Thursday, February 25, 2010

ABOUBAKAR RASHID WA MIVUMONI KUMI BORA

Imetoka: MWANANCHI, 22/2/2010 NA ABEID POYO.

Abubakar:Yatima aliyechomoza wanafunzi kumi bora kidato cha nne

ALIPOJITAMBUA hana baba wala mama, aliichukulia elimu kuwa tumaini na mkombozi pekee wa maisha yake.

Hivi ndivyo Abubakar Rashid (16) mwanafunzi kinara wa masomo ya Sayansi aliyeshika nafasi ya sita kitaifa katika mtihani uliopita wa kidato cha nne anavyoelezea maisha yake kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Abeid Poyo

Swali: Wasomaji wetu wana shauku ya kujua matokeo yako yalivyokuwa?

Jibu: Kuhusu matokeo yangu ya kidato cha nne nimepata daraja la kwanza kwa pointi 1.8 nikiwa na alama A katika masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia, Kifaransa, Maarifa ya Uislam, na Kiarabu.

Pia nimepata alama B katika masomo ya Kiingereza, Uraia, Kiswahili na Jografia. Haya ndiyo matokeo yaliyonifanya niingie katika orodha ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri kitaifa huku mimi nikishika nafasi ya sita.

Swali: Ulijisikiaje ulipogundua siyo tu ulifanya vizuri lakini Baraza la Mitihani lilikuchagua kuwa miongoni mwa wanafunzi bora?

Jibu: Baada ya matokeo kutangazwa sikuamini kama nimeweza kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora hii inatokana na uchanga wa shule yangu ya Mivumoni. Unajua sisi ndiyo wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne halafu kuna shule nyingi kongwe zenye rekodi nzuri za kitaaluma hawajatoa mwanafunzi katika 10 bora.

Pia nilikuwa na furaha kubwa kwani ndoto zangu zilitimia na zile kauli za walimu wangu kuwa naweza kufanya vizuri zilithibitika. Nakumbuka nilijiuliza nimweleze vipi bibi yangu ili ajue namna nilivyofaulu ili apate faraja na pia nidhihirishe thamani yangu kwake.

Swali: Umesema shule uliyosoma ni ngeni na nyinyi ndiyo wahitimu wa kwanza, umewezaje kufanya vizuri kwa kiwango hiki?

Jibu: Shule yangu imechangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio yangu. Kwa hakika huwezi kuzungumzia mafanikio yangu bila kuizungumzia Mivumoni Islamic Seminary.Tulikuwa na walimu wazuri, wenye ari na moyo wa kujituma huku wakifundisha kwa ufanisi mkubwa.

Hii shule iliweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunafaulu ikiwemo kufanya mitihani mingi ya ndani, mitihani ya ushindani na shule nyingine, kambi yakujisomea na kwa sisi wanafunzi wa sayansi tulifanya practical (mazoezi ya vitendo) ya kutosha.

Swali: Tukiiacha shule na walimu wako, tueleze siri binafsi ya mafanikio yako?

Jibu: Kwa kweli siri kubwa ni kuwa na nidhamu bora, hii inajumuisha kushirikiana vema na wanafunzi wenzangu, kufuata ushauri wa walimu na walezi wangu na wanajamii wazuri kwa ujumla.

Nilisoma kwa bidiii nikiwa na nia ya kujiondoa katika umaskini ili niweze kuja kuwakomboa mayatima wenzangu na kuliokomboa taifa langu kutokana changamoto mbalimbali zinazozikabili jamii za Kiafrika.

Katika maisha ya shule sikuwa na muda wa kujihusisha na vikundi viovu au kukaa vijiweni.Pia niliepuka mambo yanayopunguza ufanisi wa kusoma kama kuwa na marafiki wa kike, kuangalia picha za ngono na mengineyo.

Swali: Kusoma kuna mikiki mikiki mingi, wewe ni yatima uliwezaje kusoma bila ya usimamizi wa wazazi?

Jibu: Pamoja na kuishi katika mazingira magumu ya kukosa wazazi na kuwa na mlezi hohehahe, maendeleo yangu kitaaluma yalikuwa mazuri sana.Hali hii ilichangiwa na malezi bora ya bibi aliyekuwa akinipa nasaha bila kujali umri wangu mdogo hivyo akili yangu ilipevuka nikiwa bado mdogo.

Kwa mfano niliamini kuwa mafanikio yangu kitaaluma ndiyo chachu ya mafanikio maishani mwangu na kuwa umaskini wangu hautakiwi kunikatisha tamaa badala yake uwe changamoto ya kusaka mafanikio.

Swali: Ukimtoa bibi kuna wengine waliokusaidia na kwa vipi?

Jibu: Naomba niwashukuru walimu wa shule ya msingi Ali Hassan Mwinyi walionivumilia kusoma nikiwa na madeni mpaka namaliza.

Kwa kuwa hawakutaka kuona ndoto zangu zinaishia hapo, mwalimu mkuu aliueleza wasifu wangu kwa uongozi wa msikiti wa Mtambani waliochukua jukumu la kunilea na kunisomesha.

Hii ilinisaidia kwani matatizo yalibaki kwa bibi aliyeendelea kupata mahitaji ya lazima kwa tabu na mara nyingi nilitumia pesa za walezi wangu kununua chakula nyumbani na hili nalifanya mpaka hivi sasa.

Kwa uongozi wa msikiti wa Mtambani wanaonilea mpaka hivi sasa sijui naweza kuwaambia nini, labda niwashukuru na kuwaomba kuwa waendelee na moyo wa aina hii kwa watoto wengine zaidi wanaohitaji misaada.

Swali: Kuna madai kuwa Hisabati ni somo gumu, nini mtazamo wako?

Jibu: Gumu kivipi? mbona tuko wengi tuliopata A nchini?. Mimi maoni yangu ni tofauti kidogo na madai hayo. Mimi nasema Hesabu sio somo gumu isipokuwa wanafunzi wengi aidha hawazijui ama hawazifuati kwa makusudi zile mbinu za kufaulu hesabu nikiwa na maana hawafanyi vile ambavyo hesabu inawataka wafanye.

Swali: Una maana gani unaposema wanafunzi hawafanyi vile ambavyo hesabu inawataka wafanye?

Jibu: Labda nitoe mifano miwili, hesabu inahitaji mazoezi mengi kila unapomaliza mada fulani, sasa wanafunzi wengi hili hawalifanyi na lingine hesabu si somo la kusubiria mtu ulisome wakati wa mitihani. Unalizimika kila siku ufanye hesabu mbalimbali ili uweze kujua mbinu na mitego yake.

Swali:Baada ya mafanikio haya, nini matarajio yako kielimu kwa siku za baadaye?

Jibu: Binafsi natarajia kusomea ualimu wa masomo ya Hisabati na Fizikia na malengo yangu ni kuwa karibu na vijana ili niweze kuwafunda wawe wazalendo kwa nchi yetu Tanzania.

Nikiwa mwalimu nataraji kuanzisha taasisi za kielimu kama vile shule za msingi na sekondari zitakazotoa elimu kwa watoto yatima na wale wa maskini.Lakini pia nahitaji kushiriki katika kampeni za kuongeza wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi nchini na kisha waje kufaulu vizuri ili kuondoa yale madai kwamba masomo ya sayansi na hesabu ni magumu.

Ualimu ni kazi niipendayo na hilo linathibitishwa na historia yangu tangu nikiwa shuleni kwani nilikuwa nawafundisha wenzangu na niliwaomba walimu niwe nawafundisha wanafunzi wa mdaraja ya chini hususan somo la Hesabu na pia kuwapa mbinu mbalimbali za kufaulu.

Kwa sasa nipo shuleni naendelea kuwaongoza wanafunzi wa kidato cha nne katika mijadala na vikundi vya masomo ya sayansi na mengine ili kuwapa mbinu za usomaji na kuwatatulia matatizo ya kitaaluma yaliyo ndani ya uwezo wangu.

Swali: Unatoa wito gani kwa watoto yatima wengine wanaopata fursa ya kusomeshwa na wafadhili?

Jibu: Napenda kuwashauri watumie vizuri fursa hizo kwani wapo wengi wanaozihitaji lakini hawazipati.Nawashauri wamg'ang'anie mkombozi elimu kwani mayatima wengine na jamii

wanatutazama,waache kuiga tabia za ajabu zilizo kinyume na tamaduni za Kiafrika kwani kufanya hivyo ni kupoteza mwelekeo katika maisha yao.

Swali: Tueleze kwa ufupi kuhusu maisha yako?

Jibu: Wazazi wangu walifariki nikiwa na umri mdogo kwa mfano baba alifariki nikiwa sina ufahamu wa kutosha hivyo sijaonja ladha ya malezi ya baba hasa ninapokuwa na matatizo.

Mama alifariki mwaka 2003, kifo chake kiliniathiri sana nilijiona kama kiumbe tofauti niliyeibuka kutoka kusikojulikana.Wenzangu niliwaona wazazi wao lakini wa kwangu hawapo. Ugumu wa maisha uliongezeka na mlezi wangu wa kwanza ambaye ni bibi alikuwa mjane asiye na chochote.

Kiujumla tangu nikiwa mdogo hali ya maisha katika familia yetu ilikuwa ngumu.Alipofariki mama hali ikawa ngumu zaidi, bibi akishindwa kunilipia ada na mahitaji mengine, tukawa mimi na bibi tunaenda kuomba kwa wenye fedha.Tulikuwa tunakosa na mara nyingine tunapata fedha zisizotosheleza mahitaji.

Anachosema mlezi (Sheikh Abdallah Mohammed Ally)

Abubakar ni kijana wa ajabu, mara zote alikuwa changamoto kwa wenzake. Nilitambulishwa kwake alipomaliza darasa la saba na mtu aliyemsaidia sana elimu ya msingi akawa hana uwezo wa kumsaidia tena.

Tulichukua kwa kuwa hii ndiyo kazi ya vituo kama kama hivi. Tutaendelea kumlea na wala hatuzuii wengine kuja kutusaidia kumwendeleza.

MWALIMU NA MWANAFUNZI WAKE

Mwalimu na mwanafunzi wake


Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Tembelea http://mawaidha.info



Baada ya kumsomesha muda usiopungua miaka 30, Sheikh alimuuliza mwanafunzi wake:

"Umejifunza nini kutoka kwangu miaka yote hii?"

Mwanafunzi akajibu:

"Kusema kweli sikujifunza isipokuwa machache tu."

Sheikh akasema kwa mshangao:

"Nimekusomesha muda wa miaka 30, kisha unaniambia hukujifunza isipokuwa machache tu! Haya nielezee hayo machache ni yepi?"

Mwanafunzi akasema:

"Niliuangalia ulimwengu, nikaona kila kitu kinmahitajia wa kukiendesha. Kisha nikawaaangalia wanadamu, nikawaona wanawategemea wengine wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Na nilipofahamu kutoka kwako ewe ustadhi wangu kuwa hapana kinachoweza kuwepo bila ya Mwenyezi Mungu kutaka, nikaacha kumtegemea ye yote isipokuwa Mwenyezi Mungu."



Sheikh akasema:

"Enhe? Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawaangalia viumbe. Nikaona kila mmoja ana kipenzi chake. Wanaishi pamoja, wanacheza, wanasafiri na kurudi pamoja katika safari zao zote. Lakini katika safari ile ya mwisho, mtu anapowasili kaburini pake, anaingia kule ndani peke yake, na vipenzi vyake vyote vinabaki nje. Hawawezi kumfuata. Nikaona bora nijaalie kipenzi changu kiwe amali zangu njema ili ziwe pamoja nami nitakapokuwa kaburini peke yangu."



Sheikh akasema:

"Ahsante! Ehe? Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawaangalia wanadamu. Nikawaona kila mmoja pesa ikishaingia mkononi mwake haitoki. Watu wake wenye shida hawapati haki zao. Masikini hawapati haki zao. Kisha nikatafakari juu ya maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Nahl aya ya 96 isemayo:

مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللّهِ بَاقٍ

"Mlivyonavyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu (vya jaza yenu) ndivyo vitavyobakia."



Nikawa kila kinachoingia mikononi mwangu hukitoa ili kipate kubaki huko kwa Mwenyezi Mungu."



Kwa kukifafanua zaidi kifungu hiki, tuangalie namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alivyokuwa akitoa.

Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) baada ya kuchinja mbuzi na kuigawa nyama yote alimuuliza Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) kama bado pana chochote kilichosalia. Bibi Aisha akasema:

"Limebaki hili bega tu."

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akamsahihisha kwa kumuambia:

"Bali ile tuliyoigawa ndiyo iliyobaki ewe Aisha."



Katika hadithi nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Kipo kingine unachofaidika nacho katika mali yako isipokuwa kile unachokula kikaoza tumboni na unachokivaa kikachakaa na unachotoa sadaka kikabaki?"



Sheikh akasema:

"Enhe, endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Nikawatizama viumbe. Nikawaona kila mmoja anamuonea husuda mwenzake kwa kile alichokipata. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Zukhruf aya ya 32 yasemayo:

أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَةَ رَبِّكَ نَحْنُ قَسَمْنَا بَيْنَهُم مَّعِيشَتَهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَرَفَعْنَا بَعْضَهُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ

"Je, wao wanaigawa rehema ya Mola wako (wakampa wampendae na kumnyima wamtakae?) Sisi tumewagawiya maisha yao katika uhai wa dunia na kuwainua baadhi yao daraja kubwa juu ya wengine."



"Nikaacha kuwahusudu viumbe”.

Sheikh akasema:

"Ahsante. Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawatizama wanadamu. Nikaona tonge imewadhalilisha na kuwafanya wapige mbizi katika mambo ya haramu. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Surat Hud aya ya 6 ِAliposema:

وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

"Na hakuna kiumbe cho chote katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu.Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu)."



Nikafahamu kuwa riziki yangu hawezi kuichukua mwengine, na hapo moyo wangu ukatulia. "



Katika kukisherehesha kifungu hiki tuzingatie maneno ya Hassan Al-Basri (Radhiya Llahu anhu) mmoja katika Maulamaa wa At-Tabiina. (waliowaona Masahaba (Radhiya Llahu anhum) lakini hawakumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam).

Hassan Al Basri alisema:

"Nilipotambua kuwa amali zangu hawezi kunifanyia mwengine, nikapania kuzifanya mwenyewe. Na nilipotambua kuwa riziki yangu hawezi kuichukuwa mwengine, moyo wangu ukatulia. Na nilipotambua kuwa Mola wangu ananiona, nikaona haya asije akaniona nikiwa katika hali ya kumuasi.”



Wasalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh