Imebandikwa hapa leo hii tarehe 28/10/2012.
SHUGHULI ZA HIJJA SAUDI ARABIA - Mchango wa Dada Saada Al Ghafry wa Muscat, Oman.
Hajj imekuwa na zahma sana siku hizi, na kila serikali
ya Saudia ikiongeza huduma za kila aina, ndivyo zahma inaongezeka. Hivyo
siku hizi mtu hawezi tu kujiendea Hijja peke yake bila kujiandikisha.
Waishio Makkah wanaweza kufanya "Umra", hajj ndogo,
dakika yeyote watakayo kwa sababu wanarudi majumbani mwao kulala. Lakini
Hajj haifanyiki Makka tu, na kwa hujjaji aliyekwisha kufanya Umra,
(Hajj ndogo) hana haja ya kulala Makka hata siku moja.
Hajj inaanza kwa
kulala Mina, kilomita chache kutoka Makka - wengi wanaijua Mina kama
"The Tent City" kwa kuwa Mahujaji wengi wanalala kwenye mahema katika
hizo siku 5-6 za Hajj. Siku kama ya leo, tarehe tisa ya mwezi uuitwao
Dhul-Hijja, mahujaji wooote wanakwenda Arafat, nako kilomita chache
kutoka Mina ambako wanasimama wakiabudu kuanzia asubuhi mpaka jua
likizama, kisha woooote wanakwenda Muzdalifa, ambako wanasali na kulala
sehemu ya wazi kabisa hakuna nyumba wala hema. Baada ya sala ya
Alfajiri, woooote wanarudi Mina, wanarusha mawe kwenye Jamaraat na
kuchinja, kisha wanaoga na kuelekea Makka kuzunguka Ka'aba (kitendo
hicho kinaitwa "Tawwaaf Ifaadha" (kuzunguka Ka'aba), na kurudi Mina moja
kwa moja.
Kwa sababu ya msongamano wa malazi, usafiri na
huduma za chakula na maji, serikali inalazimika kujua ni wangapi
watakaohiji ili kila mmoja huduma hizo zipatikane bila matatizo.
Serikali imelazimika kupata msaada wa wakandarasi wa Hajj ambao nao pia
lazima wawe na usajili na kibali cha ukandarasi. Usajili wa mahujaji
unamalizika mwezi kabla ya Hajj kutoa fursa kwa serikali ya Saudia
kukamilisha matayarisho yanayolingana na idadi iliyosajiliwa.
Tukirudi kwenye swali lako: Laa, aishie Makka hawezi
kukurupuka tu na kwenda Hajj kila mwaka akitaka bila usajili. Kwa
ujumla, ingawa si wote, lakini wengi wao huondoka mjini kuwaachia malazi
watokao kila kona za dunia, Umra rukhsa wakati wote, Hajj lazima kwa
usajili, Kama leo, kwa sababu Hajj ni weekend, si chini ya wakazi wa
Saudi nao watateremka Hajj. Leo alfajiri nimeona wengi wakiitamari
(wakifanya umra) kabla na baada ya sala na wakimaliza wanaelekea Arafat
moja kwa moja. Wengi wao wakimaliza Tawwaaf Ifaadha wataondoka kurudi
makwao tayari kuingia mgodini Jumamosi. Hao wanakuwa wanajitayarisha
kulala ovyo "rough" wakiwa na mahitaji yao yote kama wanakwenda weekend
camping. Ila siku hizi waliokuwa wanalala chini ya madaraja hawaruhusiwi
tena maana ni hatari kwao na kwa mahujaji wengine, polisi hupita na
kuwahamishia sehemu za usalama. Ukikwaji wa utaratibu namna hii,
unaongezea polisi mzigo usio lazima.
Lakini binadamu anakatazika? Wapo wanaokikuka taratibu, lakini rukhsa hawana...