Saturday, October 17, 2009

PROPAGANDA ZA KIDINI PIA ZIMO !

Link: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=9159

Sheikh Matongo: Sijabadili dini
na Chalila Kibuda,
Imetoka: Tanzania Daima, 4 Oktoba, 2009.



SHEIKH Shariff Mikidadi Matongo, amekanusha taarifa iliyotolewa na chombo cha habari kinachomilikiwa na dhehebu moja la dini ya Kikristo kuwa ameokoka na kuacha dini yake ya Kiislamu.
Akizungumza na waandishi habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Msemaji wa sheikh huyo, Ally Mohamed, alisema taarifa hiyo inataka kuwabadilisha Waislamu kutoka kwenye imani yao licha ya sheikh huyo kuanza kazi yake akiwa na umri wa miezi tisa akitangza Uislamu .
Alisema taarifa hiyo iliandikwa na kuambatanishwa na picha ya sheikh huyo na nyuma yake kuwa na mchungaji wa dini hiyo ya kilokole akiwa anambatiza, jambo ambalo anasema hakulifanya.
Aliendelea kusema kama yeye alibatizwa katika dini hiyo wathibitishe na tukio hilo lilifanyikia wapi na huyo mchungaji aliyempa upako huo.
Aidha, alisema gazeti hakuweza kulitja kutokana na imani aliyonayo sheikh huyo kwa kutofanya maamuzi ya haraka ya kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa chombo hicho.
Mohamed alisema taratibu zinafuatwa za kukaa chini na mmiliki wa gazeti hilo kuthibitisha kwake kuwa aliokoka, vinginevyo aombe radhi ili kurudisha imani ya Waislamu dhidi ya sheikh huyo.
“Sisi Waislamu pamoja na dini za Kikristo tunaheshimiana, kutokana na hili tukae chini tuombane radhi ili tusiweze kuvuruga imani yetu na hasa huwa tunashirikiana vizuri sana katika shughuli za kiimani, kwa hili tumefika pabaya,” alisema Sheikh Mohamed.
Alisema taarifa hizo zilimfikia Sheikh Matongo akiwa nchini Comoro, alipokuwa ameitwa na Rais wa nchi hiyo, Abdallah Sambi, kwa ajili ya masuala mbalimbali yakiwamo ya dini ya Kiislamu.
Sheikh huyo alisema kutokana na taarifa hiyo, imemsababishia kuulizwa maswali na watu wengi, jambo ambalo linamsababishia mkanganyiko usiokuwa na maana.
Naye Sheikh Matongo alisema ana hamu ya kukutana na Watanzania ili kufanya nao mihadhara ya kidini kutokana na muda mrefu kuwa nje ya nchi.
Alisema hivi sasa anajiandaa kwa safari katika nchi za Ufaransa, Sudan na visiwa vya Reunion kwa mialiko ya wakuu wa nchi hizo.


Source: Tanzania Daima 4th Oktoba 2009
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=9159

No comments:

Post a Comment