Posted on 6/2/2015.
TAMKO LA TAASISI 11 ZA KIISLAMU KWENYE
MAENEO AMBAYO YAMEPOTOSHWA NA MATAMKO YA BAADHI YA TAASISI ZA KIDINI NA
MAGAZETI IKIWEMO MAASKOFU, BAKWATA NA GAZETI LA MIZANI KWENYE MCHAKATO WA KUTOA
MAONI JUU YA MUSWADA UNAOHUSU MAHAKAMA
YA KADHI
Utangulizi
Sisi
waislam, kupitia Jumuiya na Taasisi zetu za kiislamu chini, tumepitia matamko
kadhaa yaliyotolewa na taasisi mbalimbali, watu binafsi, viongozi wa serikali
na magezeti, hususan, maaskofu, jukwaa la wakristo Tanzania, gazeti la Mizani,
Sheikh Jongo na Sheikh Mohammed Idd kutia kipindi cha Ar-risala kinachorushwa
na Kituo cha TV cha Channel 10.
Matamko
hayo yana malengo ya kupotosha baadhi ya maeneo ya maoni yaliyotolewa na Waislamu,
kupitia Jumuiya na Taasisi zao kuhusu muswada wa marekebisho ya sheria yanayohusu
mahakama ya kadhi kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Katiba, Sheria na Utawala tarehe 19/01/2015.
Muhtasari wa Maoni ya Taasisi Kumi na moja
Kwa muhtasari maoni ya
waislamu ambayo matamko tuliyoyataja hapo juu yanalenga kuyapotosha
yalibainisha makosa,
kasoro na udhaifu mwingi ulioko kwenye muswada unaohusu mahakama ya kadhi kiasi
cha kutia shaka juu ya uthabiti wa nia ya Serikali wa kutaka kuleta sheria
itakayowezesha mfumo wa utoaji haki wa sheria za Kiislamu kufanya kazi hapa
nchini kwa ufanisi zaidi kulio mfumo wa sasa unatoa nafasi kwa maafisa wa
mahakama kama majaji na mahakimu kuhukumu masuala ya sheria za Kiislamu ambapo
mara nyingi maafisa hao hawana sifa, ujuzi, maarifa na uzoefu wa kushika nafasi
ya kuhukumu chini ya utaratibu wa sheria za kiislamu.
Maoni hayo, ya waislam, kupitia
jumuiya na taasisi zao kumi na moja, yalidhihirisha dosari kubwa kwenye muswada
huo kwenye maeneo yanayohusu, kutokuwepo kwa kifungu kinacho anzisha na/au
kuitambua mahakama ya kadhi; kutokuwepo muundo wa mahakama ya kadhi
inayokusudiwa; kutoelezwa sifa za kadhi; upungufu kwenye utaratibu wa uteuzi wa
makadhi; kukosekana maelezo ya ajira na usalama wa ajira ya makadhi; mapungufu
yanayoambatana na kuweka mamlaka ya kutengeneza kanuni za mahakama ya kadhi kwa
‘Mufti’ na ya kukazia hukumu kwa Waziri; kukosekana kwa utaratibu wa kudhibiti
nidhamu, mwenendo na maadili ya makadhi; mapungufu kwenye uwigo wa mamlaka wa
mahakama; hiyari kwa mdaawa Muislamu kufungua shauri lake la sheria ya Kiislamu
katika mahakama ya kadhi; upungufu wa dhana ya mahakama ya kadhi
kujiendesha; mamlaka ya Waziri kutoa
matamko ya sheria za Kiislamu; na ulazima wa mahakama ya kadhi kutajwa kwenye
Katiba.
Kwa hoja hizo, Waislamu kupitia
taasisi zao hizo kumi na moja, walishauri kwa kupendekeza muswada mbadala
kwamba serikali iuondoe muswada huo ili uboreshwe kabla ya kuwasilishwa bungeni
kwa mjadala.
Upotoshaji Uliofanywa na Matamko Yaliyotolewa
Upotoshwaji
wa maoni ya waislamu yaliyotolewa kupitia taasisi zao kumi na moja, uliofanywa
na matamko yaliyotolewa na taasisi mbalimbali, watu binafsi, viongozi wa serikali
na magezeti, umejikita kwenye maeneo haya ya fuatayo: (i) Kuwa taasisi 11
zilizowasilisha maoni ya Waislamu juu ya muswada wa mahakama ya kadhi zinawakilisha
wachache; (ii) Kuwa asasi hizo 11 ni za Wahabi na hivyo maoni yao hayawakilishi
waislamu wote; (iii) Kuwa Mufti ndiye kiongozi mkuu wa Waislamu; (iv) Kuwa
Mufti ndiye anastahiki kuteua makadhi; (v) Kuwa BAKWATA ndiyo taasisi baba,
nyingine watoto wake; na (vi) Kuwa mahakama ya kadhi italeta hukumu za kukata
mikono, kuhukumu wasio kuwa waislamu, na kubagua wasio kuwa waislamu. Matamko
ambayo yamebeba upotoshaji huu yametolewa kwa makusudi kwa lengo la hadaa kwa Waislamu,
wananchi na serikali kwa jumla ili wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na
taasisi hizo kumi na moja ambayo kama yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha
kupatikana kwa Mahakama ya Kadhi inayokidhi matakwa ya sheria za kiislamu na
wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na kutenda haki.
Tamko Letu Dhidi ya Upotoshaji Uliotolewa
Hivyo
basi, kwa lengo la kuweka sahihi kumbukumbu na kuondosha uwezekano wa
upotoshaji huu kuchukuliwa kuwa ni kweli, ni vyema tukabainisha ukweli kama
ifuatavyo:
1.
Jumla ya taasisi kumi na moja (11)
ziliwasilisha maoni ya waislamu juu ya muswada wa mahakama ya kadhi. Hizi ni
pamoja na taasisi ambazo zinatambulika, zimesajiliwa na zenye uwakilishi na
mtandao wa kitaifa. Baadhi ya taasisi hizo ni Baraza Kuu, TAMPRO, BASUTA,
JASUTA, IPC, HAY ATUL ULAMAA, Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania; na
Shura ya Maimam Tanzania. Maoni juu ya muswada wa mahakama ya kadhi
yalipatikana baada ya mchakato uliohusisha wanachama na wawakilishi wa asasi
hizo Tanzania nzima. Hivyo, siyo kweli kuwa asasi hizi kumi na moja (11)
zinawakilisha maoni ya wachache. Ni wazi pia kuwa upotoshaji huu unadhihirisha
kuwa waliotoa kauli za upotoshaji huu wanaona uzito wa umoja huu wa asasi za Kiislamu
na maoni yao kweye suala hili la mahakama ya kadhi.
Hawa
wanaosema taasisi hizi zinawakilisha maoni ya wachache na ya wahabi,
hawatuambii kuwa maoni yao yanawakilisha taasisi ngapi za kiislamu na ya
madhehebu yepi. Ukweli ni kwamba hoja hii inadhihirisha hofu ya mshikamano wa
asasi za Kiislamu katika kukabiliana na suala hili la mahakama ya kadhi. Ndiyo
maana badala ya kujibu hoja na mapendekezo yaliyotolewa na asasi hizi, matamko
hayo yamejikita kwenye kushambulia taasisi husika kwa hoja ambazo zina misingi
ya kuwagawa Waislamu.
2.
Madai kuwa Mufti ndiye kiongozi
mkuu wa Waislamu hapa Tanzania na kwamba ndiye anaye stahili kuteua makadhi nchini
siyo sahihi. Inawezekana kwa taasisi kuwa na muundo wa uongozi ambao unamfanya
Mufti kuwa kiongozi mkuu wa Waislamu wa taasisi hiyo na hapa huyo Mufti atakuwa
mkuu wa taasisi husika na siyo Waislamu wote wa Tanzania. Mfano wa taasisi
ambazo kiongozi wake mkuu ni Mufti ni BAKWATA. Hii haina maana kuwa kiongozi
huyo ndiye kiongozi wa Waislamu wote nchi nzima. Tulieleza kwenye kamati ya
Bunge kama tunavyoeleza hapa kuwa zipo
taasisi nyingi za Kiislamu zilizoandikishwa na mamlaka mbalimbali za uandikishaji
wa asasi huru na vyama vya kijamii (NGOs) zenye maafisa wenye cheo cha Mufti.
Kwa hivyo, siyo vyema sheria kuweka mamlaka yoyote inayohusu mahakama ya kadhi (mfano uteuzi wa
makadhi) kwa Mufti wa taasisi binafsi kwa kuwa kunaweza kukatokea mgongano na
mgogoro mkubwa kwa kila asasi kutaka kutumia mufti wake
kuteua makadhi.
3.
Madai haya kwamba Mufti ndiye
kiongozi mkuu wa waislam na anaye stahili kuteua makadhi yanalenga kupotosha
hoja ya msingi kwamba siyo sahihi kwa sheria kumpa Mufti mamlaka yeyote
yahayohusu mahakama ya kadhi kwa kuwa mufti huyu, ama wa BAKWATA au wa taasisi
nyingine yeyote, siyo chombo kinachoundwa na sheria yoyote (bali katiba ya taasis husika)
na wala hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti. Mahakama ya Kadhi kuwekwa chini ya Mufti ni
kuifanya mamlaka hiyo muhimu ya kutoa haki kuwa chombo kilicho chini ya Taasisi
binafsi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Kwa mfano, siyo kila Muislamu wa
Tanzania Bara ni mwanachama wa BAKWATA na yuko chini ya Mufti wa BAKWATA. Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa kujumuika na kujiunga katika jumuiya
mbalimbali. Kuwalazimisha Waislamu wawe chini ya Mufti wa BAKWATA au Mufti wa
taasisi nyingine yeyote ni kuvunja Katiba ya nchi. Hivyo basi si sahihi mamlaka
ya kutoa haki kuhusishwa na MUFTI anayetokana na Katiba ya Taasisi binafsi.
4.
Kama tulivyokwisha eleza kwenye
maoni yetu tuliyowasilisha kwenye kamati ya Bunge juu ya muswada wa mahakama ya
kadhi, kwa istilahi ya Kiislamu “Mufti” maana yake ni alim (msomi) mwenye upeo
mkubwa wa elimu ya dini na sheria. Ni mtu aliyebobea katika taaluma za dini na
sheria. Si afisa wa Serikali wala hana dhima ya utawala au uongozi. Alim
hutambuliwa kuwa Mufti na maulamaa wenzake wa eneo husika kwa kutambua upeo
wake mkubwa katika fani za elimu ya dini na sheria. Alim akitambuliwa na kupewa
hadhi ya mufti huchukuliwa kuwa ni marejeo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi
masuala ya elimu ya dini na sheria.Kwa hiyo Mufti jukumu lake ni kufutu mas’ala
ya dini na sheria. Si kuwa mtawala au mpangaji wa masuala ya utawala. Ni dhahiri
kuwa madai yaliyotolewa kuwa Mufti ndiye kiongozi Mkuu wa waislam hayana
mashiko kilugha wala kiistilahi.
5.
Hatuamini hata kidogo kuwa
wanaotoa madai haya na upotoshaji huu hawajui nafasi ya Mufti katika mfumo wa
sheria za kiislam na kilugha. Tunashawishika kuamini kuwa wanafahamu ukweli
kama tulivyouweka hapo juu, bali wanapotosha kwa malengo mahsusi kwa sababu
baadhi yao ni wasomi wenye shahada mpaka shahada za juu katika fani mbalimbali
za dini ya Kiislamu.
6.
Madai kuwa BAKWATA ndiyo taasisi
baba na taasisi nyingine ni watoto wake
hayana mashiko yeyote ndiyo maana hata Kamati ya Bunge haikutoa mualiko
kwa BAKWATA pekee bali kwa taasisi nyingi za kiislamu ikiwemo BAKWATA. Ifahamike
kuwa BAKWATA ni taasisi ya kidini kama zilivyo taasisi nyingine lakini pia BAKWATA
ni taasisi dhaifu na iliyopoteza imani kwa Waislamu wengi nchini. Jina la
taasisi hiyo haliifanyi taasisi hiyo kuwa ndiyo kubwa na yenye hadhi kuliko
taasisi zingine za Kiislamu. Hata hivyo, kimuundo na kiuwakilishi, taasisi hii
haina sifa ya kuwa ni taasisi kubwa na yenye mamlaka dhidi ya taasisi nyingine
za Kiislamu kwa sababu zifuatazo;(i) BAKWATA haina wanachama tofauti na taasisi
zingine ambazo zina wanachama; (ii) mara kadhaa BAKWATA
imetoa matamko kuwa haiwakilishi Waislamu wote wa Tanzania; (iii) Asili
yake BAKWATA haijaundwa na waislamu kwa umoja wao. Ndiyo maana uhalali wa BAKWATA kuwa ndicho chombo kikuu cha uongozi wa waislamu
nchini umehojiwa na Waislamu mara nyingi.
7.
Kama tulivyoeleza kwenye maoni
yetu juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi, tunarudia kusema tena kuwa iwapo Serikali
itafuata upotoshaji huo kuwa BAKWATA ndiyo chombo kikuu kinachowakilisha
waislamu wote na hivyo kuipa BAKWATA nafasi ya
kuwawekea waislamu Mahakama ya Kadhi itahesabiwa na Waislamu kuwa ni hila ya
Serikali kutaka kulazimisha mamlaka ya BAKWATA juu ya Waislamu hata wale
wasioikubali taasisi hiyo. Jambo ambalo
litakuwa limekiuka haki ya msingi ya kila Mtanzania kujumuika kwa uhuru bila
kutezwa nguvu au kushinikizwa. Inasikitisha kwamba, wakati mchakato wa maoni
juu ya muswada wa mahakama ya kadhi unaendelea, baadhi ya viongozi wa juu wa
serikali wametoa kauli ambazo zinaoana na hoja dhaifu kuwa BAKWATA ndicho
chombo cha uwakilishi cha Waislamu na kwamba serikali imeuandaa mchakato wa
mahakama ya kadhi kwa kuishirikisha BAKWATA kwa karibu kama chombo
kinachowakilisha Waislamu wote. Hili ni kosa kubwa kwa kuwa BAKWATA siyo chombo
cha waislamu wote nchini..
8.
Kuna matamko yametolewa na
taasisi na watu binafsi ambao wanatumia muswada huu wa mahakama ya kadhi kuleta
hoja zinazokusudia kuleta faraka za kimadhehebu kwa propaganda ambazo hazina
msingi au ukweli wowote katika dini ya Kiislamu hasa suala la kupinga Mufti
kuwa ndiye mteuzi wa makadhi na utengenezaji wa kanuni za mahakama ya kadhi.
Tunaotoa udhaifu wa kumpa madaraka hayo Mufti tumezingatia hoja za kisheria,
kidini na kimantiki. Hivyo si kweli kuwa tunapinga Mufti kupewa madaraka hayo
kutokana na tofauti za madhehebu ndani ya uislamu. .
9.
Kadhalika, wapo viongozi wa dini
ambao si Waislamu (mfano maaskofu) wametoa matamko ya kupinga Mahakama ya Kadhi
kwa hoja kuwa italeta hukumu za kukata mikono, kuhukumu wasio kuwa waislamu,
kubagua wasio kuwa waislamu nk. Hoja hizo zote siyo za kweli na watoaji wa hoja
hizo wanajua ukweli kuwa mahakama ya kadhi inayokusudiwa ni mahakama
itakayotumia sheria za kiislamu ambazo zinatumika kwenye mahakama za kawaida
toka enzi za ukoloni mpaka leo. Inajulikana wazi kuwa mahakama ya kadhi
itashughulika na mambo binafsi ya watu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu ambazo
ni sehemu ya sheria halali zinazotumika hapa nchini, mfano mambo kama ndoa,
talaka mirathi, wakfu na malezi ya watoto. Kinachofanywa na viongozi hao wa
dini wasiokuwa waislamu ni kuivunjia heshima jamii ya Kiislamu na kupotosha ukweli
ambao uko wazi.
…………………………………………………………………………
Sheikh Suleiman A. Kilemile
Mwenyekiti wa Hay Atul -Ulamaa
03/02/2015
No comments:
Post a Comment