Sunday, February 17, 2013

MAELFU WAMZIKA SHEIKH NASSOR ABDALLAH BACHU, ZANZIBAR, TANZANIA

Imetundikwa hapa leo hii tarehe  18/2/2013.

Kutoka:-
http://zanzibariyetu.wordpress.com/2013/02/14/maelfu-wamzika-sheikh-nassor-abdallah-bachu/



MTAFARUKU mkubwa umezuka kati ya familia na wanafunzi wa Mwanachuoni Mkubwa wa Dini ya Kiislamu wa Afrika Mashariki, Sheikh Nassor Abdallah Bachu aliyefariki dunia jana mchana huko Chukwani Mjini Zanzibar.Mtafaruku huo umekuja baada ya wanafamilia kuchimba kaburi mbele ya kibla cha Msikiti ambayo amesaliwa huku wanafunzi wa Sheikh huyo wakisema hawezi kuzikwa katika kibla cha Msikiti kwa kuwa ni kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu.

Kamati ya maandalizi ya mazishi hayo imesema kitendo kilichofanywa na wanafamilia kuchimba kaburi mbele ya msikini ni kinyume mafundisho ya dini na ni tofauti na alivyokuwa akihubiri wakati wa uhai wake ambapo mara zote alikuwa akikataza waumini wa dini ya kiislamu kuzikwa ndani ya msikiti au mbele ya msikiti.

Akiongozwa kamati hiyo, Sheikh Nurdin Kishki aliwatangazia waumini kuwa na subra wakati kamati ya maandalizi ya Sheikh huyo ikiwa ikifanya mazungumzo na wanafamilia ili kufikia mwafaka wa wapi lichimbwe kaburi lake, huku kila mmoja aliyekuwepo katika mkuanyiko huo wakisomeshana namna ya kuzikana maiti za kiislamu.

Wakati waumini hao wakitakiwa kuwa na subra baadhi ya waumini wamekwenda kulifukia kaburi la awali lililochimbwa na kusema haitowezekana kuzikwa katika eneo hilo na kutafutwa eneo jengine kwa ajili ya kuulaza mwili huo.

“Waumini tunakuombeni jamani muwe na subra lakini tunasema daima mwenyewe Marehemu Sheikh Nassor wakati wa uhai wake alikuwa akipinga suala la kuzikwa ndani ya msikiti au mbele ya msikiti lakini kaburi tunaliona limechimbwa mbele ya msikiti huku ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu na pia ni kinyume na kile alichokuwa akikihubiri na kukisomesha, hatuwezi kuwaingilia wanafamilia kwa kuwa sisi ni wanafunzi wake tu Sheikh lakini wao ndio wenye maiti na wao ndio wenye haki lakini tunawaomba sana katika hili tusende kinyume na dini” alisema Kishki mbele ya umati mkubwa.

Baada ya vuta ni kuvute hizo wanafamilia waliingia ndani ya msikiti na kujifungia na hatimae kutoa tamko la kuuliza ni masafa gani ambayo wanataka likachimbwe kaburi na mwili wa marehemu ulazwe.

Akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari, Said Masoud Gwiji ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wake Sheikh Nassor na pia ni mwana kamati ya maandalizi ya mazishi alisema kwamba ni vizuri wana familia wakafahamu kwamba alichokuwa akikihubiri Sheikh Nassor kiendane na kile kinachotekelzewa mwisho wa uhai wake.

Alisema sio busara kuvutana lakini kwa kuwa mafundisho ya dini ya kiislamu yanakataza kaburi kuchimbwa karibu na msikiti ni vyema likazingatiwa hilo na mazishi hayo kaburi likachimbwa kando na msikiti.

Hatimae wanafamilia na wanafunzi wa Sheikh Naassor wakakubaliana kuchimba kaburi mbali na msikiti na mazishi yakafanyika huku umati mkubwa ukiwa unashuhudia huku kila mmoja akitaka kushika maiti hiyo jambo ambalo limezusha ahama kubwa kutokana na umati mkubwa.

Naye Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameungana na melfu ya waumini wa dini ya Kiislamu jana katika mazishi ya Mwameanachuoni na Mhadhiri Mkubwa wa Dini ya Kiislamu Zanzibar, Sheikh Nassor Abdallah Bachu aliyefariki dunia juzi Chukwani Mjini Unguja.

Sheikh Nassor Bachu amefariki majira ya saa 5 mchana juzi baada ya kuugua kwa muda mrefu akisumbuliwa na kiharusi ambapo alisafirishwa kwa matibabu nchini India na katika hospitali mbali mbali za Dar es Salaam na Zanzibar kabla ya kufikwa na mauti.

Mwili wa Marehemu Sheikh Nassor ulilazimika kusaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja kutokana na kuwa hakuna Msikiti mkubwa ambao ungeweza kuhimili maelfu hayo ya watu waliofika kwa ajili ya kushindikiza mwili huyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa ummati mkubwa kama huo kushiriki mazishi ya Mwanachuoni huyo ambapo awali alitakiwa kusaliwa katika Msikiti wa Kikwajuni aliokuwa akiendesha darsa wakati wa uhai wake lakini kutokana na umati mkubwa ilishindikana na kuamuliwa kusaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, na baadae magari yamefuata msafara kuanzia Skuli ya Haile Sellasie na kuelekea Donge kwa kuzikwa ambapo kuanzia Mjini hadi Donge barabara imejaa wananchi wakisubiri njiani kuona msafara uliobeba maiti hiyo.

Mazishi ya Sheikh Nassor hayajawahi kutokea ambapo mbali ya ummati mkubwa kuja kushuhudia mazishi hayo wanawake na wanaume walioanzia Chukwani alipomalizikia uhai wake, na baadae kuletwa katika uwanja na Mnazi Mmoja na kupekelekwa huko Donge maelfu ya waumini wameonekana kusubiri maiti njiani na kushuhudia msafara mkubwa uliokuwa ukiongozwa na gari ya Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Makamo wa Pili, Mahammed Aboud Mohammed, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji, Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana, Sheikh Abdallah Talib na Masheikh mbali mbali kutoka Nairobi, Mikoa ya Tanzania Bara, na wenyeji wao Zanzibar.

Sheikh Nassor alinza kufundisha mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuendesha darsa mbali mbali katika Misikiti ya Kikwajuni na Rahaleo mnamo mwaka 1978 baada ya Mwalimu wake Sheikh Said Njugu kuanza kuumwa na kushindwa kuendesha darsa hizo ambapo majina ya wanafunzi wa Sheikh huyo yalipendekezwa matatu akiwemo Sheikh Ali Ahmad, Sheikh Othman Ali na yeye Sheikh Nassor Bachu.

Mwalimu wake Sheikh Nassor pia aliwahi kupigwa marufuku kufanya mihadhara na kuendesha darsa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo; jambo ambalo lililezwa kwamba kabla ya kifo chake Sheikh Said Njugu alikwenda kuombwa radhi na Mzee Aboud Jumbe.

Wanafunzi wa mwanzo ambayo amewasomesha Sheikh Nassor alivyoanza kuendesha darsa ambapo alianzia na wanafunzi wachache akiwemo Abdulghani Msoma ambaye ni Katibu Ofisi ya Utawala Bora, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Rashid na Ali Juma Shamhuna ambaye ni waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.

Sheikh Nassor Bachu alianza kuvuma katika miaka  ya 80 ambapo alikuwa na upinzani mkubwa kati yake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na Rais wa wakati huo Dk Salmin Amour Juma ambapo alionekana kuhimiza wajibu na maadili ya kiislamu kufuatwa jambo ambalo lilikuwa likionekana ni geni kwa wakati huo.

Mbali kupingwa na viongozi wa serikali lakini pia Sheikh Nassor alipata upinzani mkali kutoka kwa Maulamaa na Masheikh mbali mbali wa dini ya Kiislamu kutokana na kutangaza kwake msimamo wa kufuata Sunnah -Mila za Mtume Muhammad (s.a.w) ambapo waislamu walionekana kupingana naye.

Msimamo wa Sheikh Nassor Bachu ulikuwa ni kukataza kuadhimishwa kwa kuzaliwa kwa Mtume Muhammaa (s.a.w) kwa kusomwa maulid na akitaka maadhimisho hayo yawe ni kufuata matendo yake badala ya kukusanyika, pamoja na suala la muandamo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kufuatwa popote unapoonekana jambo ambalo lilikuwa likipingwa na baadhi ya Maulamaa hapa nchini wakitaka lazima Mwezi uonekane nchini na utangazwe na serikali.

Changamoto alizokumbana nazo Sheikh Nassor katika uhai wake ni nyingi ikiwemo kutengwa na baadhi ya jamii yake, kuzuwiwa kuendesha darsa, kufungiwa misikiti asisalishe na mara kadhaa kupigwa mabomu ya machozi wakitawanywa baada ya kusali swala ya Eid El Hajj ambapo hali hiyo ilianzia wakati wa utawala wa Dk Salmin na kumalizikia kwa Rais Mstaafu Amani Karume.



No comments:

Post a Comment