Mwanza bado wavutania kuchinja
Toleo la 280
6 Feb 2013, RAIA MWEMA
- Nyama zadoda buchani, wanunuzi wapungua.
ULE usemi wa Kiswahili kwamba mbuyu ulianza kama mchicha
unaonekana kusadifu katika mgogoro unaohusisha haki ya kuchinja wanyama na ndege
kwa ajili ya kitoweo unaoendelea Mwanza na Geita kati ya waislamu na
wakristo.
Tayari Umoja wa Makanisa ya Kikristo Jijini Mwanza
umetoa tamko la kupinga msimamo wa serikali kuwa wenye haki ya kuchinja kwa
ajili ya kuwauzia wananchi ni waislamu na wakristo wanaweza kuchinja majumbani
mwao tu.
Kwa mujibu wa tamko hilo, kitendo cha serikali inayosema
haina dini kuwalazimisha wakristo kufuata ibada ya dini isiyokuwa ya imani yao
ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 kifungu cha
1 na 2, inayotoa uhuru wa kila mtu kuwa na uhuru wa kuabudu na kwamba suala la
imani ya dini ni jambo binafsi na hiari ya mtu kulifuata.
Tamko hilo limewataka wakristo kutokula nyama
zilizochinjwa kinyume na imani yao, kwa kuwa tendo la kuchinja ni sehemu ya
ibada kwa waumini wa dini ya kiislamu tofauti na walivyokuwa wakifiriki mwanzoni
kwamba tendo hilo halina uhusiano wowote na ibada na hivyo hawaoni sababu ya
kuendelea kushirikishwa katika ibada isiyokuwa ya imani yao.
“Kwa kuwa sasa imebainika kuwa tendo
la kuchinja kwa wenzetu waislamu ni sehemu ya ibada kwa mujibu wa imani yao,
tofauti na tulivyokuwa tukidhani hapo awali kuwa tendo la kuchinja halina
uhusiano wowote na mambo ya ibada. Sisi wakristo hatuoni sababu ya kuendeea
kushirikishwa katika ibada ya imani isiyotuhusu. Tunatoa wito kwa wakristo wote
kuanzia sasa kutokula nyama zilizochinjwa kinyume na imani ya
kikristo” ilisema sehemu ya tamko hilo
lililotiwa saini na Askofu Charles Sekelwa ambaye ni mwenyekiti wa Umoja huo na
katibu Mchungaji wake Jacob Kituu.
Katika kuonyesha uthabiti wa msimamo wao wachungaji na
maaskofu walikutana Jumamosi iliyopita katika Parokia ya Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi Kirumba chini ya kamati ya Ulinzi na Mwasialiano ya Umoja huo na
kuazimia kuwatangazia waumini wao katika makanisa yote kususia kununua nyama
kwenye mabucha katika kipindi chote ambacho watakuwa hawajapata machinjio
yatakayowawezesha kuchinja kwa imani yao.
Tangazo hilo ambalo lilitolewa Jumapili iliyopita
limeanza kuathiri biashara hiyo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Umoja wa wenye
Mabucha Jijini Mwanza, Joshua Machage, biashara yao imeathirika sana kwa kuwa
hata waislamu wanaogopa kununua kwenye mabucha ya wakristo kwa kuhisi kwamba
watakuwa wamejichinjia.
“Tatizo hili ni kubwa, kuna wanachama
wangu wameleta taarifa hapa kuwa biashara haiendi kabisa kwa sababu ya mvutano
huu, wakristo jana (Jumapili) wametangaziwa kutonunua nyama zinazochinjwa na
watu wasiokuwa wa imani yao sasa hali ni mbaya sana kwenye biashara yetu, nyama
zimesimama kabisa hali ni mbaya,” alisema
Machage.
Mgogoro huo umeendelea kushika kasi pamoja na serikali
kumtuma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu na Sera, Steven Wassira,
kusuluhisha mgogoro huo, ambaye katika kikao chake na viongozi wa dini hizo
mbili alisisitiza msimamo wa serikali ambao ulikuwa umetolewa awali na Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo huko Nyehunge, Sengerema ambako ndiko mgogoro huo
ulikoanzia.
Sheikh wa Wilaya ya Sengerema, Ahmed Jaha Ally
aliliambia Raia Mwema kwamba kwa mtazamo wa wengi na imezoeleka katika jamii
kwamba muislamu hali asichochinja na kwamba mkristo akichinjia nyumbani kwake
akala mwenyewe hilo haliwasumbui lakini akafafanua zaidi.
“Hilo la kuchinja nyumbani halina
tabu, lakini wakichinja na kuanza kuweka kwenye mabucha hapo kunakuwa na shida
kwa sababu wanaweza kununua watu wenye hoteli na kwenda kuuza, sasa akila
muislamu kwenye hoteli hiyo itakuwa siyo haki, kwa sababu kwa mujibu wa
maelekezo ya dini yake hapaswi kula kisichochinjwa na muislamu, ” alisema.
Akijibu kuwa kuchinja ni ibada na hivyo wasiokuwa
waislamu wanashiriki ibada isiyo ya imani yao alisema kuwa hawawashirikishi
wakati wa ibada na kwamba kula nyama ile si kushiriki ibada hiyo kwa kuwa hiyo
inamhusu mchinjaji.
“Kwa kula tu hushiriki hiyo ibada kwa sababu inamhusu
mchinjaji, kwa hiyo hatuwashirikishi lakini ndugu zetu pia wakumbuke
tunavumiliana katika mambo mengi, Ijumaa ni siku ya kazi lakini Jumamosi na
Jumapili ni siku za mapumziko na sisi tumekaa kimya, kwa hiyo haya mambo
yanahitaji kuvumialiana” alisema Sheikh Ally.
Mwandishi wetu alipotembelea Ofisi ya BAKWATA Mkoa wa
Mwanza kutaka kujua msimamo wa Baraza hilo katika hali inayooendelea hivi sasa
mkoani hapa kiongozi aliyemkuta ofisni hapo alisisitiza kuwa wao hawana cha
kuongeza wala kupunguza kwa kuwa msimamo ulishatolewa na Waziri
Wassira.
“Sisi hatuna cha kuongeza wala kupunguza, msimamo
ulikwishatolewa siku ile, wewe si ulikuwapo? Ehee! Kama ulikuwapo basi sisi
hatuongezi wala kupunguza kwenye hilo, na wala usininukuu, kama wao wakristo
wanalo la kusema ni wao na serikali” alisema kiongozi huyu ambaye alikataa
kunukuliwa gazetini.
Hayo yakiendelea mkoani Mwanza, hali si shwari pia
mkoani Geita ambako uchunguzi wetu umebaini kuwa maaskofu wa Mkoa huo walikaa
kikao siku ya Jumamosi wiki jana katika ofisi ya Jimbo Katoliki Geita ili
kujadili suala hilo.
“Kikao hicho kilikuwa na dhamira ya kutoa tamko la
kuwataka wakristo kutokula nyama zinazochinjwa na watu wasiokuwa wa imani yao na
kulikuwa na mkakati wa kukubaliana kuwa na bucha au machinjio yao kwa kuwa
wanaamini serikali imeamua kuegemea upande mmoja wa suala hilo,” kilisema chanzo
chetu kuhusu kikao hicho cha maaskofu.
Imeelezwa kuwa hata viongozi wa kikristo walioungana na
msimamo wa serikali wakati wa ziara ya Wassira walishawishiwa na serikali mkoani
humo ili kuwasaliti wenzao.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula,
alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba katika kikao hicho na Waziri Wasirra
viongozi wote wa dini walikubaliana na wakatoa tamko hilo.
“Kile kikao kile kilikuwa kati ya waziri na viongozi wa
dini zote na si maaskofu tu, wale waliosema ni watu wazima na wana heshima zao
na ni viongozi wazito, wanawezaje kuhujumiwa? Lakini hoja hapa ni kwamba
walikubaliana wakaelewana kama walishawishiwa hilo si hoja” alisema mkuu huyo wa
Mkoa.
Maslahi ya Uchumi yahusishwa
Pamoja na kuhusishwa na imani, suala hilo pia limekuwa
likitazamwa kwa mtazamo wa kiuchumi hasa kwa kuzingatia kuwa hiyo ni sehemu ya
ajira kwa watu wanaohusika na shughuli ya uchinjaji kwa hiyo upo uwezekano
mkubwa wa hilo kuchangia katika sintofahamu hii inayoendelea.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu hoja hiyo iliibuka katika
kikao cha wachungaji Jumamosi wiki iliyopita jijini Mwanza ambako inaelezwa kuwa
mtoa hoja mmoja alisema kuwa suala hilo limekuwa likiwanufaisha waislam kiuchumi
wakati wamekuwa mstari wa mbele kuutukana na kuikashafu imani ya
kikristo.
“Iliibuka hoja humo kwamba kila ng’ombe anayefugwa na
mkristo anamuhakikishia muislamu shilingi elfu tano wakati wa kuchinja na katika
hizo, shilingi elfu moja inachangwa msikitini na kwamba pamoja na yote hayo
imani ya kikristu imekuwa ikikashfiwa bila serikali kufanya kitu, mtoa mada
akasisistiza kuwa kuendelea kuchinjiwa na waislamu ni kuendelea kufadhili
kukashifiwa kwa imani yao na kwa kuwa serikali imechukua upande katika hili ni
bora wajisimamie,” kieleleza chanzo chetu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Mabucha Mwanza Machage
anasema kuwa zamani kuchinjiwa ilikuwa ni kama huduma na ilikuwa ni bure pengine
ndiyo maana hakukuwa na kelele za namna hii lakini sasa hivi imekuwa ni
biashara.
“Chama change, kwa mfano, tunalipa karibu shilingi
milioni moja au zaidi kwa mwezi kwa ajili ya kuchinjiwa, sasa hii ni biashara
kubwa ndiyo maana hata serikali inatakiwa kuliangaliwa kwa umakini mkubwa suala
hili si kulichukua juu juu tu kama inavyofanya, kwa sababu yakiingia masuala ya
kibiashara inakuwa si haki kusema wengine wana haki na wengine hawana haki”
alisema.
Ndikillo, Wassira wanyooshewa kidole
Mtazamo wa wengi ni kwamba suala hili limefikishwa hapa
lilipo na serikali yenyewe hasa kauli zilizokuwa zikitolewa na Mkuu wa Mkoa
Ndikillo huko Nyehunge wakati wa sakata hilo na kitendo cha Waziri Wassira
kuunga mkono ikaonekana anakubaliana na kila kitu alichosema Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza.
“Hili suala limekuzwa na Mkuu wa Mkoa na kauli zake za
kejeli na dharau, alipokuja Nyehunge wakati wa mazungumzo ya mvutano ule, badala
ya kutulia na kulichunguza jambo kwa undani alipoona hakuna maelewano alitoa
amri tu kwa Polisi kuwa mkristo yeyote akichinja tia ndani, hilo liliwakwaza
viongozi wa kikristo, uhalali wa amri hiyo ulikuwa unatokana na sheria ipi?”
anahoji Mwinjilisti Ernest Charles wa Kikundi cha Biblia ni Jibu ambaye
alishiriki katika kikao hicho.
Akizungumza na Raia Mwema mzee mmoja kutoka Nyehunge
ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kuwa tangu aanze kujitambua hajawahi
kuona kiongozi anashughulikia suala la mgogoro wa dini kwa jinsi alivyofanya
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
“Mwanangu mimi sasa nina miaka 74, viongozi huwa
wanakuwa na hekima na busara. Watu wakifarakana kwenye mambo ya dini yanatakiwa
mazungumzo ya muda mrefu.
“Mkuu wetu alipokuja kwa kufoka na kutoa amri hapo
aliharibu. Mambo haya yanatakiwa watu wakae na kuyazungumza tena na tena,”
alieleza mzee huyo.
Chimbuko la mgogoro
Pengine Mwezi Mei mwaka jana ndiyo unaweza kuelezwa kuwa
ndipo vuguvugu hili lilipoibuka wakati wa mazishi ya mzee Kamuli ambaye alikuwa
muumini wa Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT)
Nyehunge.
Inaelezwa katika msiba huo ya kuwa mchungaji wa eneo
hilo, James Lutambi, alichinja ng’ombe kwa ajili ya msiba huo.
Inaelezwa ya kuwa waislamu waliohudhuria msiba huo
walipofika walihoji nani amechinja, wakaambiwa ni mchungaji. Wakataka kujua
kwanini amechinja, yakatokea majibizano kidogo lakini waislamu hao waliondoka na
kisha wakamwandikia mtendaji wa kijiji barua ya kutangaza kujitenga kushirikiana
na wakristo katika misiba na sherehe, baada ya tangazo hilo, wakristo nao
wakaamua kuwa na bucha yao.
Agosti 27, 2012 Umoja wa Wakristo Nyehunge ulimwandikia
barua Afisa Mifugo wa Wilaya yenye kumbukumbu namba UMK/ NY/01/05 wakiomba
idhini ya kuchinja katika machinjio ya Nyehunge.
Katika kujibu barua hiyo Afisa Mifugo alimwandikia
mtendaji wa kijiji cha Nyehunge barua yenye kumbukumbu namba
VYE/SENG/V.10/11/131 ya tarehe 02, Oktoba 2012 akimtaka kuitisha vikao
vitakavyosaidia kupatikana muafaka juu ya uchinjaji wa wanyama katika machinjio
ya Nyehunge, ambayo iliambatana na ufafanuzi mbalimbali wa kisheria kuhusu
uchinjaji.
“Uchinjaji na ukaguzi wa wanyama kwa ajili ya kuuza kwa
wananchi unafanyika chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 pamoja
na kanuni ya mwaka 2007. Kifungu cha 7 sheria inatamka kuwa uchinjaji wa wanyama
kwenye machinjio zilizoidhinishwa na serikali unafanywa kwa misingi ya imani za
kidini inayokubalika na jamii husika. Sheria na kanuni zake haitamki wazi
muumini wa dhehebu gani aruhusiwe kuchinja wanyama kwa lengo la kuuzia wananchi,
kwa mantiki hiyo hakuna muumini wa dhehebu fulani aliye na haki ya kisheria
kuchinja isipokuwa pale jamii husika inapokubaliana” ilieleza sehemu ya barua
hiyo iliyotiwa saini na Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo Dk. Yohana
Sagenge.
Katika kile kinachoonyesha kikao hicho kutozaa matunda
wakristu waliendelea kwenda kuchinja lakini walikutana na kikwazo machinjioni
ambako afisa aliyekuwa anahusika na kukagua nyama machinjioni alikataa kukagua
iliyochinjwa na wakristo na hivyo wakaamua kuiuza hivyohivyo. Baada ya wakristo
kuanza kuchinjia huko waislamu wakasusa kutumia machinjio hayo wakwa wanachinjia
nje.
Ilipofika hapo Mkuu wa Wilaya ya Sengerema akaingilia
kati na kutangaza wenye haki ya kuchinja kwenye machijio hayo ni waislam,
wakristo wakaweka msimamo wa kuendelea kuchinja hali hiyo ikiwalazimu Polisi
kuingilia kati na kufunga machinjio hayo kwa muda wa mwezi mmoja.
Baada ya wafanyabiashara ya nyama kulalamika, Mkuu wa
Wilaya ya Sengerema akaitisha kikao kingine na wachungaji ambacho kilikaa kwa
zaidi ya saa kumi lakini hakikupata muafaka.
Katika kikao hicho akasisitiza kuwa kwa sasa wenye haki
ya kuchinja ni waislam na kama wakristo wakitaka kuchinja wasubiri katiba
mpya.
Mgogoro ulipoendelea ndipo alipolazimika kwenda Mkuu wa
Mkoa ambaye ni kama alikwenda kuwasha moto zaidi badala ya
kuutuliza.
Inaelezwa na baadhi ya wananchi wa Nyehunge kwamba
Desemba 31, 2012 mchungaji Paul Range wa kanisa la EAGT alikamatwa na Polisi na
kuwekwa mahabusu kwa kosa la kuchinja ng’ombe machinjioni na mwenye ng’ombe
aliyechinjwa naye aliwekwa mahabusu kwa kosa hilo hilo.
Tukio hilo lilisababisha pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
kuamuru Mtendaji wa Kijiji cha Nyehunge kufukuzwa kazi kwa kushindwa kudhibiti
uchinjaji huo.
“Ndiyo maana ninakwambia Mkuu wa Mkoa amechangia sana
kulikuza hili. Mchungaji alikamatwa kwa sababu ya maelekezo aliyotoa siku ya
mkutano na hili likaibua hisia kali kwa watu ndiyo maana tuko hapa leo,” anasema
Mwinjilisti Charles.
No comments:
Post a Comment