwana Yesu, au kutokana na mila za kikafiri zilizokuwapo kabla ya Yesu huko Ugiriki, Misri, Syria na Iran?

Leo Tolstoi, Mkristo wa kweli na muaminifu wa Kirusi, ameandika katika risala yake aliyoita An Appeal to the Clergy (Ombi kwa Mapadri):
"Ikiwa Utatu, na kuchukua mimba bila ya toa (Immaculate Conception), na kuokoka binaadamu kwa damu ya Yesu, yamkinika, basi tena hapo kila kitu chamkinika - na hapana haja tena ya kutumia akili."



19- BISHARA YA YESU YATIMIA

Ikiwa Yesu hakutuachia uongozi wa kutosha katika mambo ya dhambi na kuhisabiwa haki, na hukumu, basi ni kwa sababu madhubuti, ambazo yeye mwenyewe amezitaja. (Tazama Injili ya Yohana 16.5-14 kama tulivyokwisha nukulu.)  Tena, lakini alimuelezea hivi huyo ambaye atakuja:  "Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu...atawaongoza awatie kwenye kweli yote."Yesu alisema kuwa huyo ajaye ataufundisha ulimwengu khabari ya hukumu.  Yeye mwenyewe hakuweza kuweka mfano wa uhakimu kwa kuwa maisha yake alikuwa mkimbizi anakimbia kuhukumiwa. Historia haitwambii kuwa alikuwapo mwongozi ye yote wa dini baada ya Masihi aliyeshika uhakimu isipokuwa Muhammad.  Muhammad amepitia kila namna ya maisha.  Alikuwa mchunga kondoo, mwananchi wa kawaida, mume, baba, mpigania uhuru, mtawala, mtunga sharia, mwana siasa, hakimu, walii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, tena ndiye wa mwisho wa wote.  Amebeba ujumbe uliotoka moja kwa moja kutokana na Mwenyezi Mungu.  Muhammad akihukumu, lakini hukumu yake ilikuwa imelainishwa na rehema, kama inavyoelekea kwa mtu anayehukumu kwa nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu.  Maisha yake ya kila namna ni ruwaza ya kutosha kwetu sisi sote, kuiga kama tulivyojaaliwa katika maisha yetu.  Yeye alifunza kwa maneno na vitendo. Hakuwa mtu aliyejitenga na ulimwengu akasema maneno matamu lakini maneno yenyewe hayatendeki.  Alikuwa mtu wa vitendo, mtu wa kidunia, na wakati huo huo kwa upande wa kiroho alikuwa na khulka bora kabisa hata mwenyewe Aliyemuumba hakuweza ila kumsifu kwa kumwambia:
Na hakika wewe una tabia tukufu.
(Qur'ani) Al Qalam 68.4
Mara moja Bibi Aisha, mkewe, aliulizwa (na nani amjuaye mtu kuliko mkewe?) nini tabia ya Mtume, alijibu kwa mkato: "Khulka yake ni Qur'ani!"  Hapana sifa kubwa kuliko hii. Mtu huyu aliishi ile dini yake.  Maadui zake wanakubali kuwa hapana kitabu kinachokubaliana na mtu, kuliko Qur'ani inavyokubaliana na maisha ya Mtume Muhammad s.a.w.   Amri zilizotokana na Mungu wake, ndio maisha yake.  Si ajabu basi Yesu kusema kuwa Muhammad atauhakikisha ulimwengu kwa khabari ya haki.

Huyo mtu aliyebashiriwa na Yesu kuwa atakuja ni kuwa atakuwa Mtume wa ulimwengu mzima, kwani zama za Mitume ya kabila fulani na kondoo fulani waliopotea umekwisha.  Huyo ajaye ni Mtume wa watu wote, wa kabila zote, na wa mambo yote.  Huyo ni wa kuuhakikisha ulimwengu, na wa kufunua kweli yote. Hali kadhaalika Mwenyezi Mungu anamwambia Muhammad:
Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe Mbashiri na Mwonyaji.
(Qur'ani) Saba 34.28
Na sisi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.
(Qur'ani) Al Anbiyaa 21.107
 Yesu alisema ana mengi ya kusema, lakini watu wake hawakuwa na uwezo wa kuyachukua wakati ule.  Wataongozwa kwenye kweli yote na huyo ajaye, Roho wa Kweli, ambaye itakuwa fakhari yake kuutangazia ulimwengu baada ya kutimiza ujumbe wake: "Hapana Nabii baada yangu."  Ni yeye huyo ambaye ameitwa na Mwenyezi Mungu: "Khaatamun Nabiyyiina, Mwisho wa Manabii, Muhuri wa Manabii. Waraka ukisha tiwa muhuri hapana ruhusa kuongeza kitu juu yake. Chupa ikitiwa Khaatam, (Seal), ndio imezibwa, huwezi kuongeza kitu tena. Ukiongeza unaghishi, unafanya khadaa.  Qur'ani na mwenendo wa Mtume Muhammad upo kutuongoza sisi katika mambo yetu yote mpaka Siku ya Mwisho.  Hakujuidai  ila lilio haki yake.  Alikataa katakata kufanywa mungu wa bandia.  Daima akisema:  "Mimi ni mwanaadamu tu."  Mwenyezi Mungu alimuamuru aseme:
Sema:  Bila shaka mimi ni mwanaadamu kama nyinyi.  Ninaletewa Ufunuo (Wahyi) ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu.  Basi anayetaraji kukutana na Mola wake Mlezi naatende vitendo vyema, wala asimishirikishe ye yote katika ibada ya Mola wake Mlezi.
(Qur'ani) Al Kahf 18.110
Kazi yake, kama ilivyokuwa kazi ya Yesu, ilikuwa kufanya apendavyo Yeye Mwenyezi Mungu aliyemtuma.  Muhammad hakudai kuwa yeye ni muanzishi wa dini mpya.  Bali aliendeleza na akatimiza dini aliyokuja nayo Ibrahim, Musa, Isa (Yesu), na Manaabii wote waliotoka kwa Mwenyezi Mungu.  Wote hao wakitenda mapenzi ya Mwenyezi Mungu.  Na huo ndio Uislamu.  Neno "Islam" lina maana ya Usalama, na maana ya kujisalimu kwa Mwenyezi Mungu, utende lile limpendezalo Mwenyezi Mungu, yaani kutenda mapenzi ya Mungu, kama asemavyo Yesu.  Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani kuwa hapana kaumu ila walipelekewa Nabii.  Lakini Mtume Muhammad kwa kuwa ni wa ulimwengu mzima, kama alivyobashiri Yesu, na kwa kuwa ni wa mwisho, basi ni mwenye kuthibitisha ukweli wa ujumbe wote uliotoka kwa Mwenyezi Mungu, na mwenye kuondoa makosa yaliyopachikwa na wanaadamu katika dini ya Mwenyezi Mungu.  Kwa kuwa wakati umefika wa kukusanya ulimwengu mzima uwe na Imani moja, na kuelekea kumoja, ndio akaja Mtume Muhammad, kama ni Mtume wa Mwisho wa ulimwengu mzima.  Myahudi mwenye kumkubali kumfuata Mtume Muhammad ndio basi ametimiza maamrisho ya Musa na Ibrahim na Manabii wake wote anaowaamini.  Mkristo anayemkubali Muhammad na akamfuata ndio ametimiza Ukristo wake, na amekubali kweli mafunzo yaliyomo katika Taurati na Injili na khasa ameyafuata maamrisho ya Yesu.  Qur'ani inasema:
Hakika Walioamini na Mayahudi na Wakristo na Wasabai: ye yote atakayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akatenda mema, basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
(Qur'ani) Al Baqara 2.62
Dunia wakati wa Yesu ilikuwa bado haijawa tayari kuweza kupokea fikra ya dini ya kukusanya ulimwengu mzima, dini isiyokuwa ya kabila fulani, au rangi fulani.  Sisi leo tunaona jambo hilo ni la kawaida tu, lakini zama zile kila kikabila kilikuwa na lake. Ndio maana hata Manabii wa kweli waliotokana na Waisraili walimwita Mwenyezi Mungu kwa jina la Mungu wa Israili. Na kweli kila taifa lilikuwa na mungu wake, na ibada zake. Ni khatua kubwa hiyo aliyochukua Yesu kuwaambia wanafunzi wake wende kwa kabila kumi na mbili za Israili. Yesu hakutangaza dini yake ila kwa "kondoo waliopotea wa nyumba ya Israili." Ndio maana akasema kuwa yeye hawaombei walimwengu, bali wale tu aliopewa na Mungu, Wana wa Israili.  Yesu aliogopa kuwa mafunzo yake yakipelekwa kwa mataifa mengine wasio Waisraili yatavurugwa mafunzo hayo kama nguruwe waliotupiwa lulu wangeziponda hizo lulu na kuwararua watu kwa kutojua thamani ya lulu. Lakini Yesu alisema katika Karamu ya Mwisho kuwambia wanafunzi wake kuwa wakati ukifika atakuja atayetimiza kweli yote, atafunza ulimwengu mzima juu ya dhambi, haki na hukumu.

Na kweli tumeiona. Historia iwazi kuwa hapana mtu aliyefunza udugu wa walimwengu kama alivyofunza Mtume Muhammad.  Hapana mtu aliyevunja ubaguzi kama alivyouvunja Muhammad.  Hapana mtu aliyepiga marfuku khitilafu za rangi na kabila na taifa kama Muhammad.  Ndio maana tangu mwanzo wake waliomfuata wakawa pamoja naye kufa kupona, hawakuwa watu wa kabila lake tu la Kikureshi, au taifa lake tu la Kiarabu, bali walikuwamo pia Wazungu, Waafrika na Waasia.  Ni yeye Muhammad ndiye aliyesema:  "Majivuno kwa uungwana wa kikale nayakanyaga chini ya miguu yangu.  Mwaarabu si bora kuliko asiyekuwa Mwaarabu, wala asiyekuwa Mwaarabu si bora kuliko Mwaarabu.  Mwekundu si bora kuliko mweusi wala mweusi si bora kuliko mwekundu, ila kwa uchamngu.  Watu wote ni sawa kama meno ya kitana.  Wote ni wana wa Adam, na Adam ametokana na mchanga."

Hayo ni machache katika maneno yake aliyoyasema juu ya ubaguzi wa rangi na taifa, jambo ambalo mpaka hii leo linawahangaisha wasiomfuata Muhammad.  Tena Mtume Muhammad hakusema tu bali alitenda.
Katika Uislamu hapana waajibu wenye fadhila kama sala za jamaa. Na katika hizo, nyadhifa mbili ndio tukufu:  Imamu na Muadhini.  Mtume mwenyewe alikuwa ndiye Imamu, na akamteua Bilal kuwa Muadhini wa kwanza katika Uislamu.  Bilal alikuwa Muafrika mweusi, aliyekombolewa na Abubakar kutoka utumwani. Mtume hakuona junaha kumwoza Zaid binti wa shangazi lake yeye Mtume, na ilhali huyo Zaid alikuwa kwanza ni mtumwa wa Kiarabu, wake yeye mwenyewe Muhammad, na akamuachia huru. Wala hakuona kiroja kumteua Usama, chotara wa mama wa Kiafrika mweusi, awe Jemadari wa jeshi kuu la Kiislamu kupambana na Warumi, na chini yake walikuwa Masahaba wakubwa wakubwa wa Kikureshi.  Yeye huyo kijana chotara, Usama, alikuwa umri wake miaka 18.

Safari moja walikuja baadhi ya Waarabu wakamtaka Mtume awapatie mume wa Kiarabu wa ukoo mzuri kumwoza binti yao.  Mtume akawaambia:  Mwamuonaje Bilal?  Wale jamaa wakenda zao.  Siku ya pili wakaja tena, na Mtume akawauliza suala lile lile la jana; wakenda zao.  Siku ya tatu wakaja tena, na Mtume akawauliza suala lile lile la jana na juzi, lakini akaongeza: "Mwamuonaje mwanamume katika watu wa Peponi?"  Wakamwoza.  Watu wote wakajua kuwa Muhammad habagui baina ya watu ila kwa uchamngu wao tu.  Masahaba walimtukuza Bilal kama alivyokuwa akitukuzwa na mwenyewe Mtume.
Mwenyezi Mungu wa watu wote, dini ya watu wote, Udugu wa watu wote - hayo yasingeweza kufunzwa ila na mtu kama yule, na kukubaliwa na watu kama wale, kwa zama kama zile.  Si ajabu basi vile Uislamu ulivyotanda kama kwamba ni moto wa nyikani.  Thomas Carlyle, muandishi na mtu mwenye mawazo madhubuti, maarufu wa Kiingereza alisema katika khutba yake kumsifu Mtume Muhammad aliyoitoa London yapata miaka mia mbili iliyopita:
"Taarikh (Historia) ya taifa huwa ina wingi wa matunda, inatukuza roho na inakuwa kubwa pale lile taifa linapoamini. Waarabu wale, yule mtu Muhammad, na ile karne moja - hebu si kama cheche moja  ilioanguka, cheche moja juu ya ulioonekana kuwa ni mchanga mweusi usio na maana?  Lakini lo! kumbe ule mchanga ni baruti inayoripuka, ukawaka ukiangaza mpaka mbinguni, kutoka Delhi (Bara Hindi) mpaka Granada (Uspania)!"

 Si imani tu ndio iliyofanya muujiza, lakini namna ya imani yenyewe, imani ya udugu wa binaadamu wote, na dini ya ulimwengu mzima.  Kutoka Kaskazini mpaka Kusini mwa dunia, kutoka Mashariki mpaka Magharibi, wote wakaifuata imani moja.  Wote wakaelekea Makka. Wote wakawa ndugu, wote wakachanganya damu na tamaduni. Wakawa Umma mmoja, Taifa moja, Taifa la Kiislamu, wafuasi wa Muhammad na Isa na Musa na Ibrahim, na kila Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu. Wote walimuamini Mungu Mmoja, asiyezaa wala kuzaliwa, wala hana mfano wake. Wote waliwaamini Manabii walioletwa na Mwenyezi Mungu, na wakaamini ukweli wa asli ya dini zote zilizitoka mbinguni.


20- MSAIDIZI, MSHAURI, MLIWAZI AU MSIFIWA

Hebu sasa natulichungue hili neno lililofasiriwa Msaidizi katika Bibilia ya Kiswahili, na ambalo limeitwa "Comforter" yaani Mliwazi katika Biblia ya Kiingereza ya zamani ya King James, na likaitwa "Counsellor", yaani Mshauri katika Biblia ya Kiingereza ya Revised Standard Version, na likaitwa "Helper" yaani Msaidizi katika Biblia za Kiingereza mpya mpya kama New World Translation na Good News Bible, na "Mu'azzi", yaani Mliwazi  katika Biblia ya Kiarabu ya Darul Kitabul Muqaddas ya Cairo.

Taabu inayotupata katika kuisoma Biblia ni kuwa asli ya maandiko yote yamepotea. Tumebakiwa na nakala za tafsiri tu.  Na hata tukipata kwa mfano Injili ya Yohana iliyoandikwa kwa lugha ilioandikwa mwanzo, nayo ni Kigiriki, hatuna ushahidi wo wote kuwa ndivyo ilivyoandikwa hapo mwanzo.  Injili hii iliandikwa mwanzo wake kiasi miaka mia baada ya Yesu.  Lakini nakala zilio kongwe kabisa zinazopatikana si chini kuliko miaka mia mbili baada ya kuandikwa kwake.

Hali kadhaalika maneno aliyoyasema Yesu tunayapata kwa tafsiri tu, kwani Yesu hakusema Kigiriki wala Kilatini, bali lugha ya kawaida Palastina wakati ule ilikuwa ni Kiaramiya na lugha yao ya dini ni Kiebrania.  Zote mbili hizo zina asli moja na Kiarabu. Injili ya Yohana ndio hiyo iliyotaja hiyo bishara ya Yesu kuwa atakuja huyo aitwae Msaidizi.  Katika utangulizi wa nakla ya Biblia ya Revised Standard Version imeelezwa kuwa hata hiyo matini ya Kigiriki ilioko "imeharibiwa na makosa yaliyojumlika kwa kukosoea kosea kwa walionukulu muda wa karne kumi na nne." Wataalamu wa Biblia wakubwa kama Rudolf Bultmann (Mprotestanti) na Father John Lawrence Mackenzie (Mkatoliki) wanakubali kuwa sehemu nyengine za Injili si kweli kihistoria, na ya kwamba maneno fulani ya Yesu kwa hakika yamebuniwa na Kanisa la kale.  Ye yote asomae maandishi ya wataalamu wa Kikristo wenyewe, bali hata mwenye kusoma hizi hizi tafsiri za Biblia mbili tatu ataona vipi maneno yanavyogeuzwa, yanavyoongezwa, na yanavyopunguzwa, hata kugeuza kabisa makusudio. Encyclopaedia Brittanica (nuskha ya 15) baada ya kueleza hayo imesema: "Ushahidi kuwa hayo hakika yametokea ni mwingi na wa namna mbali mbali." Qur'ani inasema:
 Na kuna baadhi yao wanaopindua ndimi zao kwa Kitabu ili mpate kuyafikiri hayo kuwa ni ya Kitabu, wala si ya Kitabu, na wanasema:  Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu;  na hali hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu, na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na hali wanajua.
(Qur'ani) Al Imran 3.78
Je, ni neno gani hilo lilioandikwa Kigiriki kuwa Yesu kalitumia hata wengine wakalifasiri Mliwazi,  wengine Mshauri,  na wengine Msaidizi, kuwa ndiye wa kutarajiwa kuja?  Nakla kongwe kabisa iliyopo ya hiyo Injili imetumia neno la Kigiriki Parakletos ndilo wanalolifasiri Msaidizi katika Injili ya Kiswahili. Katika Kamusi la Kigiriki neno Parakletos linafasiriwa kuwa ni "mwenye kuitwa kusaidia, mtetezi, mwombezi."  Baada ya kuzingatia hayo tuliyoyasema hapo juu vipi yalivyogeuzwa geuzwa maneno, basi si jambo la kustaajabisha ikiwa neno hili Parakletos nalo wamelipotoa waandishi na wanaonukulu kwa karne na karne zilizopita, kama ilivyosemwa katika utangulizi wa Biblia ya Kiingereza ya Standard Revised Version. Tunajua vipi Wazungu walivyolipotosha jina la Muhammad, na kuliandika "Mahomet".  Hali kadhaalika neno la Kigiriki la Periklitos ni wepesi kulipotoa na kuliandika Parakletos.  Kwa dhaahiri khitilafu ni ndogo, lakini kwa hakika neno Periklitos maana yake ni Msifiwa, ambalo kwa Kiarabu ndio khasa Muhammad au Ahmad au Mahmuud.  Jambo la ajabu ni kuwa tangu wakati wa Yesu hapakutokea Mwaarabu mwenye jina hilo ila huyo Muhammad bin Abdullah, ambaye alipewa jina hilo na babu yake tangu kuzaliwa kwake bila ya kujua huyo mzee kuwa mjukuu wake atakuja kuwa Nabii ambaye amebashiriwa na Yesu.  Na huyo babu hakuwa Mkristo bali alikuwa akifuata mila ya kishirikina na wala hakuijua Taurati wala Injili.  Na wala hakutokea Giriki mwenye jina la Periklitos.

Ni makosa kusema kuwa huyo Periklitos (Msifiwa) aliyefasiriwa kwa kukosea Msaidizi, ni Roho Mtakatifu, ambaye Wakristo wanasema ni nafsi ya Mungu.  Ushahidi wa makosa hayo umo humo humo katika Injili ya Yohana.  Kama huyo Msaidizi ni Roho Mtakatifu yawaje basi Yesu kusema "yawafaa ninyi mimi niondoke;  kwa maana mimi nisipoondoka, huyo (Periklitos) hatakuja kwenu."  Roho Mtakatifu twaambiwa ni Mungu wa milele. Je, kwani Mungu hatokuwepo maadamu Yesu yupo? Je, yeye Yesu na Manabii wote waliomtangulia na watakatifu wengine hawakuteremkiwa na Roho Mtakatifu?  Hayo yamo katika Agano Jipya na Agano la Kale pia.

Huyo Periklitos (Ahmad au Muhammad) "atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu."  Na ndio hivyo ilikuwa ni Muhammad aliyedhihirisha ukweli wote wa Mwenyezi Mungu mmoja, asiyezaa wala asiyezaliwa, na akawaokoa umma mzima wasimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu cho chote, wala mtu ye yote.  Ni yeye ndiye aliyewarejesha Wakristo kwenye mafunzo ya Yesu na Musa kwamba Mwenyezi Mungu hana utatu, bali Mungu wao ni Mungu mmoja kama alivyofunza Yesu (Tazama Marko 12.29), na kama alivyoamrishwa Musa (Tazama Kutoka 20.3-4).  Ni yeye ndiye aliyemtoa Yesu katika matusi ya Mayahudi walipomshutumu kuwa ni mdanganyifu, na matusi ya wanaojiita Wakristo kumzulia kuwa kafa kifo cha laana msalabani, na kuwa yeye ni mungu wa bandia kama walivyo miungu ya washirikina makafiri.  Kweli yote imehakikishwa na huyo Periklitos, Muhammad, Roho wa Kweli.  Huyo ambaye "hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena" hawezi kuwa Mungu,bali huyo ni Mtume wa Mungu, Mtume ambaye ametuachia Kitabu kizima ambacho kila neno liliomo humo ni neno alilolisikia kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe.  Hicho ni Kitabu pekee duniani, nacho ni Qur'ani.  Na ni Mwenyezi Mungu katika Qur'ani ndiye aliyesema:
Na  aliposema Isa bin Mariam: enyi wana wa Israili! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kumbashiria Mtume atakayefika baada yangu, jina lake litakuwa Ahmad.
(Qur'ani) As Saff 61.6
Injili ya Mtakatifu Barnaba ambayo ilipigwa marfuku kwa amri ya Gelasius katika mwaka 496 B.K., karne nzima  kabla ya kuja Nabii Muhammad s.a.w. inaeleza:
Tena Yesu akasema:  Kwa maneno yenu siliwaziki, kwa sababu mnapotaraji mwangaza patakuja kiza;  lakini maliwaza yangu ni kwa kuja Mtume ambaye ataivunja kila fikra mbaya juu yangu mimi, na dini yake itaenea na kutanda ulimwengu mzima, kwani hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyomuahidi Ibrahimu baba yetu. Na linalonipa maliwaza ni kuwa dini yake haitakuwa na ukomo, kwani itahifadhiwa na Mwenyezi Mungu. Kuhani akajibu:  Baada ya kuja huyo Mtume wa Mungu watakuja manabii wengine?  Yesu akajibu:  Hawatakuja Manabii wa kweli baada yake waliotumwa na Mwenyezi Mungu, lakini watakuja manabii wengi wa uwongo, na hayo ndiyo masikitiko yangu.  Kwani shetani atawanyanyua kwa hukumu ya haki ya Mwenyezi Mungu, na atawaficha chini ya udanganyifu wa injili yangu....Tena akasema kuhani:  Huyo Masihi ataitwaje, na ishara gani itaonyesha kuja kwake?  Yesu akajibu:  Jina la Masihi ni Msifiwa, kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe alimpa jina hilo alipoiumba roho yake na akaiweka katika utukufu wa mbinguni.
Injili ya Barnaba Sura 97
Imehaririwa na kufasiriwa kutoka Muswadda uliopo katika Maktaba ya Vienna, Austria, na Lonsdal na Laura, Oxford. Hii Injili ya Barnaba ndiyo inaaminiwa kuwa ni Injili ya pekee iliyoandikwa na mwanafunzi wake mwenyewe Yesu.  Zilizobaki zimeandikwa na watu wengine baada yao hao wanafunzi kwisha kufa, lakini yakatumiwa tu majina ya hao wanafunzi.  Injili hii ilikuwa inakubaliwa kuwa ni sahihi na Wakristo wa kwanza, na ikitumiwa katika kanisa la Alexandria mpaka mwaka 325 B.K.   Mwaka huo ndipo Baraza la Nikaia likaamua kuzikubali hizi Injili nne za Mathayo, Marko, Luka na Yohana ziingizwe katika Biblia kuwa ni maandiko matakatifu, na likapiga marfuku Injili nyenginezo, na mojawapo ni hii ya Barnaba, kuwa ati si sahihi.  Vitabu hivyo vilivyokataliwa viliitwa Apokrifa, yaani vinavyofichwa, na hapo zamani ye yote aliyeonakana navyo aliuwawa.

Injili iliyokubaliwa na Baraza kuwa ni sahihi, na iliyomo katika Biblia, Injili ya Mathayo, nayo inatueleza kuwa Yesu alibashiri kutokea kwa Muhammad, ambaye ni katika uzao wa Ismaili, anayefananishwa na jiwe liliokataliwa na wajenzi.  Pia Yesu  alibashiri kuinuka kwa Umma wa Kiislamu utakaopewa Ufalme wa Mungu, nayo yote hayo yakatimia:
Yesu akwaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko,
Jiwe walilolikataa waashi,
Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni;
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu?
Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.  Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vunjika;  naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.
Mathayo 21.42-44
Yesu kwa maneno hayo tuliyoyanukulu anawaambia Waisraili:
"Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake."  Taifa la Israili halitazaa matunda tena.  Yesu alililaani.  Twasoma katika sura hii hii ya 21 ya Mathayo:
Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.  Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu;  akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele.  Mtini ukanyauka mara.
Mathayo 21.18-19
Wataalamu wa Biblia wanakubaliana kuwa huo mtini ulionyauka, usioleta matunda yake, ni taifa la Israili. Na hatuna haja kutafuta maoni ya mtaalamu ye yote kutufasiria kuwa taifa lizaalo matunda lenye kubarikiwa ni taifa la Ismaili liliomzaa Mtume Muhammad.  Biblia yenyewe inatwambia kuwa Mwenyezi Mungu alimwambia Ibrahim:
Na kwa khabari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana.  Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.
Mwanzo 17.20
Kwa hivyo tunaweza kusema bila ya wasiwasi kuwa Yesu alikusudia kuwambia Mayahudi:  "Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu kwa kuwa nyinyi mmeacha amri za Mwenyezi Mungu alizozileta Musa na nilizothibitisha mimi, na ufalme huo watapewa taifa la Muhammad, mwana wa Ismaili, taifa liliobarikiwa na Mwenyezi Mungu, lenye kufuata maamrisho yake kama alivyofundisha Ibrahim na Musa na mimi na Manabii wote waliokuja kabla yangu mimi."

Kama alivyobashiriwa Nabii Ibrahim kuwa katika uzao wake kwa mwanawe Ismail utatokea umma uliobarikiwa wenye kuleta matunda, kadhaalika alibashiriwa Nabii Musa na Mwenyezi Mungu kwamba katika ndugu zao Wana wa Israili, yaani Wana wa Ismaili, atatokea Nabii, naye ni Nabii Muhammad, ambaye Mwenyezi Mungu anawataka viumbe wote  wamuitikie na  wamfuate.  Na ye yote "asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake."  Kwa ukamilifu Mwenyezi Mungu alimwambia Nabii Musa haya:
Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao (yaani Wana wa Israeli) mfano wako wewe (Musa), nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.  Lakini nabii atakayenena nena kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena kwa jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.  Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena Bwana?  Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana;  kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope.
Kumbukumbu la Torati 18.19-22
Zingatia vyema:  maneno hayo anaambiwa Nabii Musa a.s., naye ni Nabii wa Wana wa Israili.  Nabii anayebashiriwa hatotoka miongoni mwao Wana wa Israili, bali miongoni mwa ndugu zao,  yaani Wana wa Ismaili.  Lakini Nabii huyo hatokuwa kwa Wana wa Ismaili tu, bali hata wao Waisraili pia, kwani Mwenyezi Mungu anawaambia: "Nitawaondokeshea",  yaani  wao  pia  Wana wa Israili.  Tena Mwenyezi Mungu anasema: "Mtu asiyesikiliza mananeo yangu atakayosema yule (Nabii) kwa jina langu, nitalitaka kwake."  Ni dhaahiri kuwa yawapasa watu wote, mataifa yote, wampokee huyo Nabii atakyetokea katika ukoo wa Ismaili.

Mungu anasema:  "Nitatia maneno yangu kinywani mwake." Kitabu gani ambacho kinadai, na madai yenyewe yakawa ya kweli, kuwa ni maneno khasa ya Mwenyezi Mungu isipokuwa Qur'ani? Muhammad alikuwa ni mkalimani wa Mwenyezi Mungu, akiyatamka tu   yale yaliyokuwa yakifunuliwa kwake;  na waandishi waliokuwepo miongoni mwa wafuasi wake wakiandika na wengine kuhifadhi kwa moyo maneno ya Mwenyezi Mungu wakati ule ule yeye Nabii Muhammad alipokuwa akiyatamka. Mwenyezi Mungu anamuamrisha katika  Qur'ani:
Sema:  Mimi si kizushi katika Mitume. Wala sijui nitakavyofanywa mimi wala mtakavyofanywa nyinyi.  Sifuati ila yaliyofunuliwa kwangu;  na mimi si cho chote ila ni Mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
 (Qur'ani) Al Ahqaf 46.9
Mwenyezi Mungu mwenyewe anawakabili kwa majadiliano wenye kutia shaka kuwa hii Qur'ani ni maneno yake au la:
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomtermeshia Mja wetu, basi leteni sura moja katika mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.  Na mkitofanya - na hakika hamtafanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe ulioandaliwa kwa wakanushao.
(Qur'ani) Al Baqarah 2.23-24
Kwa muda wa miaka 1400 hapajatokea mwanaadamu wala jini aliyeweza kujibu hoja hiyo.  Qur'ani ndio muujiza wa kudumu milele. Huu si muujiza wa kusimuliwa ya kwamba ulitokea, na watu wakazozana ulitokea kweli au haukutokea.  Huu ni muujiza uliobaki na utabaki ukionekana tangu siku ulipoteremka mpaka leo na mpaka milele. Unaweza kuusoma leo, kesho, kesho kutwa na mtondogoo na daima dawamu, na ukuathiri kwa ufasihi wake uliokuwa hauna mfano, utamu wa maneno yake, ukakuongoza kwa ubora wa mafunzo yake, ukakusaidia kukabiliana na ulimwengu wako, ukaondoa matatizo yako ya kidunia na ya kiroho, ukatengeneza dunia yako na akhera yako.

Yamkinika kuwa mimi nikatuhumiwa kuwa imani yangu inanipelekea kuisifu hivi Qur'ani, lakini hebu natuiachie kalamu ya Muingereza Mkristo, Edward Gibbon, ambaye ni mtaalamu mkubwa wa historia, na bingwa wa uandishi, tuiache kalamu yake isiyo na  khofu wala mapendeleo ituhukumie. Gibbon ameandika:
"Hapana kitabu duniani ambacho ndani yake Mwenyezi Mungu ameelezwa kwa utakatifu zaidi, kwa ubora zaidi, kwa usafi zaidi, kwa uzuri zaidi, kwa ukamilifu zaidi, kwa utukufu zaidi, na chenye kustahili zaidi Ungu kuliko Mungu huyu aliyekuwa Muhammad akimuabudu.  Ruwaza hii haiwezi kutengenezwa kuliko ilivyo;  sifa moja tu ikiondolewa italeta nuksani katika ukamilifu wake, na haiwezekani hata moja kuongezwa bila ya kuonekana kuwa imezidi na haina maana.  Ni jinsi hiyo alivyo Mungu wa Muhammad kama alivyoelezwa katika Qur'ani.  Kwa ujasiri kweli amepiga chapa isiyofutika kabisa juu ya sahifa za historia wazo la imani safi kabisa ya Mwenyezi Mungu Mmoja wa pekee;  na kuliendea wazo hilo mwanaadamu mwenye akili, akitaka asitake, hawezi ila aliendee kwa yakini, hata ingawa pole pole."

Basi ni kitabu hichi ndicho kilichowafanya Waislamu wa zamani wa Vyuo vyao Vikuu vya Cordova (katika Uspania), Cairo, Damascus na Baghdad wakawa ndio waanzishi wa ilimu za Algebra, Alkimya (chemistry), Falaki (Astronomy) na utibabu wa kisasa. Peke yake ni jambo la kustaajabisha kuwa mtu ambaye mwenyewe alikuwa hajui kusoma wala kuandika, katika kaumu ya wajinga, amri ya kwanza iliyofunuliwa kwake - si kusali,wala kutoa zaka, wala kutazama wagonjwa na wazee, bali hata si kuamini Mungu mmoja, bali:
Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba, amemuumba mwanaadamu kwa tone la damu iliyotundikwa. Soma! na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote, ambaye amefundisha kwa kalamu.  Amemfundisha mwanaadamu yale aliyokuwa hayajui.
 (Qur'ani) Al 'Alaq 96.1-5
Umma uliokuwa mjinga, mabedui wa jangwani - hali yao haikukhitalifiana sana na kabila yo yote ya Kiafrika yenye kutangatanga na mifugo yao, kama Wamasai, ambao ndani yake waliokuwa wakijua kusoma na kuandika wakihisabika kwa vidole vya mkono mmoja - Umma kama huo ukaamrishwa la mwanzo la kulifanya ni kusoma, na Mwenyezi Mungu mwenye kutoa amri hiyo hakutafuta sifa kubwa kuliko Aliyefundisha kwa kalamu,  Aliyemfundisha mwanaadamu yale aliyokuwa hayajui.   Kama huu si muujiza upi mwenginewe? Hii ni Ishara kuwa enzi mpya imekuja, enzi ya kusoma, enzi ya kalamu, enzi ya kutumia akili. Enzi za kugeuza fimbo kuwa nyoka, kufufua walioonekana kama wamekufa, kugeuza maji yakawa mvinyo na mazingaombwe kama hayo zimepita. Hayo labda yafanywe juu ya jukwaa katika majumba ya tamasha kwa kuwastarehesha vijana.  Lakini katika mambo yaliyo na uzito kweli yahitaji masomo, kujifunza, na kufundisha kwa kalamu. Huu wakati wa muujiza wa hichi Kitabu kilichoandikwa kwa kalamu na kinachoweza kusomwa milele, na kila mwenye tatizo lake anaweza kulitatua kwa kusoma na kuzingatia vilivyo yaliyoandikwa humu na mwenyewe Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanaadamu kutokana na tone la damu, bali kutokana na mchanga khasa. Zama za muujiza wa kutumia akili na masomo umefika.

Bila ya Qur'ani ilimu zote za Warumi, za Magiriki, za Waajemi, za India, za China, za Misri, na za Iraq, zingelipotea kabisa, badala ya kuwa zimehifadhiwa, na zikazidi kukuzwa na kuendelezwa na zikakabidhiwa ulimwengu huu wa leo.

Kila tunapoona neema ya uvumbuzi wo wote ambao tukafikiri kuwa ndio wa kisasa na umetokana na Wazungu yafaa tushukuru kuwa lau kwamba ingelikuwa Qur'ani haikuamsha ulimwengu, na wakazindukana Waislamu wakatuhifadhia yaliyopita na wakayaongeza mengi sana yao wenyewe tunsingezipata hizi neema za leo, ikiwa ni katika matibabu, ikiwa ni katika vipando, ikiwa katika makaazi, ikiwa katika vyakula, ikiwa katika usafiri, na ikiwa katika fanni zo zote na ilimu zo zote za sayansi.  Kitabu hichi ndicho kilichowageuza waliokuwa wakiabudu jua  na mwezi na nyota na mawe na mito na miti na milima, kikawaambia kuwa vyote hivyo na vyenginevyo vyote vimeumbwa ili vimtumikie mwanaadamu.  Ni Kitabu hichi kilichokomboa akili za watu zichungue mpaka katika sehemu ambazo watu kabla yake hata hawajaziotea:
Enyi jamii ya majini na watu!  Mkiweza kupenye kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni!
(Qur'ani) Ar Rahman 55.33
Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama, na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanaozingatia.
(Qur'ani) Al Baqarah 2.164
Vifungu hivi viwili tu tulivyovinukulu hapa vyatosha kukupa mawazo vipi Qur'ani ilizindua wanaadamu waliolala washughulikie ilimu, na uchunguzi, na utafiti na uvumbuzi.  Uropa iliolala katika Karne za Giza (Dark Ages) ilizinduliwa na muamko wa Kiislamu katika kila ilimu.  Katika vifungu hivi tunaona mahimizo na ishara ya kuanzisha ilimu za anga (Space Sciences), ilimu za matabaka ya ardhi na uvumbuzi wa maadini (Geology na Minerology), Jiografia, ilimu ya unahodha (Navigation), ilimu ya hali za hewa (Meteriology), na ilimu za zaraa (ukulima).  Huu  ni mfano mdogo tu; ni kama tone katika bahari.  Mwenye kuisoma Qur'ani kwa moyo safi na akili kunjufu atagundua ndani yake uwongofu ambao haupati po pote kwengineko, atapata ilimu ambazo hazipati po pote, na atapata ukunjufu wa moyo ambao hawezi kuupata penginepo.
Katika bishara aliyopewa Musa na Mwenyezi Mungu juu ya kuja Nabii Muhammad aliambiwa:  "Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii usimwogope."

Ikiwa Mtume Muhammad alikuwa na sifa yo yote ambayo ilizagaa zaidi kuliko nyengine basi ni hiyo sifa ya kubashiri jambo nalo likatokea kama  alivyosema.  Hayo yajuulikana kikweli kwa kuwa maisha yake, kinyume na waongozi wa dini zilizotangulia,  yalikuwa katika zama ambazo zinajuulikana vyema na wanachuoni wa taarikh (historia).  Yeye si mtu wa hadithini, lakini ni mtu wa hakika, anayejuulikana vilivyo, mtu aliyekuwa akikatibiana na kupambana na wakuu wa serikali na dola zilizokuwapo zama zake.  Akikatibiana na Mfalme wa Uajemi, na Mfalme wa Rumi, na Wakuu wa Misri na Uhabeshi, na Wakuu wengineo walioko Arabuni na nje ya Arabuni. Kwa kutimia kauli zake, kama tulivyokwisha toa mifano kadhaa wa kadhaa, ndio akaitwa As saadiq, Msema Kweli, Al Amin, Muaminifu.

Bishara aliyopewa Nabii Musa a.s. inasema:  "Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe." Hakuja Nabii baada ya Musa aliyefanana naye kama alivyofanana naye Nabii Muhammad.  Musa na Muhammad walikuwa wakhubiri wa dini kwa mambo ya kiroho, na vile vile wakawa ni waongozi katika mambo ya dunia.  Walikuwa wamekusanya dini na siasa, Unabii na utawala, uwalii na uamiri jeshi.  Walikuwa ni maraisi wa kaumu zao, walikuwa mahakimu, walikuwa wapigania uhuru licha ya kuwa wanasiasa.  Nabii Musa alipambana na Firauni na kaumu yake, Muhammad alipambana na Abu Jahli na kaumu yake. Musa ilimlazimu akimbie ahame Misri alikozaliwa ende Palastina. Muhammad pia ilimlazimu aongoze watu wake kukimbia adhabu za Makureshi Makka alikozaliwa ende Madina.  Nabii Musa kapokea sharia ya Mungu katika Taurati, na Nabii Muhammad kapokea sharia ya Mungu katika Qur'ani. Wote wawili walioa wakawa na wake na wakazaa.  Wote wawili walikufa kitandani ulipotimia mwisho wa maisha yao.
Mwenyezi Mungu alimwambia Nabii Musa:  "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa."

"Nabii yule atakufa." Nini maana ya haya?  Kufa ni faradhi kwa kila kilio hai.  Maana yake atakufa siku si zake, yaani atakufa ghafla naye kijana, au atauliwa.  Nabii Muhammad alikufa na umri wake miaka 63, kiasi ya umri wa utuuzima wakati ule na mpaka hivi sasa.  Juu ya misukosuko isiyokadirika, na vita alivyopambana navyo, na majaribio ya kumuua aliyofanyiwa katika maisha yake, Mwenyezi Mungu alimsalimu mpaka akafika wakati wake baada ya kutimiza na kukamilisha ujmbe wake aliyopewa, na akafa kitandani, na huku kazungukwa na ahali zake. Yaliyosemwa katika Taurati pia yamesemwa katika Qur'ani:
Na kama (Mtume) angelizua juu yetu baadhi ya maneno tu bila shaka tungelimshika kwa mkono wa kulia - kisha kwa hakika tungelimkata mshipa mkubwa wa moyo;  na hapana ye yote katika nyinyi angeweza kutuzuia naye.
(Qur'ani) Al Haqqah 69.44-47
Ama wanavyodai wengine kuwa bishara hii yamkhusu Yesu wamekosea sana. Yesu hakufanana na Musa ila katika kuwa ni Nabii na kuwa ni Mwana wa Israili.  Kwa unabii wale wanaomdaia ungu Yesu wanamkatalia kuwa ni Nabii.  Ikiwa Yesu kafanana na Musa, basi si Mwana wa Mungu wala si Mungu. Kwa hivyo wanajipinga wenyewe. Bishara inasema wazi kuwa huyo Nabii hatakuwa katika Wana wa Israili, bali miongoni mwa ndugu zao, nao ni Wana wa Ismaili. Yesu ni Muisraili. Kwa hoja hii pia Yesu siye aliyebashiriwa hapa. Nabii huyo aliyebashiriwa kama ni wa kweli hauliwi, wala hafi kijana.  Yesu, kama wanavyodai Mayahudi na wakaamini Wakristo, aliuwawa msalabani, tena yungali kijana.  Ikiwa bishara hii wanataka kumuambatisha nayo yeye Yesu, basi itakuwa wanamtuhumu kuwa Yesu ni nabii wa uwongo "aliyenena neno kwa kujikinai kwa jina la Mungu, ambalo hakuagizwa kulinena." Mwenyezi Mungu apishe mbali. Zaidi ya hayo Nabii Isa kinyume na Nabii Musa na Nabii Muhammad (rehema na amani ya Mungu iwashukie wote) hakuja na sharia yo yote. Yeye alifuata ile ile sharia ya Musa iliomo katika Taurati, na mwenyewe kasema yeye hakuja ila kutimiza tu. Wala yeye hakuongoza watu katika mambo ya kilimwengu, bali alimwachia Kaisari ulimwengu na yeye kashughulikia mambo ya akhera, ufalme wa mbinguni. 

Miezi mitatu tu kabla ya kifo chake Mtume Muhammad s.a.w. aliyataja maneno ya Mwenyezi Mungu aliyoteremshiwa: 

Leo waliokufuru wamekata tamaa katika Dini yenu, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi.  Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.
 (Qur'ani) Al Maida 5.3

Miaka mia sita kabla ya haya Yesu naye alisema:  "Chakula changu ni kufanya mapenzi ya yeye aliyenituma na kutimiza kazi yake." 
 
Wote wawili wamekutana kwenye kutenda apendayo Yeye aliyewatuma, na huo ndio Utume, na huo ndio Unabii, na huo ndio Uislamu.  Kutenda mapenzi ya Mwenyezi Mungu ndio waajibu wa binaadamu, na katika hayo ndio hupatikana wema, na katika hayo ndio kuhisabiwa haki katika maisha haya na maisha ya milele ya baadaye. Huko ni kufuata mwenendo wa maumbile aliyowaumbia Mwenyezi Mungu wanaadamu wote kama mwenyewe asemavyo: 

Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la mwenyewe Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu;  hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu.  Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa, walakini watu wengi hawajui.
(Qur'ani) Ar Rum 30.30
 

21- MWISHO

Nalianza risala hii kwa kunukulu maneno aliyoyasema Father John Mackenzie. Sioni bora kuliko kumalizia kwa kuyanukulu maneno ya Mkristo mwingine, Geoffrey Parrindar, aliyeandika katika kitabu chake Jesus in the Quran (Yesu katika Qur'ani). Amesema: 

Inadhaniwa, bila ya kuzingatia vilivyo, ya kwamba imani zote zinazoaminiwa kwa dasturi, kuwa msingi wake ni Biblia. Fikra za kumfikiria Mungu zenye asli ya vitabu vya mbinguni, yafaa zisafishwe na yale mawazo ya Kigiriki yaliyozipamba.  Tena pia ikiwa ilimu ya "Thiolojia" (Ilimu ya Ungu) iambatane na ulimwengu wa leo, basi ni lazima ielezwe kwa njia yenye maana.  Maneno kama Mwana wa Mungu, Utatu na Uwokofu yapasa yapewe sura nyingine na maana nyingine.  Mawazo ya unabii, na ufunuo, lazima yachunguliwe upya kwa vile ya kuwa hakika bila ya shaka yo yote Mwenyezi Mungu amemfunulia Muhammad katika Qur'ani.  Tena yapasa tuonyeshe ukarimu zaidi na mafahamiano mema zaidi kwa watu wa dini nyenginezo.  Sisi mara nyingi tunafedheheshwa vile walivyo kuwa Waislamu wanatuonyesha mfano bora kwa Watu wengine wa Kitabu.  Siku zote Wakristo yahitaji wakumbuke maneno ya Yesu, "Kwa nini kuniita, Bwana, Bwana, na hamfanyi niyasemayo?"


Source: