Sunday, December 2, 2012

ZUBERI MIPIKO ANAISHI KWA KUCHOMA MIILI YA WAFU DAR ES SALAAM



IMETUNDIKWA HUMU TAREHE  2/12/2012.

Mtanzania Anayeishi Kutimiza Mila za Kihindi za Kuchoma Miili ya Marehemu
Zuberi Mipiko 
Na Florence Majani , MWANANCHI, TANZANIA,  Ijumaa, Novemba 30,  2012  saa 13:9 PM

 Mzee huyu anasema kwa miaka 36 aliyoifanya kazi hiyo ameona na kuchoma miili mingi, hivyo amekuwa mzoefu na mahiri pengine zaidi hata ya Wahindi wenyewe.

SENTENSI iliyoandikwa katika lango kuu ni ‘Hindu Crematory’, yaani ‘Tanuru la Wahindi la Kuchomea Maiti.’

Ipo katika eneo la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambalo limetawaliwa na miti mirefu, ikiwamo miembe, mipera na mingine isiyo na matunda. Upande wa kulia, kuna nyumba mbili ndogo nyeupe.

Upande wa kushoto kuna kitu mfano wa kaburi lililosakafiwa vyema pamoja na picha ya mtu anayeonekana kuwa na hadhi kutokana na mavazi yake.

Mbele yake kuna majengo mawili makubwa yaliyoshabihiana kiasi. Yameezekwa juu kwa bati, bali  nguzo nne kubwa zinazoshokilia paa hilo ambalo kwa ndani limesheheni moshi mweusi.

Katikati ya jengo hilo, kuna kitu cha chuma, mfano wa kitanda…na hilo ndilo tanuru la kuchomea miili ya wafu, kama zinavyohubiri mila na tamaduni za Wahindi.

Ndani ya mandhari hii anaishi  Mzee Zuberi Mipiko, mwenye umri wa miaka 79 sasa.
Pamoja na ulinzi, lakini kazi yake kubwa ni kuchoma miili ya wafu.

Mipiko, mwenyeji wa Kisarawe Mkoani Pwani anasema alianza kazi katika tanuru hilo mwaka 1976.
Katika miaka 36 aliyofanya kazi ndani ya tanuru hilo, amekwishachoma maelfu ya miili ya wafu wa mataifa mbalimbali wakiwemo pia Watanzania wenzake.

Mzee Mipiko huwachomaje wafu?

 Kwanza kabisa, anasema baada ya mwili wa marehemu kuingia ndani ya jengo hilo, Wahindi huvunja  nazi tatu katika kaburi lililo karibu kabisa na lango kuu.

Baada ya hapo mwili huletwa katika tanuru lenyewe.  Yeye (Mipiko ) hupanga kuni juu ya tanuru hilo   ambalo limeundwa mithili ya kitanda cha chuma.

“Mimi huanza kupanga kuni kabla hata mwili haujafika ili kuokoa muda kwa sababu huwa napigiwa simu na kuambiwa kuwa leo kuna maiti inakuja,” anasema.

Kuni hupangwa kwa ustadi mkubwa. Zile  za ukubwa kiasi hupangwa katika umbile la reli. Magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia magharibi na mashariki  ya tanuru hilo.

“Kuni zinatakiwa ziwe nyingi kwa sababu kazi ya kuchoma mwili si ndogo,” anasema Mipiko.
 Kabla ya kuuweka mwili katika tanuru, anasema ndugu wa marehemu huuzungusha mara nne, kulizunguka tanuru hilo.

Baada ya hapo, Mwili wa marehemu ukiwa na sanda huwekwa katikati ya kuni hizo, kichwa kikielekezwa magharibi.

Kabla ya uchomaji wenyewe kuanza, mila za Wahindu hasa Baniani, hutaka kuhakikisha iwapo kweli ndugu yao amefariki.

Ndugu mmoja wa marehemu hutakiwa kuhakiki kwa kuchukua kipande kidogo cha kuni  chembamba kilichoshika moto, kisha humchoma marehemu katika unyayo mara nne, huku akilizunguka tanuru.

“Yaani, anachoma mara moja, kisha anazunguka, na anarudia hivyo hivyo hadi mara nne,” anasema.

Hatua   inayofuata ni kuchukua moto kwa kutumia makoleo maalum, kisha kuuchanganya moto huo na mafuta ya samli.

“Ninachofanya mimi hapo ni kuupaka uso wa marehemu kwa mafuta ya samli, kabla ya zoezi jingine halijaanza,” anasema.

Mzee Mipiko anasema husaidiana na ndugu za marehemu kuweka moto na mafuta ya samli katika mwili, baada ya hapo moto huanza kuwaka na kwa kawaida huwa ni mkali zaidi ya gesi.

Anasema mafuta ya samli pamoja mafuta ya marehemu mwenyewe huufanya moto kuwa mkali kuliko kawaida.

Wakati moto unaendelea kuwaka kwa kasi, Mzee Mipiko hushika mfuko uliojaa mbegu za ufuta na ndugu za marehemu hutakiwa kuzichota mkononi na kuzirusha juu ya mwili unaoendelea kuungua.

“ Hayo ndiyo mazishi yenyewe sasa na wakati huo ndugu zake huwa wamelizunguka tanuru,” anasema Mipiko
Anaongeza kuwa kwa kawaida mwili wa marehemu huchomwa na kumalizika kabisa baada ya saa mbili au mbili na nusu.
Mwili unatakiwa kuungua na na kwisha kabisa,  kinachotakiwa kubaki  ni vipande vya mifupa, lakini  wakati mwingine moto huweza kwisha kabisa na wakati huo mwili bado haujamalizika.

Kama mwili haujamalizika kabisa, Mipiko hutumia koleo lake maalum kutoa sehemu ya mwili iliyobaki, kuiweka pembeni, kisha
kupanga kuni mpya… na kuuchoma tena.
“Nikishaweka samli na mkaa pale, dakika tano tu, kila kitu tayari,” anasema Mipiko akitabasamu
Anasema wakati mwingine mwili unaobaki unakuwa ni sehemu ya tumbo, ambapo yeye hushuhudia utumbo au nyamanyama zilizoungua.

“Hii ndiyo kazi yangu, nausogeza taratibu, nauweka pembeni, halafu naanza kuchoma upya,” anasema.
Baada ya mwili kuchomwa na kwisha, ndugu mmoja wa marehemu huchukua chungu maalum kilichojazwa maji na kukiweka katikati ya miguu, kisha anatakiwa kutazama  magharibi akiyapa kisogo mabaki ya mwili huo wakati huo  waombolezaji wote wageuke pia.

Anachofanya ndugu huyo wa marehemu akiwa amesimama ni kuchukua jiwe na kukipiga chungu hicho kwa nguvu hadi kivunjike na maji yamwagike  kuelekea lilipo tanuru.

Baada ya tukio hilo  yeye pamoja na umati wote wa waombolezaji hutakiwa kuondoka bila kugeuka nyuma.
Mzee Mipiko anasema baada ya mwili kuchomwa  na moto kumalizika kabisa, yeye huchukua chuma kirefu mfano wa koleo na kuanza kuyatoa mabaki ya mwili huo ambayo kwa kawaida ni vipande vya mifupa  ya mwili na fuvu, vilivyochanganyika na majivu na mkaa kutoka tanuruni.

“Nikishasogeza mabaki yaliyochanganyika na majivu na mkaa kwa kutumia fimbo hii (anaionyesha), naanza kuvitenga vipande vya mifupa peke yake,” anasema

Mifupa hiyo huwekwa katika mifuko maalum na hatua ya mwisho ni ndugu kwenda kuyatupa baharini.
Mzee huyu anasema kwa miaka 36 aliyoifanya kazi hiyo ameona na kuchoma miili mingi, hivyo amekuwa mzoefu na mahiri pengine zaidi hata ya Wahindi wenyewe.

Anasema si raia wa India pekee ambao wanachoma  wafu, bali aliwahi kuchomwa mwanamke wa Kichagga ambaye alikuwa ameolewa na Baniani.

“Hata Wazungu wanachomwa hapa, na baadhi ya Waafrika ambao wana imani za Kibaniani,” anasema Mzee Mipiko

Hilo ndilo tanuru na kibarua ambacho Mipiko amekiishi kwa miaka 36 na kufanikiwa kujipatia kipato.
Uongozi wa Hindu Mandal umemjengea nyumba yeye na familia yake.

Anasema hana hofu juu ya kazi yake hiyo ambayo pengine yeye ndiye mtanzania pekee anayeifanya.
“Mimi najihisi kama ni malaika siogopi na ninazunguka katika matanuru haya wakati wote bila woga, kwani hata mimi si nitakufa tu,” anasema.

Anasema hana woga wala wasiwasi kuhusu kazi yake hiyo na anawafundisha watoto wake wa kiume ili siku atakayoondoka duniani, basi wawe warithi wake.


No comments:

Post a Comment