Imetundikwa hapa leo hii 2/12/2012.
MWANANCHI, Tanzania, Novemba 30, 2012
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limemkana
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na
wenzake, baada ya kudai mahakamani kuwa eneo walilovamia wakidai ni mali ya
Waislamu linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila alisema hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili Ponda na wenzake 49 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa pamoja na mambo mengine kuvamia na kupora ardhi na wizi wa vifaa vya ujenzi.
Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa likimilikiwa kihalali na Bakwata.
Hata hivyo, alidai kuwa baadaye Bakwata walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited baada ya kuona eneo lililobaki halifai kujengwa chuo kikuu kutokana na ufinyu wake.
Alidai kuwa awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini miaka ya 2000 lilianza kumegwa na kuzigawia baadhi ya taasisi na wafanyabiashara na kwamba tume iliundwa na kubaini kwamba hayo yalifanyika kinyume na utaratibu.
“Baada ya kumegwa eneo lililobakia ni finyu ambalo halitoshi kujengwa chuo kikuu. Mimi nilikuwapo wakati Baraza la Wadhamini wa Bakwata wakijadili jinsi ya kupata eneo kubwa na kuijadili Kampuni ya Agritanza iliyokuwa na eneo la ekari 40 Kisarawe ili tubadilishane,” alidai.
Shahidi huyo aliongeza kuwa Agritanza ilikubali kubadilishana maeneo na kwamba wao walichukua ekari nne zilizopo Markaz (Chang’ombe) na Bakwata ikachukua ekari 40 zilizopo Kisarawe.
“Hayo yalifanyika baada ya kupata baraka kutoka katika Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22, 2011,” alisema shahidi huyo na kuongeza:
“Baada ya kufanyika mabadilishano, Agritanza walianza kushughulikia usajili wa kiwanja namba 311/3/4 na walipata. Hivyo kwa sasa ni wamiliki halali, tulishamalizana nao.”
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa eneo hilo Serikali ililitoa kwa Wamisri kwa ajili ya kujenga chuo chini ya usimamizi wa Bakwata.
Alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba huo uliosainiwa mwaka 2003, endapo Wamisri wataondoka Tanzania watarejesha eneo hilo katika umiliki wa Bakwata.
Shahidi huyo pia alitoa kielelezo cha makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza, kuhusu kubadilishana uwanja.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alipinga kwa madai kwamba kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kweka alidai kuwa barua halisi wanayo na kwamba ipo katika kumbukumbu za Bakwata, huku akisisitiza kuwa shahidi anastahili kutoa kielelezo hicho kwa sababu saini yake ipo.
Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo, alikikataa kielelezo hicho akisema Serikali ilitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.
Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa barua halisi ipo wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani, lakini akasema endapo barua halisi haipo, basi taarifa ya jana itatambulika kuwa notisi na wataruhusiwa kuiwasilisha.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13 itakapoendelea kusikilizwa kwa mashahidi wengine wa upande wa mashtaka.
Sheikh Ponda na wenzake walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 18, mwaka huu na kusomewa mashtaka manne likiwamo la wizi wa mali ya Sh59.6 milioni.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wote 50 wanakabiliwa na makosa manne kwa pamoja, lakini Sheikh Ponda na Sheikh Mukadamu Swalehe wakasomewa shtaka jingine zaidi.
Mashtaka manne yanayowakabili washtakiwa wote ni wizi, kula njama, kuingia kwa nguvu kwenye eneo lisilo mali yao kwa nia ya kutenda kosa na kujimilikisha ardhi kwa nguvu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Shtaka la tano ambalo linawakabili Sheikh Ponda ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Sheikh Swalehe ambaye ni mshtakiwa wa tano, ni la uchochezi.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo wako nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Swalehe tu ambao dhamana zao zimezuiliwa na DPP.
Wakati washtakiwa hao wakipandishwa kizimbani katika Mahakama hiyo kwa tarehe tofauti, Wakili Kweka alidai kuwa DPP ametoa hati ya kuzuia dhamana yao chini ya Kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao 50, Nassoro aliipinga hati hiyo kwa madai kuwa sababu zilizotolewa na DPP za kupinga dhamana za usalama na masilahi ya Jamhuri ni za kiujumla na kwamba Mahakama haiendeshwi kwa namna hiyo.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kweka alidai kuwa kwa Kifungu cha 148 (4), alichokitumia DPP, Mahakama inafungwa mikono na kwamba kwa mujibu wa kifungu hicho, DPP halazimishwi kutoa sababu yoyote.
CHANZO: MWANANCHI , Novemba 30, 2012
No comments:
Post a Comment