Imeandikwa na Neema Kidumba, MIJO, Mbeya; Tarehe: 10th March 2011 Habari Leo
TANZANIA.
MTU anayetarajiwa kuepusha madhila kwa mwingine kutokana na taaluma yake kumbe anaweza akafanya kinyume chake na kuwa chanzo cha madhila hayo.
Taswira hiyo ndiyo imejitokeza mkoani Mbeya ambapo daktari ambaye alitarajiwa kuwa mwadilifu na kuhakikisha hasababishi matatizo kwa si tu mgonjwa lakini hata mtu mzima, ameshindwa kufanya hivyo.
Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Wazazi Meta mkoani hapa, Moses Achiula (57) ndiye aliyefanya hayo na hatimaye kujikuta akianza kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiuka maadili yake.
Dk Achiula amepatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11 na kumwambukiza virusi vya Ukimwi(VVU).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa, Michael Mteite ambaye alisema Mahakama pia imemwamuru daktari huyo kulipa faini ya Sh. milioni mbili.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na waendesha mashitaka, mawakili wa Serikali Giriffini Mwakapeje na Francis Rojas, kuwa mshitakiwa alibainika kufanya kitendo hicho Januari 21 mwaka jana.
Kwa mujibu wa madai ya waendesha mashitaka hao, Dk. Achiula alikuwa akimfanyia msichana huyo kitendo hicho mara kwa mara na siku aliyothibitika, ilikuwa ni mara ya tatu.
Ilielezwa kuwa mshitakiwa alikuwa akimwita msichana huyo anayesoma darasa la nne nyumbani kwake eneo la Forest jijini hapa na kumwomba amfanyie usafi katika nyumba aliyokuwa akiishi peke yake.
Lakini inadaiwa kuwa baada ya mtoto huyo kumaliza shughuli aliyoombwa kuifanya, daktari huyo alikuwa akimlazimisha kufanya naye ngono.
Waendesha mashitaka hao walidai kuwa daktari huyo pia alikuwa akimwambia mtoto huyo akiona wazazi wake wakiondoka, aende nyumbani hapo na kumtisha kuwa asipokwenda, atamwua.
Wakati akitenda unyama huo kwa msichana huyo mdogo ambaye kiumri ni sawa na mjukuu wake, inadaiwa daktari huyo alikuwa akimtishia kumpiga iwapo angelia au kupiga yowe kuomba msaada.
Waendesha mashitaka walidai kuwa baada ya kumaliza kumfanyia unyama huo, daktari huyo alikuwa akimpa fedha kidogo, ili asieleze kilichokuwa kikiendelea kwa mtu yeyote.
Ilidaiwa kuwa siku ya kwanza, daktari huyo alimpa Sh. 1,000, siku ya pili Sh. 500 na siku ya tatu Sh. 200 na ndipo msichana huyo alipoamua kutoa siri kwa wazazi wake waliochukua hatua za kisheria.
Walisema baada ya wazazi kulifikishwa suala hilo panapostahili, msichana huyo alipelekwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya uchunguzi na kukutwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa vikiwamo virusi vya Ukimwi.
Hakimu Mteite alisema ametoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya daktari huyo.
Saturday, March 12, 2011
Subscribe to:
Posts (Atom)