Wednesday, June 23, 2010

MASHABIKI WA MPIRA (11/6/2010 - 11/7/2010) MKUMBUKENI MUNGU

SHAIRI HILI LIMEANDIKWA NA MTUNZI TOKA ARABIA NA KWA KUWA NI MAWAIDHA, KARIBUNI TUYASOME NA KUYAZINGATIA KIPINDI HIKI AMBAPO KOMBE LA DUNIA LA SOKA LINASHINDANIWA HUKO AFRIKA YA KUSINI TANGU 11/6/2010 HADI 11/7/2010.

Imehifadhiwa humu kwa hisani kubwa ya Bi. Saada Al-Ghafry wa Muscat, Oman, 23/6/2010.

Mashabiki Wa Mpira

Abdallah Bin Eifan ( Jeddah , Saudi Arabia )

Salamu nawarushia, kama mvua nchini,

Na hali kuwajulia, ni wajibu wa kidini,

Nyote nawasalimia, toka huku Arabuni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Mashabiki nawaambia, tukumbuke ya mwishoni,

Tutakuja kujutia, majuto yafaa nini?

Mapema kuangalia, tudiriki maishani,

Dini yetu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Firimbi imeshalia, mpira upo mguuni,

Watu wanashangilia, hekaheka uwanjani,

Na wengine wanalia, mashaka tupu usoni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Sasa nawahadithia, mechi ndani ya medani,

Hapa nawatangazia, nipo sasa redioni,

Naomba kunisikia, masikio yategeni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Ronaldo kampasia, kanyang’anywa na Oweni,

Ona anavyokimbia, aelekea golini,

Hatari sana sikia, kipa yupo mashakani,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Anazidi kusogea, Ronaldo angalieni,

Lakini ameotea, mpira simamisheni,

Na hapo anarejea, nyuma ashike foleni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Kaingia Maradona, na wote wapo mbioni,

Sasa anapiga kona, huo mpira angani,

Na kipa hakuuona, umeshaingia ndani,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Wengine wanalizana, na wengine furahani,

Wanazidi kukazana, wameshafika pembeni,

Huku wanaumizana, refa kasema chezeni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Sasa anaonekana, ameingia Zedani,

Kaanza kuwatukana, na kuwapiga kichwani,

Refa kasema hapana, huyu nje mtoeni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Manchester na Liverpooli, tupo kwenye ushindani,

Chelsea na Arsenali, na hizi zipo kundini,

Na timu ya Brazili, Amerika ya Kusini,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Hizi ni timu za nje, sio za hapa nyumbani,

Sasa zinatuwashaje, pilipili za shambani,

Tena umewajuaje, wa Ulaya uzunguni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Nani leo huwataja, wachezaji wa zamani,

Ali Kajo na Elija, Kadenge-Kenya nchini,

Kalibala alikuja, toka Uganda yakini,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Zama zile za awali, Tanganyika kubaini,

Alikuwa Salum Ali, mchezaji kwa makini,

Okoth kipa mkali, asomjua ni nani ?

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Watu hutiana ngumi, damu hutoka puani,

Bima milioni kumi, haramu hiyo oneni,

Inaharibu uchumi, bora wape masikini,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Wakivaa kaptura, wapo wazi mapajani,

Vazi halina sitara, wapo uchi hadharani,

Hii sasa ni izara, haramu tupu machoni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Ninasikia adhana, kwa mbali msikitini,

Tumeghafilika sana, yupo na sisi shetani,

Sasa hapa tunaona, haramu wazi jamani,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Wanawake, wanaume, wapo pamoja jukwani,

Huku ni kwenda kinyume, kinyume na yetu dini,

Acha mashekhe waseme, haramu jiepusheni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Hakuna alokataza, mazoezi ya mwilini,

Wameruhusu kucheza, mipaka msivukeni,

Swalah zitimizwe kwanza, kwa wakati tazameni,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira

Tusidharau ibada, hakuna cha samahani,

Tazama yenye faida, akhera na duniani,

Ujiepushe na shida, na ghadhabu Za Manani,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Viwanja vya kuchezea, vinakalifu thamani,

Wakati unapotea, na pesa mabilioni,

Adui anachochea, “umma wapotezeni,”

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

Mpira umeshakwisha, nawaaga kwaherini,

Shetani katubebesha, madhambi tupu shingoni,

Na swalah zimeshakwisha, wameswali Waumini,

Dini yenu kumbukeni, Mashabiki wa Mpira.

No comments:

Post a Comment