Monday, June 8, 2015

KIMORALI, MBUNDIMBUNDI ZINAVYOVUNJA NDOA WILAYANI ROMBO, TANZANIA !!!

Kimorali, Mbundimbundi ‘zinavyovunja ndoa’ Rombo [Mungu ameharamisha  Ulevi wa aina yoyote katika Kur-an-  blogger]

Na Fina Lyimo, Mwananchi, Tanzania.

Posted  Jumanne, Juni 2  2015  saa 12:1 PM
Kwa ufupi
  • Wilaya ya Rombo yadaiwa kuwa na aina 52 ya pombe za kienyeji, Mkoa wa Kilimanjaro waanzisha operesheni kukabili utengenezaji na unywaji uliokithiri.

Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro imekuwa na sifa nzuri ya  uchapakazi na kuifanya kuwa na wafanyabiashara pia wajasiriamali wengi hivyo kuchagiza maendeleo ya eneo hilo hata Taifa.
Hata hivyo, sifa hiyo nzuri inaporomoka kutokana na kuingia doa kwa kukumbwa na wimbi la utengenezaji, uuzwaji na unywaji wa pombe za kienyeji ikiwamo maarufu na haramu ya gongo.

Wilayani Rombo sasa kunakadiriwa kuwa na aina 52 za pombe zinazotengenezwa kienyeji bila kuzingatia ubora. Pombe hizo zimesababisha vijana wengi kujiingiza na kuzama katika ulevi uliopindukia hivyo kupoteza nguvu kazi.

Hali hiyo pia imeanza kuibadili sifa iliyokuwapo ya kukubalika kuwa na watu wachapakazi na wajasiriamali. Mtazamo huo umebadilika na Rombo kuanza kutazamwa kama eneo la wanywaji pombe wa kupindukia.

Matokeo ya hivi karibuni ya Ripoti ya Utafiti wa Ukubwa wa Matumizi ya Pombe nchini, yaliutaja Mkoa wa Kilimanjaro kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanywaji huku Wilaya ya Rombo ikitajwa kuongoza hasa vijana na wanaume.

Mbali na matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na matokeo yake kutangazwa Machi,  2015 unywaji uliopitiliza wa pombe haramu umeleta mifarakano ndani ya baadhi ya familia za Wilaya ya Rombo na kuzua malalamiko kutoka kwa wanandoa hasa kina mama, wanaodai kunyimwa unyumba.

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa matumizi ya pombe hizo yanatokana na wananchi wengi kushindwa kumudu bei ya bia ambayo ni kati ya Sh2,200 hadi 3,500, hivyo kukimbilia pombe za kienyeji na pombe kali (spirit). Hali hiyo ya unywaji wa pombe kupita kiasi, inaelezwa kuwa ilianza takriban miaka 15 iliyopita, ambako pia uzalishaji wa pombe zisizo na viwango ulianza na kudhoofisha baadhi ya wanaume, ambao ndiyo wateja wa kubwa.

Ingawa kina mama pia wa wilayani Rombo wamekuwa wakinywa pombe hizo, lakini hali imekuwa mbaya zaidi kwa baadhi ya wanaume na vijana.

Mkazi wa Kijiji cha Kikelewa kilichopo Tarakea wilayani humo, Germana Kimario anasema awali pombe haramu aina ya gongo ilikuwapo na ilitumiwa na baadhi ya wananume lakini  haikuwa na madhara makubwa kama ilivyo sasa.

Anasema tangu kuanza kuzalishwa aina hizo za pombe katika wilaya  hiyo, baadhi ya vijana na wanaume wamekuwa wakidhoofika siku hadi siku hali inayosababisha wanawake  kufanya kazi ambazo zingefanywa na wanaume kama vile kuchimba mitaro na kubeba zege.

Germana anasema Serikali inawajibika kuangalia namna ya kudhibiti pombe hizo kwa kuwakamata na kuwafilisi wanaozizalisha.

Anadokeza kuwa mara kadhaa wazalishaji pombe haramu wamekamatwa lakini waliachiwa na kuendelea na kazi yao. Anaeleza kwamba vijana wengi katika kijiji hicho wamegeuza pombe kuwa kama ‘wake zao’, wakisahau mambo mengi ya msingi ya kifamilia hata yale ya ujenzi wa Taifa.

“Vijana wengi hapa Rombo wakiamka asubuhi kitu wanachoweza ni ‘kimorali’ au ‘mbundimbundi’, hizo ni baadhi ya pombe zinazozalishwa hapa, ambazo zimekuwa zikiharibu afya za baadhi ya  vijana. Hali imekuwa ngumu kwa kuwa wanaume wakishaanza kunywa  pombe hizo hawawezi kufanya kazi nyingine yoyote zaidi ya kuanza kuuza vitu vya ndani ili aweze kupata fedha za kunywa,” anasimulia mama huyo.

Anaeleza kwamba katika kijiji hicho wanaume walio na nguvu, wengi ni Wakenya na kwamba  ndiyo wanaofanya kazi kutokana na mwingiliano wa eneo hilo la mpaka.

“Ndiyo hao pia wamekuwa wakitoa huduma ya ‘tendo la ndoa’ kwa wanawake wa kijiji hiki kutokana na wanaume kushindwa kutoa huduma hiyo,” anasema Germana.

Mkazi mwingine wa wilaya hiyo, Joyce Shirima ambaye hivi karibuni amehamia Dar es Salaam anasema: “Tatizo hilo linakuwa siku hadi siku kutokana na pombe hizo kupikwa karibu kila nyumba katika Tarafa ya Tarakea   na zinazidi kuharibu wanaume na vijana hapa Rombo.” Anaongeza: “Hali ilivyo sasa baadhi ya  wanaume na vijana wamekuwa wakishindwa kurudi nyumbani na kuishia kulala kwenye mitaro kutokana na ulevi.”

Mkazi mwingine, Athanas Kimario, anasema baadhi ya wanawake kutoka nje ya Rombo sasa hutumia mbinu ya kuolewa na wanaume wa Rombo ili kupata makazi ya kudumu lakini baadaye hufanya mbinu ya kupata watoto  kutoka kwa mwanaume wa nchi  jirani ya Kenya.

“Kuna uwezekano unywaji wa pombe hizo ukasababisha Tarakea ikawa na watoto wenye baba zao nchi jirani kutokana na unywaji wa hizi pombe, kwani hata ukinywa, hutamani tendo la ndoa kabisa,” anasema Kimario na kuongeza: “Kuna pombe nyingine wanaume wanaokunywa wanavimba mashavu, nyingine zinaharibu mwili, kuhakikishia hilo mtu aliyekunywa pombe hizo akikojoa kwenye majani hunyauka, hiyo inaonyesha wanachokunywa ni sumu.S"

“Mimi natumia pombe hizo pia hata tendo la ndoa silitamani kwa kuwa nikishakunywa ‘kimorali’  naishiwa nguvu kwa ulevi na siwezi kufanya chochote, ninalala tu. Sasa mke wangu ameniacha naishi mwenyewe.”

Padri wa Kanisa Katoliki, Kigango cha Kikelelwa, Serafin Kilawe anasema  kiwango cha ulevi katika tarafa hiyo ni kikubwa  na kwamba kimeathiri  baadhi ya vijana na wanaume.

Anasema hali hiyo imesababisha wanandoa wengi hasa wanawake kufikisha malalamiko yao kanisani wakiomba kusuluhishwa kutokana na waume zao kushindwa kuwahudumia katika haki ya ndoa.

“Tumekuwa tukitangaza katika ibada tunazozifanya kutaka watu waache unywaji pombe kupita kiasi, lakini hali hii imekuwa inaendelea kuota mizizi siku hadi siku kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali kugeuza maeneo yanayopika pombe hizo kuwa ‘ATM’ ya kujipatia fedha,” anasema Padri Kilawe.

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa baadhi ya wasimamizi wa sheria wamekuwa wakiwatafuta wapika pombe na kuunga urafiki nao hivyo kutowathibiti kutokana na wao kuchukua rushwa  hali inayoruhusu wapikaji kuendelea kutengeneza pombe hizo  zinazoua nguvu kazi ya Rombo.

“Kweli kazi za maendelo sasa zinafanywa na kina mama kwa kuwa ndiyo wenye nguvu na wanaume kuishia kwenye pombe na kushindwa kusaidia familia zao,” anasema Padri Kilawe na  kuongeza:
“Kuna matajiri katika kijiji hiki kazi yao ni kuua watu kwa kuwa ndiyo watengenezaji wa pombe ambazo hazina kiwango. Siasa pia imeingia, viongozi wanaochaguliwa na wananchi hawathubutu kukemea ulevi kwa kuhofia kutochaguliwa.

Huku Tarakea,  baadhi ya viongozi wanafanya kampeni za kuomba kura kwa kusema endapo wakichaguliwa wataruhusu  uuzwaji wa pombe pamoja na unywaji wa pombe hizo. Hali hiyo  inasikitisha, kiongozi kuongoza wananchi wasio na nguvu na kuruhusu wanywe sumu?”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikelelwa, Justine Shirima anakiri kuwapo kwa tatizo la wanandoa kutopewa haki yao ya msingi kutokana na ofisi yake kupokea malalamiko mengi hasa kutoka kwa wanawake.

“Wanawake wengi wanafika ofisini kuwalalamikia waume zao kutowatimizia tendo la ndoa kutokana na unywaji wa pombe uliokithiri,” anasema Shirima.

Anasema baadhi ya wanawake wanapata huduma hiyo kutoka kwa wanaume wa nchi jirani kutokana na eneo hilo kuwa mpakani na Kenya.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama anaeleza kuwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC),  mwaka jana ajenda iliyotawala ilikuwa ni unywaji wa pombe uliokithiri ndani ya mkoa na kwamba wilaya iliyokithiri ilitajwa kuwa ni Rombo.

Gama  alitoa agizo la kusambazwa kwa Waraka namba moja wa mwaka 2014 maeneo yote, ambao ulifafanua lengo la Serikali kufanya operesheni ya kudhibiti ulevi wa kupindukia ndani  ya mkoa huo.

Waraka huo uliogiza mamlaka zote za usalama na uongozi wa Serikali kuanza rasmi operesheni maalumu ya kudhibiti matumizi ya pombe yanayokiuka sheria kuanzia Desemba 15, 2014,  ulisomwa katika nyumba zote za ibada, kwenye mikusanyiko na kusambazwa kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO) mkoani Kilimanjaro kwa muda wa mwezi mmoja, kuanzia Novemba 15, 2014.

Gama anasema waraka huo ulitokana na viongozi wa dini na baadhi ya wananchi wa mkoa huo kuona baadhi wa watu wakinywa pombe zisizo na viwango.

“Rombo ilionekana kuathirika zaidi hali ambayo ilinafanya nifanye  ziara nikajionee. Nilipokwenda niliwakuta wanawake wakichimba mitaro. Nilipowauliza wakasema wanaume hawawezi kufanya tena hiyo kazi kutokana na kuathirika na pombe zisizo,” anasema Gama.

Anasema pombe zinazozalishwa  ndani ya wilaya hiyo ni sumu kutokana na kuharibu afya za binadamu kwa kuwa  hata ukiwaona baadhi ya wanywaji, wamevimba mashavu na tumbo.

“Naambiwa pombe hizo zinachanganywa na betri za magari, kinyesi cha binadamu na mbolea ya urea. Kwa kweli hali hii isiposimamiwa na kudhibitiwa kwa haraka, kizazi cha Rombo kitakwisha,” anasema Gama.

Anaongeza: “Hali hiyo ilinisukuma kuwaagiza wakuu wa  wilaya kuweka mpango mikakati ya kutokomeza pombe  haramu zinazozalishwa ndani ya wilaya, ikiwa ni pamoja na kudhibiti unywaji wa pombe saa za kazi.”

Mkuu Walaya ya Rombo, Lembris Kipuyo anasema wilaya hiyo imeonekana kuwa na viashiria 10 vya uvunjifu wa amani  alivyovitaja kuwa ni watu kujichukulia sheria mkononi, malumbano ya kisiasa, matukio ya ubakaji, mimba kwa wanafuzi na uharibifu wa mazingira.

Vingine ni dawa za kulevya, pombe haramu ya gongo, utengenezwaji wa pombe ambazo ni zaidi ya aina 52 zisizo na viwango, kukithiri kwa uhalifu wa kutumia silaha na migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima.

Kipuyo anasema kuwa kati ya vyote alivyotaja, kilichokithiri wilayani humo ni utengenezaji na unywaji wa pombe zisizo na viwango hali inayosababisha kuharibu nguvu kazi ya vijana.

Anasema kuwa kutokana na hali hiyo, wameanzisha operesheni endelevu ya kutokomeza pombe haramu ndani ya wilaya na kwamba katika ya miezi mitatu iliyopita, wamefanikiwa kukamata  na kuharibu zaidi ya lita 3,000 za gongo, mapipa  1,200  yenye lita 240  na kisima chenye zaidi ya lita 3,000 za  malighafi ya utengenezaji wa gongo.

Mkuu huyo wa wilaya anasema operesheni hiyo inayoshirikisha vitongoji, vijiji, kata pamoja na uongozi, inabena ujumbe usemao: “Wilaya Rombo bila gongo inawezekana.”

No comments:

Post a Comment