Saturday, October 27, 2012

SHUGHULI ZA HIJJA SAUDI ARABIA

 Imebandikwa hapa leo hii tarehe 28/10/2012.

SHUGHULI   ZA  HIJJA   SAUDI   ARABIA -  Mchango wa Dada Saada  Al Ghafry wa Muscat, Oman. 
 
Hajj imekuwa na zahma sana siku hizi, na kila serikali ya Saudia ikiongeza huduma za kila aina, ndivyo zahma inaongezeka. Hivyo siku hizi mtu hawezi tu kujiendea Hijja peke yake bila kujiandikisha. 

Waishio Makkah wanaweza kufanya "Umra", hajj ndogo, dakika yeyote watakayo kwa sababu wanarudi majumbani mwao kulala. Lakini Hajj haifanyiki Makka tu, na kwa hujjaji aliyekwisha  kufanya Umra, (Hajj ndogo) hana haja ya kulala Makka hata siku moja.

Hajj inaanza kwa kulala Mina, kilomita chache kutoka Makka - wengi wanaijua Mina kama "The Tent City" kwa kuwa Mahujaji wengi wanalala kwenye mahema katika hizo siku 5-6 za Hajj. Siku kama ya leo, tarehe tisa ya mwezi uuitwao Dhul-Hijja, mahujaji wooote wanakwenda Arafat, nako kilomita chache kutoka Mina ambako wanasimama wakiabudu kuanzia asubuhi mpaka jua likizama, kisha woooote wanakwenda Muzdalifa, ambako wanasali na kulala sehemu ya wazi kabisa hakuna nyumba wala hema. Baada ya sala ya Alfajiri, woooote wanarudi Mina, wanarusha mawe kwenye Jamaraat na kuchinja, kisha wanaoga na kuelekea Makka kuzunguka Ka'aba (kitendo hicho kinaitwa "Tawwaaf Ifaadha" (kuzunguka Ka'aba), na kurudi Mina moja kwa moja.

Kwa sababu ya msongamano wa malazi, usafiri na huduma za chakula na maji, serikali inalazimika kujua ni wangapi watakaohiji ili kila mmoja huduma hizo zipatikane bila matatizo. Serikali imelazimika kupata msaada wa wakandarasi wa Hajj ambao nao pia lazima wawe na usajili na kibali cha ukandarasi. Usajili wa mahujaji unamalizika mwezi kabla ya Hajj kutoa fursa kwa serikali ya Saudia kukamilisha matayarisho yanayolingana na idadi iliyosajiliwa. 

Tukirudi kwenye swali lako: Laa, aishie Makka hawezi kukurupuka tu na kwenda Hajj kila mwaka akitaka bila usajili. Kwa ujumla, ingawa si wote, lakini wengi wao huondoka mjini kuwaachia malazi watokao kila kona za dunia, Umra rukhsa wakati wote, Hajj lazima kwa usajili, Kama leo, kwa sababu Hajj ni weekend, si chini ya wakazi wa Saudi nao watateremka Hajj. Leo alfajiri nimeona wengi wakiitamari (wakifanya umra) kabla na baada ya sala na wakimaliza wanaelekea Arafat moja kwa moja. Wengi wao wakimaliza Tawwaaf Ifaadha wataondoka kurudi makwao tayari kuingia mgodini Jumamosi. Hao wanakuwa wanajitayarisha kulala ovyo "rough" wakiwa na mahitaji yao yote kama wanakwenda weekend camping. Ila siku hizi waliokuwa wanalala chini ya madaraja hawaruhusiwi tena maana ni hatari kwao na kwa mahujaji wengine, polisi hupita na kuwahamishia sehemu za usalama. Ukikwaji wa utaratibu namna hii, unaongezea polisi mzigo usio lazima. 

Lakini  binadamu anakatazika? Wapo wanaokikuka taratibu, lakini rukhsa hawana...

No comments:

Post a Comment