Tuesday, March 17, 2015

REVEREND CHRISTOPHER MTIKILA IN COURT AGAINST KADHI'S COURT IN TANZANIA

Imetoka  Mwanahalisi.online

MCHUNGAJI  MTIKILA  AZUWIA MAHAKAMA  YA  KADHI  MAHAKAMANI

Huku ni kutafuta umaarufu kwani Mwanasheria Mkuu wa Serikali  George Masaju, na Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda alishasema kuwa  Mahakama hii itashughulikia masuala ya  Ndoa, Mirathi, Malezi ya Watoto, na Wakfu.

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), MCHUNGAJI Christopher Mtikila, leo amefungua kesi ya kikatiba namba 14 ya mwaka 2015 katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria kwa ajili ya kuitambua rasmi Mahakama ya Kadhi. Deusdedit Kahangwa anaripoti.

Muswada huo umepangwa kuwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa katika kikao cha Bunge litakaloanza vikao vyake Jumanne wiki hii mjini Dodoma.

Katika mashtaka yake, Mchungaji Mtikila aliye Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Democratic (DP), anaitaka mahakama kuu kufanya mambo makuu matatu.

Kwanza, anaitaka imwadhibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kwa kumpa kifungo kisichopungua miaka mitano kutokana na kitendo chake cha jaribio la kuvunja ibara ya 19 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Pili, anaitaka itamke kwamba ni kinyume cha sheria kwa serikali kujihusisha katika masuala yoyote yanayohusu Mahakama ya Kadhi au Shirika la Waislamu Duniani (OIC).

Na tatu, anaitaka Mahakama Kuu itamke kwamba adhabu zinazotolewa na Mahakama ya Kadhi kwa mujibu wa sheria za Kiislam (sharia), kama vile viboko, kupondwa mawe hadi kufa, kukata kichwa, na kukata mikono, zinapingana na utu wa binadamu, na ni kinyume cha Tamko la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyo mikononi mwa MwanaHALISIOnline, mshitakiwa mkuu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, ambaye ni mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala yote ya kisheria. Masaju anakabiliwa na mashtaka makuu mawili.

Kwanza, Mtikila anamtuhumu Masaju kushirikiana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri Mary Nagu, Asha-Rose Migiro na mawakala mbalimbali katika kuratibu uanzishwaji wa “Mahakama ya Kadhi” kazi ambayo ni sehemu ya mradi mpana wa “kuibadilisha Tanzania kuwa dola ya Kiislam.”

Kwa mujibu wa Mtikila hili ni jaribio la “kuipindua serikali ya kidemokrasia na isiyofungamana na dini yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” na badala yake kusimika mfumo wa serikali yenye mnasaba na dini ya Kiislam “chini ya usimamizi wa makadhi.”

Mtikila anadai kwamba, kwa mujibu wa sheria za Kiislam (sharia), kiongozi aitwaye “Kadhi Mkuu” anapaswa kuwa na mamlaka ya pili baada ya rais wa nchi.

Hivyo, anasisitiza kuwa mfumo huu wa kisheria utawainua waislamu wapatao milioni 12.4 dhidi ya Wakristo wapatao milioni 29 hapa nchini Tanzania.

“Muswada kuhusu Mahakama ya Kadhi haukubaliki Tanzania kwa kuwa ni wa kibaguzi, kwani unawahusu Wasislam pekee ambao ni sehemu ndogo ya wananchi, na hivyo utawafanya wananchi baki kuwa watumwa wa waislam, jambo ambalo ni kinyume cha ibara za 12, 13(2), 13(4), 13(5) na 19 katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977,” anasema Mtikila.

Kwa mujibu wa Mtikila Wakristo hao milioni 29 wanajumuisha Walutheri milioni 5.5, Wakatoliki milioni 11, Waanglikana milioni 3, Wamoraviani milioni 1.8, Wapentekoste milioni 5.8, Waadventisti milioni 1.8 na waumini wa dini za asili milioni 7.

Pili, Mtikila anamtuhumu Masaju kushirikiana na Waziri Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Ernest Ndikilo, Karen Yunus, Issa Njiku, Dan Makanga, na Ernest Mangu kusigina katiba ya nchi kwa kuwaweka Wakristo milioni 29 chini ya utumwa wa Kiislam, kwa kuwazuia kuchinja mifugo yao kwa ajili ya kitoweo, na badala yake kuwataka wale kitoweo kutokana na wanyama waliochinjwa na Waislam.

Kwa mujibu wa mchungaji Mtikila, jambo hili ni kinyume cha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003; kinyume cha Sheria ya Chakula, Madawa na Vipodozi ya mwaka 2003; na kinyume cha ibara ya 19 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa kuzingatia tuhuma hizi, Mtikila anaiomba Mahakama Kuu kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na washirika wake kujieleza ni kwa nini wasifungwe jela kwa miaka mitano na zaidi kwa kosa la kuisigina katiba ya nchi ambayo walikula kiapo cha kulinda na kuitetea.

Mtikila amefungua mashtaka hayo kwa kutumia mamlaka yake kama raia wa Tanzania mwenye jukumu la kuilinda katiba ya nchi dhidi ya dharau na usiginaji mwingine wa aina yoyote. Mamlaka hayo anapewa na ibara ya 26(2) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Chanzo ni Mwanahalisi.oline

No comments:

Post a Comment